Aisha Masaka Mtanzania anayebeba matumaini BK Hacken
WIKI iliyopita wadau wa soka la Tanzania walipokea habari njema za mchezaji kinda wa kike, Aisha Masaka kuula huko Sweden ambako alitambulishwa, Alhamisi na kuanza rasmi mazoezi ikiwa ni siku chache mara baada ya kutua Gothenburg.
Aisha amejiunga na wababe hao wa soka la wanawake huko Sweden akitokea Yanga ya Tanzania baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili ambao unatarajiwa kufikia tamati 2024 huku kukiwa na kipengele cha kuongezewa mwaka mwingine mmoja kulingana na kiwango chake.
Hatimaye Aisha hayupo ndotoni tena. Yale maisha ambayo alikuwa akiyaota ya kucheza soka la kulipwa kama ilivyotokea kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, yametimia kiasi cha kuonekana kuwa mwenye furaha muda wote wakati wa utambulisho wake.
Kwa sasa anakuwa mchezaji wa kwanza wa kike ambaye atacheza ligi yenye ushindani mkubwa zaidi ukilinganisha na wengine ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi kama vile Opah Clement (Yukatel Kayserispor, Uturuki), Mwanahamisi Omary (SCCM, Morocco), Tatu Salum (Thika Queens, Kenya), Enekia Lunyamila na Diana Msewa wote wa AUSFAZ ya Morocco.
Mbali na BK Hacken kuwa inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake huko Sweden, imekuwa ikishiriki pia Ligi ya Mabingwa Ulaya na msimu huu waliishia hatua ya makundi, walikuwa kundi moja (D) na Lyon, Bayern Munich na Benfica.
Ugumu wa kundi hilo, uliwafanya kumaliza nafasi ya mwisho wakiwa na pointi tatu huku zikishuhudiwa, Lyon na Bayern zikitinga hatua ya robo fainali.
Kwa sasa michuano hiyo ipo hatua ya nusu fainali ambapo Lyon waliotoka kundi moja na chama jipya la Mtanzania huyo, itacheza dhidi ya PSG huku Barcelona ikiwa dhidi ya Wolfsburg ya Ujerumani.
MSIKIE KIGOGO
Mara baada ya kukamilika kwa uhamisho wa mchezaji huyo, Mkurugenzi wa michezo wa BK Hacken, Martin Ericsson amesema wanamtazama mchezaji huyo wa Kitanzania kama tunu kwenye klabu hiyo kulingana na umri wake na kile ambacho amekuwa akikifanya.
“Aisha ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa ambaye nina imani kubwa kwamba atasisimua wengi pale ambapo ataanza kucheza. Kiukweli ana sifa zote pamoja na udogo wa umri wake, ana uzoefu mkubwa,”
“Ni mzuri katika kutumia kasi na nguvu kwenye safu ya ushambuliaji na ni mfungaji mzuri. Tuna hakika kwamba ataongeza makali kwenye safu yetu ya ushambuliaji, na tunamkaribisha kwa moyo mkunjufu,” alisema mkurugenzi huyo.
HUYU NDIYE AISHA
Aisha alizaliwa Singida, Tanzania na ametokea Yanga, ambayo ni moja ya timu maarufu nchini. Pia aliwahi kuichezea Alliance Girls FC ya jijini Mwanza.
Msimu wa 2020/2021, alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara akiwa ametupia mabao 35 katika mechi 20. Amefunga mabao 27 katika mechi 14 za timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka U17. Siku hizi amekuwa kicheza kikosi cha wakubwa, Twiga Stars na kwenye michezo minne ametupia mabao mawili.
IFAHAMU HACKEN
Kwa kirefu, inafahamika kama Bollklubben Hacken Fotbollsforening, ni klabu ya soka ya wanawake yenye maskani yake huko Gothenburg, Sweden.
Ilianzishwa mwaka wa 1970 kama Landvetters IF ikiwa ni timu ya wanaume na ikaja kujulikana kama Kopparbergs/Goteborg FC, kati ya 2004 na 2020 ndipo timu ya wanawake ilipoanzishwa lakini kutokana na sababu za kisheria ilibidi kufanyika mgawanyiko kwa timu hizo mbili, kila moja kujiendesha na kujisimamia kivyake.
BK Hacken wanacheza mechi zao za nyumbani kwenye Uwanja wa Bravida Arena huko Gothenburg. Rangi za timu ni njano na nyeusi. Klabu hiyo ilishinda taji lao la kwanza la Ligi Kuu Sweden ‘Damallsvenskan’ mwaka 2020.