Yanga inavyopiga pesa kwa mastaa wake
Muktasari:
- Wakati ushindani wa Ligi Kuu ya Wanawake ukiongezeka msimu huu, Yanga imefanya mwendelezo wa kuuza wachezaji wake muhimu nje ya nchi kisha kunufaika pale wachezaji hao wanapopata ofa kutoka klabu za kimataifa.
IMEKUWA kawaida kwa Yanga Princess kuona ikiuza wachezaji ambao wapo kwenye viwango bora kutafuta changamoto nje ya nchi na kuwa kama daraja la nyota wake kutimkia soka la kulipwa nje ya Tanzania.
Wakati ushindani wa Ligi Kuu ya Wanawake ukiongezeka msimu huu, Yanga imefanya mwendelezo wa kuuza wachezaji wake muhimu nje ya nchi kisha kunufaika pale wachezaji hao wanapopata ofa kutoka klabu za kimataifa.
Hatua hiyo imeifanya klabu hiyo kuwa miongoni mwa timu zinazotengeneza thamani ya wachezaji na kujipatia mapato kutokana na uhamisho.
Mwanaspoti imekuchambulia baadhi ya nyota waliouzwa nje na kuinufaisha timu hiyo.
JEANINNE MUKANDAYISENGA
Hivi karibuni Yanga ilitangaza kumuuza mshambuliaji wake tegemeo, Jeaninne Mukandayisenga kwenda Wuhan Jiangda Women's FC ya China. Ingawa dili hilo halikuwekwa wazi lakini tetesi zinaeleza Yanga imevuta mkwanja mrefu kwa mshambuliaji huyo aliyeibuka mfungaji bora kwenye Ligi ya Wanawake msimu uliopita.
Mukandayisenga alijiunga na Yanga Princess dirisha dogo la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sports ya Rwanda msimu wa 2024/25 ambako tayari alikuwa na kiwango bora na msimu wake wa kwanza alifunga mabao 13 na uliopita alifunga mabao 20.
AISHA MASAKA
Masaka aliitumikia Yanga kwa misimu miwili 2019/20 na 2020/21 na msimu wake wa mwisho aliandika historia kwa kufunga mabao 35 na kumaliza kinara wa ufungaji wa ligi.
Alikuwa mchezaji wa mwisho mzawa kufunga idadi hiyo kubwa rekodi ambayo hadi sasa imeshindwa kuvunjwa ukiwa ni msimu wa saba sasa.
Ubora huo ulimpeleka BK Häcken ya Sweden, huku Yanga ikinufaika kifedha kutokana na kuwa mchezaji huyo alikuwa bado ana mkataba. Baadaye akajiunga na Brighton & Hove Albion ya England ambapo pia ilielezwa wananchi hao waliingiza asilimia 15 kwenye mauzo hayo.
CLARA LUVANGA
Clara Luvanga ndiye mshambuliaji bora kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya Wanawake ya Saudia akiweka rekodi mbalimbali za mabao ndani ya misimu mitatu alioitumikia Al Nassr ya Saudia.
Msimu wake wa kwanza 2023/24 alifunga mabao 11 na asisti saba, huku msimu uliofuata alifunga mabao 21 na asisti saba na msimu huu alimaliza na mabao 24.
Yanga alisajiliwa mwaka 2022 akitokea Mapinduzi baada ya kung'ara kwenye Ligi Daraja la Kwanza na hapo ndipo kocha Edna Lema alimwona akiwa na uwezo mkubwa wa kuwa nyota wa baadaye.
Baada ya kung'ara akiwa Yanga, alihamia DUX Logroño ya Hispania kwa dau lililoripotiwa kufikia Sh51 milioni, huku akipata pia mkataba wenye masilahi makubwa ya mshahara.
Katika mauzo hayo inaelezwa Yanga pia ilipata faida licha ya kutoweka wazi kiasi gani ama asilimia ngapi inapata kwa mshambuliaji huyo.
Mbali na mafanikio ya klabu, Clara amekuwa mmoja wa nyota muhimu wa timu za taifa za wanawake. Aliiongoza Tanzania kufuzu Kombe la Dunia la Wasichana chini ya miaka 17 mwaka 2022 na kuwa moja ya nyota walioweka historia kwa kufika robo fainali India.
CUTA
Winga huyo raia wa Msumbiji alijiunga na Yanga Princess msimu wa 2022/23 akitokea nchini kwao, akacheza jangwani msimu mmoja ambao hakuwa na kiwango bora na alipata ofa kutoka FC Minsk ya Belarus na klabu ikakubali kumuuza Februari 2024.
Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo aliwahi kueleza kuwa falsafa ya Yanga si kuwazuia wachezaji wanapopata nafasi za kucheza nje.
"Soko la wanawake bado ni dogo, hivyo mchezaji akipata nafasi ya kwenda kucheza nje tunampa ushirikiano kwa sababu ni maendeleo yake na pia ni faida kwa klabu," alisema.
BLESSING
Alikuwa mshambuliaji hatari tangu alipoojiunga na Yanga mwaka 2022 akitokea Sunshine Queens ya kwao Nigeria alipokuwa na kiwango bora akifunga mabao 20 kwenye mechi 18.
Ndani ya muda mfupi akawa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa timu hiyo kutokana na uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi.
Yanga alifunga mabao manane na ubora huo uliifanya Gaziantep AsyaSpor ya Uturuki kuvutiwa naye na kumnunua mwaka 2023, huku Yanga ikinufaika na mauzo yake.
Kutoka Uturuki alihamia Deportivo La Coruña ya Hispania kabla ya baadaye kusajiliwa na Dynamo Brest ya Belarus.
MAIMUNA KHAMIS 'MYNACO'
Kiungo Maimuna Khamis 'Mynaco' ni miongoni mwa wachezaji wenye historia kubwa katika soka la wanawake Tanzania.
Baada ya kushinda mataji matano mfululizo akiwa JKT Queens na Simba Queens, alijiunga na Yanga Princess mwaka 2022 kwa matarajio ya kuisaidia kutwaa ubingwa wa kwanza.
Licha ya kutofanikiwa msimu huo, kiwango chake kiliwavutia ZED FC ya Misri na kujiunga nao msimu wa 2024/25 kabla ya kurejea tena Yanga Princess msimu wa 2025/26.
Ingawa safari yake haikuhusisha faida kubwa ya mauzo kama ilivyokuwa kwa wengine, bado ilikuwa sehemu ya mkakati wa Yanga wa kusajili wachezaji wenye thamani kubwa ambao huvutia masoko ya kimataifa.