Hasnath Ubamba Kutoka Fountain Gate hadi Hispania
Muktasari:
- Ubamba aliuzwa kutoka FC Masar ya Misri kwenda Madrid CFF kwenye moja ya klabu zinazoshiriki ligi kubwa duniani na huu ndiyo mwanzo wa vita nyingine ya kutafuta namba, baada ya kushinda mtihani kama huo akiwa kwa Waarabu.
NI ndoto ya baadhi ya wachezaji wa Tanzania kucheza ligi kubwa za kiushindani barani Ulayana wiki hii ilikuwa ni zamu ya kiungo mshambuliaji, Hasnath Ubamba aliyeandika historia mpya kwenye karia yake baada ya kusajiliwa na moja ya klabu kubwa ya Ligi Kuu ya Wanawake Hispania, Madrid CFF.
Ubamba aliuzwa kutoka FC Masar ya Misri kwenda Madrid CFF kwenye moja ya klabu zinazoshiriki ligi kubwa duniani na huu ndiyo mwanzo wa vita nyingine ya kutafuta namba, baada ya kushinda mtihani kama huo akiwa kwa Waarabu.
Katika miaka michache ameonyesha ukuaji mkubwa, akitokea Fountain Gate Princess ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, kwenda Misri na sasa Hispania, moja ya ligi zenye ushindani mkubwa barani Ulaya.
TAKWIMU ZAKE
Kutoka Tanzania hadi Misri wengi waliamini pengine alikwenda kupata uzoefu na kujifunza mazingira mapya, lakini alionyesha kiwango bora kiasi cha kuonyesha upinzani dhidi ya wageni na katika misimu miwili aliyokaa Misri alicheza mechi 50, akifunga mabao 30 na kutoa asisti 19, rekodi iliyomfanya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa FC Masar.
Pia aliiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri mara mbili mfululizo na kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, jambo lililomweka kwenye rada za klabu mbalimbali za Ulaya, ndipo Madrid CFF ilipoamua kutoa nafasi nyingine kwa nyota huyo, hatua inayomfanya kuwa miongoni mwa Watanzania wachache waliowahi kucheza katika Ligi Kuu ya Wanawake Hispania.
MTIHANI ULIOPO
Ligi ya Hispania ni tofauti na ile ya Misri. Kasi ya mchezo, ubora wa wachezaji na ushindani wa namba ni wa kiwango cha juu zaidi kulinganisha na alipotoka.
Ubamba ametua katika Liga F, moja ya ligi mbili bora za wanawake duniani, ambako ushindani wa kupata nafasi ya kucheza ni mkubwa kuliko aliozoea akiwa Misri.
Kinachofanya ligi hiyo kuwa namba mbili kwa ubora duniani ni kasi ya mchezo, ubora wa kiufundi na ushindani wa kupata nafasi ya kucheza lakini hata klabu zinazotoka kwenye ligi hiyo zinafanya vizuri mara kwa mara katika michuano mikubwa ya UEFA.
Kama ataongeza kasi zaidi aliyoonyesha kwenye ligi ya Misri anaweza kuwa moja ya nyota kutoka Tanzania ambao wanaweza kuandika rekodi katika ligi hiyo.
Mfano mzuri upo kwa Mtanzania mwenzake, Opah Clement ambaye licha ya kucheza msimu mmoja Ligi ya Hispania bado amekuwa akipambana kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Eibar.
Hilo linaonyesha wazi mafanikio ya kufika Ulaya ni hatua moja, lakini kujihakikishia nafasi ya kucheza ndiyo mtihani mkubwa zaidi.
ATAVUNJA REKODI
Sasa hivi kumekuwa na ongezeko kubwa la wachezaji wa Tanzania kusajiliwa na klabu kubwa duniani, Ubamba anaongeza idadi hiyo kwenye soka la wanawake.
Wapo kina Opah anayekipiga Hispania, Diana Msewa (Trabzonspor ya Uturuki), Enekia Lunyamila (Querétaro FC Femenil ya Mexico), Aisha Masaka (Brighton, England), Noela Luhala wa MFA Zalgiris ya Lithuania, Clara Luvanga (Al Nassr, Saudia) na wengineo.
Kati ya wachezaji hao Diana, Noela, Clara ndio wamejihakikishia nafasi ya kucheza kwenye timu mara kwa mara wengine wamekuwa wakiingia na kutoka. Hivyo kama Ubamba ataonyesha juhudi za ziada ataongeza idadi ya nyota tegemeo kwenye timu.
Endapo atafanya hivyo, si tu atakuwa amepiga hatua binafsi, bali atafungua mlango kwa wachezaji wengine wa Tanzania kuamini wanaweza kushindana katika ligi kubwa za Ulaya.
HAWA WANAMKABA
Safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ina ushindani mkubwa, baadhi ya wachezaji wameshajitengenea nafasi kutokana na viwango bora wanavyoonyesha kwenye timu.
Baadhi ya wachezaji wenye namba kwenye kikosi hicho ni Mnorway, Emilie Nautnes alikuwa kinara wa mabao kwa klabu hiyo baada ya kufunga mabao saba katika mechi 29.
Mhispania Anita Marcos alifunga mabao sita katika mechi 21 na kuwa miongoni mwa washambuliaji waliotumika mara kwa mara. Pia yupo Mserbia Allegra Poljak, aliyefunga mabao matano katika mechi 26, huku Bárbara López na Alba Ruiz nao wakipata dakika nyingi za kucheza na kuwa sehemu muhimu.
Takwimu hizo zinaonyesha timu hiyo haina washambuliaji hatari kwani kila mchezaji ana nafasi ya kuanza lakini na endapo Ubamba ataonyesha mazoezini atakuwa ana nafasi ya kuanza.
Ubamba atalazimika kufanya kazi ya ziada ili kupenya kwenye kikosi cha kwanza. Hata hivyo, hilo si jambo jipya kwake. Alipotimkia FC Masar ya Misri mwaka 2024 alikuta ushindani kama huo, lakini ndani ya misimu miwili alijihakikishia nafasi ya kudumu, akicheza mechi 50, kufunga mabao 30 na kutoa asisti 19, rekodi iliyomfungulia mlango wa kutimkia Hispania.
Faida kubwa ya Ubamba ni uwezo wake wa kucheza nafasi tofauti katika safu ya ushambuliaji, iwe kama mshambuliaji wa pembeni, kiungo mshambuliaji au nyuma ya mshambuliaji wa kati.
Akiweza kuendana haraka na kasi ya Liga F na kutumia vyema kila nafasi atakayopewa, anaweza kuandika historia nyingine kama alivyofanya Misri na kujihakikishia nafasi ya kudumu Madrid CFF.
MSIKIE MAKAU
Wakati Ubamba akianza safari yake mpya, Fountain Gate Princess inaendelea kuvuna matunda ya uwekezaji wake katika kukuza vipaji na Rais wa timu hiyo, Japhet Mboto Makau anasema klabu hiyo inajivunia kuona wachezaji waliowalea wakisajiliwa na kucheza kwenye ligi kubwa duniani.
"Tunajivunia kuona mchezaji aliyepitia Fountain anafika hatua hii. Haya ndiyo malengo yetu, kutengeneza wachezaji watakaocheza kwenye ligi kubwa duniani jambo linalotupa nguvu ya kuendelea kuwekeza katika kukuza vipaji vingine," alisema Makau.