Aguero awatuliza mashabiki Mlandege
Muktasari:
- Aguero alifafanua kuwa wachezaji wamekubaliana kuongeza juhudi uwanjani, kupunguza makosa madogo yaliyowagharimu katika baadhi ya mechi zilizopita na kupambana kwa dakika zote 90 bila kukata tamaa.
KIUNGO mshambuliaji wa Mlandege FC, Mahmoud Haji Mkonga ‘Aguero’, amesema licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu cha matokeo yasiyoridhisha, kwa sasa wamejipanga kurekebisha makosa yao na kurejesha ushindani.
Amesema kikosi hicho kipo tayari kupambana katika michezo inayofuata na kuhakikisha kinapata ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wake.
Aguero alifafanua kuwa wachezaji wamekubaliana kuongeza juhudi uwanjani, kupunguza makosa madogo yaliyowagharimu katika baadhi ya mechi zilizopita na kupambana kwa dakika zote 90 bila kukata tamaa.
Amesema licha ya Mlandege kupoteza baadhi ya michezo katika Ligi Kuu Zanzibar, bado wanaendelea kujiimarisha kwa lengo la kurejesha kiwango na heshima ya timu hiyo.
“Tunatambua kuwa timu yetu haikuanza vizuri msimu huu, lakini bado tunaendelea kusuka mikakati ya kuimarisha kikosi na kupambana kwa dakika zote 90 katika kila mechi,” amesema.
Kiungo huyo alisisitiza kuwa bado kuna michezo mingi mbele yao, hivyo hakuna sababu ya kukata tamaa kwa kuwa wanaamini wanaweza kubadilisha mwenendo wa matokeo iwapo wataendelea kuwa na nidhamu na kujituma.