Yanga, Azam zapangua ratiba ZPL
Muktasari:
- Mabadiliko hayo yamehusisha baadhi ya michezo ya mzunguko wa 13 na 15, baada ya Yanga na Azam kutumia Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya mechi zao za hatua ya makundi ya CAF.
BODI ya Ligi Zanzibar (ZLB), imefanya mabadiliko katika ratiba ya baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), kufuatia kugongana na mechi za kimataifa za mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Mabadiliko hayo yamehusisha baadhi ya michezo ya mzunguko wa 13 na 15, baada ya Yanga na Azam kutumia Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya mechi zao za hatua ya makundi ya CAF.
Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotolewa na Bodi hiyo, mchezo wa Mlandege dhidi ya Uhamiaji sasa utachezwa Alhamisi, Novemba 26, 2026, saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Mao A, badala ya Novemba 27, 2026 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Siku hiyo pia, Wembe FC itakuwa mwenyeji wa Polisi katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
Katika mabadiliko mengine ya ratiba ya mzunguko wa 13, Muembe Makumbi itakutana na JKU Novemba 29, 2026 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Mao A, huku Raskazone ikiikabili Black Sailor katika Uwanja wa Mao B, Unguja.
Kwa upande wa Mzunguko wa 15, Chipukizi United itamenyana na Wembe Desemba 3, 2026, katika Uwanja wa Gombani, kabla ya Mwenge kukutana na Fufuni Desemba 4, 2026 katika uwanja huo huo.
Michezo mingine ya mzunguko huo itakuwa kati ya Muembe Makumbi dhidi ya Polisi SC, Raskazone dhidi ya Mlandege FC, Black Sailor dhidi ya Mafunzo na Uhamiaji dhidi ya Zimamoto.
Aidha, michezo ya KVZ dhidi ya KMKM na Kipanga dhidi ya JKU itachezwa kati ya Desemba 18 na 20, mwaka huu.
Awali, ratiba ilionyesha kuwa raundi ya Kwanza wa ligi hiyo ingekamilika Novemba 27, 2026, lakini uwepo wa mechi za kimataifa za CAF pamoja na maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2027, umeilazimu Bodi kufanya marekebisho hayo.
Bodi imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuweka uwiano kati ya ratiba ya Ligi Kuu Zanzibar na majukumu mengine ya soka yanayofanyika Zanzibar, huku ikiwataka wadau wa soka kushirikiana na kuwa wavumilivu wakati wa utekelezaji wa ratiba mpya.
Ikumbukwe kuwa, Ijumaa hii Novemba 27, 2026, Azam itaikaribisha Al Ahli Tripoli kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 10:00 ukiwa ni mchezo wa kwanza Kundi B wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Kisha Jumamosi Novemba 28, 2026, Yanga itaikaribisha MC Alger uwanjani hapo saa 10:00 jioni ikiwa ni mechi ya kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika.