Zimamoto yakomaa kileleni
Muktasari:
- Zimamoto imeonyesha kiwango bora msimu huu, ikiwa imeshinda mechi 10, sare moja na kupoteza moja. Katika michezo hiyo, imefunga mabao 18 na kuruhusu sita, takwimu zinazoonyesha uimara wake katika mashindano hayo.
LIGI Kuu Zanzibar msimu wa 2026-2027, imezidi kupamba moto baada ya kukamilika kwa Mzunguko wa 12, huku Zimamoto ikiendelea kukomaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 31.
Zimamoto imeonyesha kiwango bora msimu huu, ikiwa imeshinda mechi 10, sare moja na kupoteza moja. Katika michezo hiyo, imefunga mabao 18 na kuruhusu sita, takwimu zinazoonyesha uimara wake katika mashindano hayo.
Hata hivyo, JKU inaendelea kuifukuzia kwa karibu, ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 27. JKU imeshinda michezo nane, sare tatu na kupoteza mmoja, huku ikiwa imefunga mabao 26 na kuruhusu 12, ikiwa na idadi kubwa zaidi ya mabao kati ya timu tatu za juu.
Polisi inashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 26 baada ya kucheza michezo 12. Timu hiyo bado haijapoteza mchezo, ikiwa imeshinda saba na kutoka sare tano, huku ikiruhusu mabao sita, idadi inayolingana na ya vinara Zimamoto.
Katika nafasi nne za juu, KVZ inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza michezo 12. Bingwa huyo mtetezi anafuatwa na KMKM yenye pointi 20 baada ya kucheza michezo 13, huku Uhamiaji ikiwa nafasi inayofuata kwa pointi 20 baada ya kucheza michezo 12.
Muembe Makumbi City inashika nafasi ya saba kwa pointi 18, ikifuatiwa na Mafunzo yenye pointi 16. Kipanga na Raskazone zinashika nafasi ya tisa na 10 zikiwa na pointi 15 na 14 mtawalia.
Mlandege, moja ya klabu zenye historia kubwa katika soka la Zanzibar, ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza michezo 12. Inalingana kwa pointi na Chipukizi United iliyo nafasi ya 12 pamoja na Wembe inayoshika nafasi ya 13.
Ushindani huo unaonyesha namna vita ilivyo kali katika sehemu ya kati ya msimamo, ambapo tofauti ndogo ya pointi kati ya timu inaweza kusababisha mabadiliko makubwa ya nafasi baada ya kukamilika kwa mchezo mmoja.
Katika eneo la chini la msimamo, Black Sailor FC inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 10, huku Mwenge ikiwa nafasi ya 15 kwa pointi sita na Fufuni SC ikiburuza mkia ikiwa na pointi tano.
Fufuni imecheza michezo 13, ikishinda mmoja, kutoka sare mbili na kupoteza 10. Pia imekuwa na changamoto ya safu ya ulinzi baada ya kuruhusu mabao 24, hali inayoonyesha ukubwa wa kazi inayokikabili kikosi hicho katika harakati za kujinasua kutoka nafasi ya mwisho.
###
ZFF YAJIPANGA KUJENGA OFISI ZAKE
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limeanza hatua za kutafuta na kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi zake, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za soka visiwani humo.
Akizungumzia mipango hiyo, Katibu wa ZFF, Hussein Ahmada Vuai, alisema shirikisho hilo linakusudia kuwa na makao yake ya kudumu yatakayorahisisha utekelezaji wa majukumu yake pamoja na usimamizi wa shughuli mbalimbali za mpira wa miguu.
Alisema ZFF linakusudia kutumia kipindi hiki cha kuelekea kutimiza miaka 63 ya Mapinduzi kuweka msingi imara wa kumiliki eneo na kujenga ofisi zake, hatua ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo.
Vuai alieleza kwamba, kuwa na ofisi za kudumu kutasaidia kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi wa kiutawala na kuweka mazingira bora kwa watendaji wa shirikisho hilo kutekeleza majukumu yao.
Alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za ZFF kujiimarisha kitaasisi na kuweka msingi wa maendeleo endelevu ya soka la Zanzibar katika miaka ijayo.