Kutoka Tanzania hadi QPR, simulizi ya kipekee ya Kealey Adamson
Muktasari:
- Adamson mwenye umri wa miaka 23, alizaliwa na mama mwenye asili ya Ireland na Australia, Shivaun, huku baba yake akiwa Mtanzania. Hata hivyo, kinachovutia zaidi katika historia ya familia yake ni namna wazazi wake walivyokutana, hadithi ambayo imeifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya maisha ya beki huyo.
KUNA simulizi ambazo soka pekee haliwezi kuzisimulia, zinahitaji kuangalia maisha ya mchezaji nje ya uwanja, familia yake na safari iliyomfikisha hapo alipo. Ndivyo ilivyo kwa beki wa kulia wa QPR, Kealey Adamson mwenye asili ya Tanzania, ambaye licha ya kukulia Australia na kucheza soka England, ana uhusiano wa karibu na Tanzania kupitia baba yake, Nickson.
Adamson mwenye umri wa miaka 23, alizaliwa na mama mwenye asili ya Ireland na Australia, Shivaun, huku baba yake akiwa Mtanzania. Hata hivyo, kinachovutia zaidi katika historia ya familia yake ni namna wazazi wake walivyokutana, hadithi ambayo imeifanya Tanzania kuwa sehemu muhimu ya maisha ya beki huyo.
Akizungumza na Football360, Adamson alifichua kuwa baba yake alikutana na mama yake wakati Shivaun alipojiunga na kundi la watalii waliokuwa wakifanya safari ya kutembelea Tanzania. Wakati huo, mama yake alikuwa mwalimu, huku Nickson akifanya kazi ya kuwaongoza watalii.
“Baba alikutana nao kwenye kituo cha mabasi na inaonekana alikuwa mwenyeji mzuri, kwa sababu mama alirudi tena mwaka uliofuata. Kabla hawajajua, tayari walikuwa wameoana,” alisema Adamson.
Hiyo ndiyo simulizi iliyounganisha familia yenye asili ya pande mbili tofauti, baadaye ikampa Adamson mizizi ya Tanzania ambayo sasa anajitahidi kuifahamu zaidi, licha ya maisha yake mengi kuwa Australia na sasa England.
SAFARI YA TANZANIA
Kwa Adamson, uhusiano na Tanzania hauishii katika simulizi za wazazi wake pekee, bali pia ni sehemu ya maisha aliyopata nafasi ya kuishi na kufurahia akiwa na familia yake.
Beki huyo anaeleza kuwa alipata fursa ya kutembelea Tanzania akiwa na mwenza wake, walipotakiwa kuhudhuria harusi iliyokuwa ikifanyika Mombasa, Kenya. Kipindi hicho alikuwa mapumzikoni baada ya kuachana na Sydney FC na kabla ya kujiunga na Macarthur Bulls, hivyo alikuwa na takribani miezi mitano ya uhuru.
“Nilialikwa pamoja na mwenza wangu kwenye harusi huko Mombasa, Kenya, na wakati huo nilikuwa katikati ya kuondoka Sydney FC na kujiunga na Macarthur, hivyo nilikuwa na miezi mitano ya uhuru,” anasema.
Anaeleza kuwa safari hiyo haikuwa ya kwenda Kenya tu, kwani walipata nafasi ya kuwatembelea ndugu zao jijini Dar es Salaam na Zanzibar kabla ya kuendelea na safari ya kuelekea Mombasa.
“Tulitembelea familia huko Dar es Salaam, Zanzibar, kisha tukafanya safari ya barabarani hadi Mombasa. Ilikuwa safari ya kushangaza na nilipata nafasi ya kutumia Kiswahili changu ambacho bado hakijakaa vizuri,”€ anasema.
DARASA LA KISWAHILI
Wakati wachezaji wengi wakitumia muda wao wa ziada kupumzika au kujifunza mambo yanayohusiana na soka, Adamson amekuwa akitumia muda huo kujifunza lugha ya Kiswahili ambayo ni upande wa baba yake mzazi.
Beki huyo anasema ana mwalimu wa kumsaidia kujifunza lugha hiyo kwa miaka mitatu, akilenga kuweza kuzungumza na ndugu zake wa upande wa baba yake, hasa bibi yake.
“Nimekuwa na mwalimu kwa miaka mitatu iliyopita nikijaribu kujifunza lugha ya mama ya baba yangu ili niweze kuwasiliana na familia, kama vile bibi yangu. Hili limekuwa jambo ambalo nimelipenda na kulifuatilia kwa shauku binafsi,”€ anaongeza.
Adamson anaamini kujifunza Kiswahili si suala la kujiongezea ujuzi wa lugha tu, bali pia ni njia ya kuimarisha mizizi yake ya Kitanzania na kuwasiliana vizuri zaidi na watu wa familia yake ambao lugha hiyo ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Anaongeza kuwa anafurahia shughuli inayomtoa nje ya mazingira ya soka, hasa kutokana na maisha ya mchezaji wa kulipwa kuzungukwa na mazoezi, maandalizi ya mechi na mahitaji ya kiufundi.
“Nadhani ni jambo zuri kufanya kitu kinachokutoa kwenye soka mara kwa mara. Ni mojawapo ya mambo machache yasiyohusiana na soka ambayo hunifanya niendelee kuchangamsha akili yangu,” anasema.
QPR, SAFARI MPYA
Wakati akiendelea kujifunza lugha ya baba yake, Adamson naye anaendelea kujenga jina lake katika soka la England akiwa na QPR, inayoshiriki Ligi ya Championship.
Beki huyo wa kulia aliyekulia Sydney, Australia, amekuwa akipata nafasi katika kikosi cha QPR, huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaoweza kuingia katika mipango ya timu ya taifa ya Australia, maarufu Socceroos.
AISUBIRI STARS
Kuhusu utayari wake wa kuichezea Taifa Stars, Adamsoon anasema: “Ni suala la kusubiri kwanza na kuona nini kitatokea mbeleni lakini kwangu sioni tatizo kwa sababu najua Tanzania ni nchi nzuri na watu wake wamekuwa na upendo siku zote na hilo nimekuwa nikiliona pale na huwa naenda kwa ajili ya mapumziko.