Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wachezaji wa Diaspora kuipa nguvu Stars kabla ya AFCON 2027

Muktasari:

  • Timu za ukanda huo zinaenda kuandika historia nyingine kwenye soka baada ya awali kuandaa mashindano ya CHAN.

NCHI tatu za Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda zimepewa ridhaa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuandaa mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani.

Timu za ukanda huo zinaenda kuandika historia nyingine kwenye soka baada ya awali kuandaa mashindano ya CHAN.

Ukiwa umesalia mwaka kabla ya fainali hizo kupigwa, swali ni je itakuwaje kama wachezaji wenye asili ya Tanzania wanaocheza ligi kubwa duniani wakaitwa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na wakaamua kuvaa jezi hiyo.

Ikumbukwe hivi karibuni kocha wa Stars, Miguel Gamondi pamoja na Shirikisho la Soka nchini (TFF) limeanza mchakato wa kuwashawishi baadhi ya wachezaji wenye asili ya Tanzania kuitumikia timu hiyo miongoni mwao ni Benard Kamungo anayeitumikia Dallas FC ya Ligi Kuu Marekani.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wachezaji ikitokea wakakubali kuitumikia Taifa Stars itakuwaje?


BENARD KAMUNGO

Inaelezwa kwamba huyo ni nyota wa kwanza kuwa kwenye mpango wa kushawishiwa Stars kutokana na uhitaji wa washambuliaji wenye uwezo mkubwa wa kufunga.

Eneo la ushambuliaji kwa Stars lina nyota kama Mbwana Samatta anayekipiga Ligi Kuu Ufaransa akiwa na Le Havre, Simon Msuva (Al Talaba, Iraq), Cyprian Kachwele (Whitecaps FC 2) na wengineo.

Kamungo ana uzoefu mkubwa na Ligi Kuu Marekani tangu aitumikie Dallas 2022/23, akifunga mabao 23 katika mechi 54 akiwa mmoja wa washambuliaji muhimu kwenye kikosi hicho. Kabla ya kujiunga na Dallas aliitumikia North Texas SC ya Ligi Kuu Marekani, alipocheza misimu miwili akifunga mabao 22 katika mechi 52.

Kwa miaka kadhaa Stars imekuwa ikiwategemea Samatta na Msuva kwenye eneo la ushambuliaji, nyota ambao wanaonekana nguvu yao kupungua baada ya kucheza kwa muda mrefu, hivyo kama Kamungo ataitwa na kuitumikia huenda akaongeza ushindani kwenye kikosi hicho.

Juni mwaka 2023 aliwahi kuitwa kwenye kikosi cha Stars kilichokuwa kinajiandaa na mechi dhidi ya Niger kwenye mashindano ya AFCON lakini hakucheza baada ya pasi yake ya kusafiria kuchelewa.

Kamungo pia amewahi kuitwa katika kikosi cha Marekani chini ya miaka 23 kilichoshiriki Michezo ya Olimpiki 2024.

Lakini swali ni je ikiwa Kamungo ataamua kuichezea Tanzania ataweza kuendelea kuonyesha makali yake kutoka MLS hadi kwenye mashindano ya Afrika yenye ukakamavu zaidi, ataweza kuibeba Stars katika nyakati ngumu.

Mshambuliaji huyo ni mzaliwa wa Kasulu mkoani Kigoma na familia yake iliishi katika kambi ya wakimbizi mkoani humo baada ya wazazi wake kukimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwaka 2016 baada ya familia yake kupata msaada kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) walitimkia Texas ndipo safari yake ya soka ilipoanzia.

Baada ya kuhamia Marekani Kamungo alianza soka katika shule ya Abilene High School (Abilene Eagles) chini ya kocha Kyle Riese.

Baada ya kuhitimu yeye na kaka yake Imani walitafuta majaribio mtandaoni akapata nafasi ya kujaribiwa katika kikosi cha North Texas SC kwa ada ya dola 90.

Alifanya vizuri kwenye majaribio hayo na kusajiliwa rasmi Machi 25, 2021 na kocha Eric Quill. Mechi yake ya kwanza kucheza ilikuwa Aprili 24 akikipiga dhidi ya Fort Lauderdale CF akitokea benchi, dakika nane baadaye akafunga bao lake la kwanza katika ushindi wa 4–2.

Agosti 30, 2022 alisaini mkataba wa miaka minne na FC Dallas, na Aprili 15, 2023 akafunga bao lake la kwanza la ligi dhidi ya Real Salt Lake dakika ya 88 lililoipa ushindi wa 2–1.


NESTORY IRANKUNDA

Ni mmoja ya nyota wenye asili ya Tanzania waliopata makuzi kwenye akademi mbalimbali ikiwemo Adelaide Croatia Raiders ya Kusini mwa Australia.

Ni winga mwenye kasi aliyeitumikia timu hiyo misimu minne ya vijana, akifunga mabao 22 katika mechi 90.

Kiwango hicho kiliwavutia mabosi wa Bayern Munich walioamua kumpa mkataba kuichezea timu ya vijana lakini alikuwa akipata nafasi ya kucheza timu ya wakubwa.

Alicheza mechi 15 akifunga mabao manne, mwaka 2025 akatolewa kwa mkopo kwenda Grasshopper ya Switzerland akacheza mechi 19 akifunga bao moja. Msimu huu amejiunga na Watford ya Ligi Daraja la Kwanza England na tayari amecheza mechi 31 akifunga mabao matatu.

Winga huyo mzaliwa wa Kigoma, Tanzania, ameshaichezea timu ya taifa ya Australia ya vijana msimu wa 2022/23.

Wazazi wake wanatokea Burundi, lakini walikimbia nyumbani kwao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vinaendelea nchini humo. Baadaye walihama Perth, Western, Australia wakati Irankunda alikuwa na miezi mitatu kisha wakaenda kuishi Kaskazini mwa Adelaide 2013.


KEALEY ADAMSON

Ni beki wa kulia wa kisasa anayekipiga QPR FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England aliyejiunga na klabu hiyo msimu huu akitokea Macarthur ya Ligi Kuu Australia.

Hadi sasa beki huyo amecheza mechi tano kati ya 38 ilizocheza timu hiyo iliyopo nafasi ya 16 kati ya 24 zinazoshiriki ligi hiyo.

Adamson alizaliwa Australia nchi ya mama yake lakini baba yake mzazi ni mzaliwa wa Tanzania.

Mara kadhaa nyota huyo alionyesha nia ya kuja kuichezea Taifa Stars kama atapata nafasi ya kuitwa, hivyo huenda Gamondi akamjumuisha kwenye kikosi kijacho cha AFCON.

Eneo hilo pia wanacheza nyota kama Shomari Kapombe (Simba), Haji Mnoga (Salford City, England), Israel Mwenda (Yanga), Lusajo Mwaikenda (Azam FC) na wengineo.

Amecheza ligi zenye ushindani na kama ataongezwa kwenye kikosi kijacho huenda akaongeza nguvu kwenye eneo la beki wa kulia kutokana na kasi yake na uwezo wa kupanda na kushuka.


ASHQAR AHMED

Beki huyo wa kati alizaliwa England, hata hivyo ana asili ya Tanzania pamoja na Kuwait jambo linalompa sifa ya kuchagua kulitumikia taifa lolote kati ya hayo, kwani hakuwahi kuitwa timu yoyote ya taifa.

Kwa sasa anakipiga katika Klabu ya Forest Green Rovers kwa mkopo akitokea Reading FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England (EFL League One). Maisha yake ya soka yalianza akiwa na kikosi cha Reading cha vijana kabla ya kupandishwa timu ya wakubwa 2024.

Ni beki aliyekulia kwenye malezi ya soka na anatajwa kuwa mmoja wa mabeki chipukizi wenye utulivu mkubwa na uwezo wa kukaba kwa akili. Kama ataichezea Taifa Stars anaweza kupunguza makosa kwenye safu ya mabeki kwa kushirikiana na waliopo.


MO MISSANGA

Ni mshambuliaji anayechipukia kwenye soka akichezea Oxford United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza England.

Mchezaji huyo ambaye jina lake kamili ni Mohamed Missanga ni miongoni mwa vipaji vinavyochipukia kwa kasi akiwa tayari anaanza kuonja timu ya wakubwa.

Mshambuliaji huyo wa chini ya miaka 18 hajaanza kupata nafasi ya kucheza moja kwa moja lakini ni wazi kuwa kocha Gamondi anahitaji vijana wadogo wenye uwezo wanaokipiga kwenye ligi kubwa.

Missanga yupo kwenye hesabu za kocha huyo na kama atashawishika kuitumikia timu hiyo anaweza kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji.