38 zaanzisha vita ZFF Cup
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, mechi 19 zimepangwa kuchezwa kuanzia Oktoba 22 hadi 27 mwaka huu, huku michezo yote ikitarajiwa kuanza saa 10 jioni katika viwanja tofauti vya Unguja.
MASHINDANO ya Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF FA Cup 2026) hatua ya awali ya mchujo inatarajiwa kuanza Oktoba 22, 2026 huku yakihusisha timu 38 zitakazowania nafasi ya kusonga mbele.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo, mechi 19 zimepangwa kuchezwa kuanzia Oktoba 22 hadi 27 mwaka huu, huku michezo yote ikitarajiwa kuanza saa 10 jioni katika viwanja tofauti vya Unguja.
Katika siku ya kwanza ya mashindano hayo, kutakuwa na mechi nne zitakazochezwa kwa wakati mmoja katika viwanja tofauti ambapo Mbuyuni itaikabirisha Ujamaa kwenye Uwanja wa Mao B na Flamingo itachuana na Paje Stars katika Uwanja wa Kitogani.
Mechi nyingine ya siku hiyo itawakutanisha Sharp Boys dhidi ya Ranger Bulls katika Uwanja wa Mao A, wakati ZMCL ikicheza na Villa katika Uwanja wa Maisara A.
Oktoba 23, michezo minne imepangwa kuchezwa, ambapo Sungungu itakutana na Sebleni katika Uwanja wa Mao B, Pitanazako itacheza na Muungano Ranger katika Uwanja wa Kitope, huku Nungwi City ikipambana na New King kwenye Uwanja wa Matemwe.
Mchezo mwingine wa siku hiyo, Cairo itakuwa mwenyeji wa Mwera Star katika Uwanja wa Mao A.
Oktoba 24, ratiba inaonesha Black Lion itacheza na Malindi katika Uwanja wa Maisara B, Maungani United itakutana na Kikungwi katika Uwanja wa Mao A na Mbiji itapambana na Kundemba katika Uwanja wa Kitope, huku ZAFSA Academy ikivaana na Bridge katika Uwanja wa Mao A.
Michezo hiyo itaendelea Oktoba 25 kwa mechi mbili pekee, ambapo Bububu FC itacheza na Urafiki katika Uwanja wa Mao A, huku Nyangobo FC ikikutana na Negro United katika Uwanja wa Mao B.
Oktoba 26, mashabiki wa soka watashuhudia michezo mitatu, ikiwemo Muembe Makumbi dhidi ya Bweleo katika Uwanja wa Mao A, New Power dhidi ya New City katika Uwanja wa Mao B na Ngome itakayocheza na Mundu katika Uwanja wa Maisara A.
Ratiba ya mechi za awali itahitimishwa Oktoba 27 kwa michezo miwili, ambapo SCUD SC itapambana na New Academy katika Uwanja wa Mao A, huku Zantex ikikutana na Kitope katika Uwanja wa Mao B.