28 zawania ubingwa wa kikapu
Muktasari:
- Nahodha wa Stein Warriors ya jijini Dar es Salaam, Brian Mramba amesema kwa msimu huu wamejipanga vyema ambapo ametoa wito kwa wadhamini wengine kujitokeza kudhamini mchezo huo.
Timu 28 za mpira wa kikapu kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, zimeanza kushiriki mashindano ya Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) inayofanyika jijini Dodoma, inayodhaminiwa na BetPawa kupitia programu yake ya Locker Room Bonus.
Akizungumza katika ufunguzi wa mashindano hayo yanayofantika katika viwanja ya Chinangali, Kamishna wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Robert Manyerere, amesema huo ni mwendelezo wa mashindano baada ya klabu shiriki kushinda kwenye mikoa yao.
Amesema katika mashandano hayo, timu 16 za wanaume na 12 za wanawake ambapo baadhi zimetamba kuchukua ubingwa kutokana na namna zilivyojipanga.
"Michuano imeanza Novemba 28, na inatarajiwa kumalizika Desemba 8 mwaka huu katika viwanja vya Chinangali hapa Dodoma ambapo zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa kila mechi zinazotolewa na BetPawa kupitia program ya Locker Room Bonus imeongeza hamasa kwa kila timu kutaka kuibuka na ushindi," alisema.
Amesema mshindi katika mashindano hayo ndiye atakayewakilisha nchi huku mshindi wa pili na tatu akiwakilisha Zone Five kwa mashindano ya Afrika Mashariki.
Esther Matiko ambaye ni Rais wa mabingwa mara mbili mfululizo kwa upande wa wanawake, Fox Divas kutoka mkoani Mara, ambaye ni mbunge wa Tarime Mjini, ameiomba Serikali kuwekeza kwenye mpira wa kikapu huku akiwataka wadhamini wengine kujitomeza kudhamini mchezo huo kwani unapendwa na ni fursa kwa vijana wenye vipaji.
"Mchezo wa kikapu Tanzania unakua kwa kasi, hivyo taasisi binafsi zijitokeze kuwekeza kwenye mchezo huu, lakini changamoto kubwa ni kukosekana kwa viwanja kuanzia ngazi ya chini kwa maana ya shule za msingi," amesema Matukio.
Naye Mwakilishi wa BetPawa, Rose Kishimba, ameeleza kuwa wao kama wadhamini wamesukumwa kudhamini moja kwa moja mchezo huo ili kuwasaidia wachezaji kwa kujikimu hasa kwa vijana ambao wamekuwa wakijitolea kucheza kwa kutumia muda wao na kwamba fedha hizo zinawasaidia nauli na kununua vifaa vya michezo.
"Tangu tumeanza kufadhili kuna mabadiliko makubwa yamejitokeza kwa wachezaji ikiwemo kupata morali na timu nyingi kutaka kushinda na kucheza kwa kiwango cha juu," amesema Kishimba.
Nahodha wa Stein Warriors ya jijini Dar es Salaam, Brian Mramba amesema kwa msimu huu wamejipanga vyema ambapo ametoa wito kwa wadhamini wengine kujitokeza kudhamini mchezo huo.