Angel Nyigu anataka kuacha alama katika kudansi
Muktasari:
- Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Nyigu anasema muda wake mwingi anautumia kwa vitu vinavyoleta tija, akisisitiza amejifunza kutowapa nafasi watu ambao mitazamo yao haina msaada na maisha yake.
KATI ya mambo anayoyafanya mnenguaji maarufu wa kike hapa nchini, Angel Nyigu anaamini katika anachokifanya, ni kujifunza kwa wapambanaji waliofanikiwa na siyo wanaopunguza ukubwa wa ndoto zake kutokana na mitazamo yao.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti, Nyigu anasema muda wake mwingi anautumia kwa vitu vinavyoleta tija, akisisitiza amejifunza kutowapa nafasi watu ambao mitazamo yao haina msaada na maisha yake.
“Nimejifunza vitu vingi katika maisha ya dansi, siruhusu vitu dhaifu viue ukubwa wa ndoto zangu, mimi ni mpenzi wa kufuatilia zaidi watu waliofanikiwa, jambo lililonisaidia kukomaa kiakili kukabiliana na mambo yanavyokuwa yanakuja tofauti,” anasema.
KUJIAMINI
Anasema anajiamini katika kazi yake, hilo ndilo lililomsaidia kufika alipo na kuaminika na wasanii wakubwa kuvutiwa kufanya naye kazi, haruhusu mtu kumuondoa katika mstari wa kile anachokiamini.
“Jambo linalowavutia mashabiki wengi kupenda kazi yangu najiamini na mtu yeyote akitaka kufanikiwa anapaswa kujiamini kabla ya kuaminiwa na mtu yeyote, hapa duniani hakuna mtu ambaye anapambania mafanikio ya mtu mwi ngine, isipokuwa muhusika mwenyewe ajipambanie, hilo ndilo nililolifanya wakati wote katika kazi zangu,” anasema na kuongeza;
“Nakumbuka wakati nipo chini ya wasanii, nilisimamishwa kazi kwa muda wa wiki mbili, ilinipa msongo mkubwa wa mawazo, lakini nikapata muda wa kufikiria kwa kina, nikaona ni fursa ya kujisimamia mwenyewe na dunia ijue kipaji changu, nikaongeza bidii ya kujifunza kwa waliofanikiwa kila siku.”
Anasema watu wengi walifeli katika kile wanachokifanya, waliyashikilia maneno ya watu waliowakatisha tamaa, badala ya kujituma na kuongeza vitu vipya katika kazi zao.
“Katika maisha yangu, chalenji yoyote ni somo kwangu la kunivusha kuwa mtu mwingine, haikuwa rahisi kufika hapa nilipitia vingi, ila niliviweka kwenye nafasi ya kunijenga na siyo kunibomoa, kwani wakati naanza wapo walioona siyo kazi ya heshima ila nilifanya bidii ya kuonyesha ni kazi kama zingine.
“Kuna mitazamo ya watu kukuona unatakiwa kuishia levo fulani, ila mimi niliwaonyesha levo zangu siyo hizo bali ni kuvuka mipaka ya kimataifa na imekuwa hivyo.”
Anaeleza vitu vinavyotakiwa katika kazi hiyo, anataja cha kwanza ni nidhamu, kufanya mazoezi kudansi, gym, kukimbia ili kuuweka mwili fiti na utayari wa kazi, kutokana na anapokuwa jukwaani anatumia nguvu.
“Ndiyo maana nimeitaja nidhamu siyo kazi inayohitaji uvivu, ina misingi yake, wengi wao ambao ni wavivu wanajikuta mwisho wa siku wanaishia njiani, kila kitu anachokifanya mtu lazima kujituma na ubunifu, ukileta mazoea basi ujue kazi yako inakuwa ya kawaida sana,” anasema.
NDOTO YAKE
Anatolea mfano wa supastaa wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz hatua alizozianza kwenye muziki hadi kutengeneza jina kubwa, linalotamaniwa na wengi kufikia hatua zake, kwamba katika majukumu yake anataka aache legasi kwa jamii na vijana wenzake. “Natamani kuhusika kwenye maisha ya watu wengi, ndiyo maana nilianza kwa kuamini kwenye ndoto zangu, nimepiga hatua za mafanikio nahitaji kuwashika wengine mkono hasa wale wenye vipaji kuwasaidia vianze kuwalipa, hiyo ndiyo ndoto yangu kubwa ya kutaka kuacha legasi katika jamii,” anasema Nyigu na kuongeza;
“Wakati wa kujipambania nilijifunza vitu vingi, vitakavyowafaidisha wengine, ukisikia watu wenye mafanikio au majina yanayoishi ni yale yaliyopanda mbegu kwa wengine, siyo ubinafsi, ukitaja kwa wema kwenye maisha ya watu au kuinua vijana badala ya kufanya vitu vya hovyo wakawa wanapata pesa kupitia vipaji vyao ni baraka tosha.”
USHAURI
Jambo analowashauri vijana wengi wanaotamani kuingia katika sekta hiyo, wajitahidi kujifunza vitu vipya kila wakati hata wakiwa nyumbani kwao, jambo la msingi zaidi watafute koneksheni zitakazowapa hatua ya kujulikana zaidi.
“Lazima watafute koneksheni na watu ambao wamefanikiwa, wasiogope kuthubutu, nidhamu, juhudi na bidii hivyo ndivyo vitakavyowawezesha kufanikiwa, nina uzoefu na hilo ndiyo maana nimefika hatua niliyopo,” anasema.
KUFANYA KAZI NA MASTAA WAKUBWA
Anasema kufanya kazi na wasanii tofauti wakubwa, kumemsaidia kupanua wigo wa kufanikiwa zaidi na kujifunza vitu tofauti, ambavyo vinaendelea kulinda heshima yake katika jamii. “Kufanya kazi na wanamuziki wakubwa inakuwa ni rahisi kufika levo za juu, endapo ukifanya kazi vizuri itakayokuwa na ushawishi wa wengine kukuona na kutamani kufanya nao kazi, ingawa pia inakuwa inambeba na msanii mwenyewe, hilo limenifanya nipafomu kwenye majukwaa makubwa, ambayo isingekuwa rahisi kufika,” anasema Nyigu na kuonyesha.
“Kazi nzuri zinakubeba na ndiyo maana unaona nimefanya na wasanii mbalimbali, imenifanya nizunguke nchini zaidi ya 16, kuna watu wameniona kwenye mitandao ya kijamii wakanipa mwaliko, wengine niliwatafuta mwenyewe kufanya nao kazi ili kuendelea kujitangaza zaidi.
“Kuna wakati mwingine safari ninazokwenda ninajigharamia, lakini ninapofanya vizuri nalipwa pesa ndefu, hivyo nakuwa sijaingia hasara, bado naendelea kupambana hadi vizazi vingine vitakuja kusimulia misingi ninayoijenga,” anasema Nyigu ambaye ni shabiki wa Simba SC.
KITUO
Anasema ni ndoto ya kila dansa kuwa na kituo, hivyo ni jambo ambalo analifanyia kazi na tayari ana darasa la kuwasaidia watoto kuwafundisha ili wakulie katika misingi sahihi ya kazi hiyo.
“Mimi ni mtu ambaye natamani kila mtu awe na mafanikio, ndiyo maana nguvu yangu kubwa naitumia kwenye vitu vya maana na siruhusu huzuni ama maumivu yawe sehemu ya maisha yangu,” anasema.
Anasema maisha ya dansa yamemfunza uvumilivu na kumpa nguvu ya kuwasaidia wengine kuhakikisha wanafikia ndoto zao: “Maisha ya dansa siyo marahisi, lakini nimejifunza maisha ndiyo maana elimu hiyo natamani kuitoa kwa wengine.”
Mbali na hilo, anasema asilimia 90 ya maisha yake, yanaendeshwa na kazi ya dansi.
“Naisaidia familia yangu, nina vijana ninaofanya nao kazi wanazisaidia familia zao, hivyo dansi ni kazi yenye heshima kubwa, ukiachana na hilo simsikilizi msanii mmoja, nasikiliza nyimbo nzuri zinazonipa morali ya kucheza,” anasema.
Anasema ameamua kutengeneza thamani yake ya kulipwa vizuri akibainisha kwamba: “Sikimbilii tu kufanya kazi, msanii ananiuliza unataka kulipwa kiasi gani, kuliko kukimbilia kupata wafuasi kwenye mitandao ya kijamii.”
SAFARI YAKE
Anasimulia safari yake ya kudansi, alianza akiwa nyumbani kwao Njombe mkoani Iringa lakini alihamia jijini Dar es Salaam kifamilia, akiwa kidato cha kwanza aliendeleza hilo akiwa shule na kufanya shoo kwenye mahafali shuleni.
“Marafiki zangu walikuwa wananipa nguvu kwamba naweza kucheza, hivyo nilikuwa nikirudi nyumbani nafanya mazoezi zaidi niwafurahishe marafiki zangu, kuingia moja kwa moja katika kazi hiyo, nilienda kwenye mashindano nikapata moyo kuona itakuwa njia ya kujipatia kipato,” anasema.