Tunamlaumu nani ubovu wa kanuni za uchaguzi TFF?
HAKUNA ubishi, Kanuni za Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) za awamu hii ni uhuni mtupu, Kanuni zetu za Uchaguzi ni kama mtego wa Panya, aliyeko nje, atabaki nje, aliyeko ndani, atabaki ndani.
Badala ya watu kupata wasaha wa kutazama wagombea na kupima Sera zao, agenda kubwa imebaki kuwa Kanuni, tunamlaumu nani ubovu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Tanzania ina watu zaidi ya Milioni 55 lakini, wanaopiga kura kumchagua Rais wa TFF hawafiki watu mia moja, kuna wakati wanakuwa 85, kuna wakati wanakuwa 83, ni vigumu sana kumtoa Rais aliyeko madarakani, ni rahisi sana kupata kiongozi wa ajabu kwa sababu, anapitishwa na watu wachache mno.
Ni rahisi sana watu kushawishika kwa tamaa zao na kutupa mtu asiyefaa, nini tunaweza kufanya katika hili? Jibu ni rahisi tu, tutanue wigo wa wapiga kura, Mkutano Mkuu peke yake, usituamulie Rais.
Nimekuwa nikitazama mfumo unaotumika kutupatia Mchezaji Bora wa FIFA wa Dunia, nadhani tunaweza kuchukuwa baadhi ya vitu, Mchezaji Bora wa FIFA anapatikana kwa kura za Kamati ya Ufundi ya FIFA, manahodha wa mataifa yote ambao ni wanachama wa FIFA, makocha wa mataifa yote ambayo ni wanachama na majukwaa ya mtandaoni.
Tuko kwenye zama mpya, mitandao ya kijamii haiepukiki kwenye ulimwengu huu, ni dhambi kubwa kwa Rais wa TFF kwenye Taifa lenye watu zaidi ya Milioni 55 kupatikana kwa kura ambazo hazifiki hata 100.
Tunahitaji mabadiliko ya Kanuni za Uchaguzi ambayo yatatoa mwanya wa watu wengi kupiga kura, Mkutano Mkuu wa TFF unaweza kubeba 50% ya kura, vyombo vya Habari wanaweza kupiga kura na hasa Waandishi wa Habari za Michezo na kutupa 25% na Mitandao ya kijamii ambako ndiko waliko mashabiki na wapenzi wa michezo wenyewe, wangepewa nafsi ya kupiga kura na kutupa walau 25% nyingine.
Ukiongeza wigo wa wapiga kura wengi na kwenye majukwaa tofauti, unapunguza harufu ya mgombea mmoja kununua watu, mpira wa nchi hii ni wetu sote, lengo letu wote linapaswa kuwa mpira na sio maslahi binafsi, Kanuni zetu zimebadilishwa kwenye mkutano Mkuu wa TFF na zikapata baraka zote kutoka serikalini kupitia chombo chake, Baraza la Michezo (BMT). Tunamlaumu nani Kwa ubovu wa Kanuni hizi za Uchaguzi? Nipe jibu kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Kuna Kanuni mpya nyingine ambayo inaruhusu mgombea mmoja kupata udhamini usio na kikomo kutoka kwa vyama shiriki na wachama wa TFF, mgombea akikosi udhamini, anakosa sifa za kugombea, huu ni uhuni usiovumilika, hii Kanuni haina mashiko hata kidogo, amewekwa kwa lengo tu la kuzuia haki ya msingi ya Watu kwenda kugombea nafasi.
Wagombea wengi wamekosa udhamini, watu wengi wamekata tamaa, ukiniuliza kama kuna mantiki yoyote ya Kanuni hii? Nitakujibu hakuna. Huo ni uhuni mtupu, mazingaombwe matupu, tatizo la viongozi wetu, wanawaza zaidi kushinda uchaguzi kuliko kuusaidia mpira wetu.
Lakini hizi Kanuni zote, zilipelekwa serikalini kupitia BMT na zikapata baraka zote. Tumlaumu nani ubovu wa Kanuni hizi za Uchaguzi? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Kwa Taifa lenye watu zaidi ya Milioni 55, sio sawa kupata kiongozi Mkuu wa Taasisi ambaye amechaguliwa na watu kisoda, watu wachache ambao hawafiki hata 100, msingi wa mpira wetu uko kwenye Klabu zetu lakini, wao wanapiga kura chache kuliko makundi mengine yoyote, Kanuni tulizonazo zinaonyesha Rais wa TFF anakwenda kuongoza Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na ligi ngazi ya Mikoa lakini, wanaompigia kura ni klabu za Ligi Kuu tu.
Hii ni Kanuni nyingine ya mauza uza tuliyonayo! Kwani nini hizi timu za madaraja mengine hazipewi haki ya kumchagua Rais wamtakaye? Wajumbe wawatakao? Usinipe jibu. Huu ni uhuni wa kanuni zetu za Uchaguzi, Uchaguzi tangu utangazwe, Agenda imekuwa ni Kanuni tu, hakuna hata muda wa kuwatathimini wagombea, hakuna muda wa kuwaza maendeleo.
Mpira wetu hauwezi kuendelea kwa kuwaza Kanuni za Uchaguzi kila siku, kuna Kanuni nyingi tu ambazo kimsingi hazina tija, hakuna chuo kinachotoa kozi ya kuwa Rais wa TFF, hakuna, lazima tukubali kubadilisha Kanuni ili kuongoza zaidi ushindani wa hoja.
Kwa namna mambo yalivyokwa sasa, mwenye ushawishi kwa wajumbe ndiyo mshindi hata kabla ya Kampeni na Uchaguzi, Sera hazina maana tena, hoja ni kupoteza muda tu, ni kama mshindi amepatikana siku Kanuni mpya za Uchaguzi zilipopitishwa kwenye mkutano Mkuu.
Kinachonishangaza ni Kanuni hizi kupitishwa na mkutano Mkuu, kinachonishangaza zaidi ni Kanuni hizi kupata baraka ya BMT.
Namna mpira wetu unavyoendeshwa ni kama Mtego wa Paya, aliyeko ndani, anabaki ndani, aliyeko nje, anabaki kuwa nje. Tunawajibu wa kuboresha Kanuni zetu ili kuusaidia mpira wetu. Urais utakuwa haina maana kama utakuwa unapatikana kwa njia za Panya, ujumbe wa Kamati ya Utendaji utakuwa hauna maana kama watu wanatakiwa kuzungukana kuupata. Tumepoteza muda mwingi sana kujadili Kanuni za Uchaguzi wa TFF badala ya kuyatazama mahitaji yetu ya msingi ya mpira wetu, Kanuni zilipitishwa na Mkutano Mkuu wa TFF, Kanuni zilipitishwa na BMT, Tunamlaumu nani ubovu wa Kanuni za Uchaguzi wa TFF? Kamati ya Uchaguzi wa TFF inapaswa kutumia busara sana kwenye Uchaguzi wa mwaka huu na hasa kwenye kigezo cha wadhamini, hapa kuna uhuni mwingi sana umetumika kuwanyima watu haki ya kugombea, mpira sio wa mtu mmoja Tanzania, ni mchezo wa kila mtu, atakaye pitishwa na Kamati ya Uchaguzi tunapaswa kumkubali na kumpa ushirikiano lakini, Kanuni lazima zibadilishwe.