Kwa hili Timu zijifunze, zisirudie kosa
Muktasari:
- Hali inayoikumba sasa Fountain Gate ni mfano hai wa namna uzembe wa kiutawala na kushindwa kuendana na kanuni za uendeshaji wa mpira wa kisasa unavyoweza kuipeleka timu kwenye janga.
LIGI Kuu Bara ni kipimo kikubwa cha ubora wa soka letu na kioo cha jinsi klabu zetu zinavyopaswa kujiendesha. Katika miaka ya karibuni kumekuwapo na changamoto kubwa zinazojirudia kwa baadhi ya timu ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na kutoendeshwa kisasa na kutozingatia wajibu wa msingi.
Hali inayoikumba sasa Fountain Gate ni mfano hai wa namna uzembe wa kiutawala na kushindwa kuendana na kanuni za uendeshaji wa mpira wa kisasa unavyoweza kuipeleka timu kwenye janga.
Ni fedheha kuona timu ikianza msimu ikiwa na idadi ndogo ya wachezaji - 14 pekee kwa sababu tu ya kutoshughulikia madeni ya zamani ya wachezaji waliowahi kuitumikia. Kanuni na sheria za Fifa zipo wazi timu inayoshindwa kulipa wachezaji wake fidia au mishahara, inafungiwa usajili.
Fountain Gate iliwahi kukumbana na hali kama hii msimu uliopita ya kujikuta ikikumbana na rungu la Fifa lililotokana na masuala ya wachezaji na sasa imerudi kulekule ikianza msimu na wachezaji 14.
Historia pia inatufundisha Tabora United iliwahi kupitia tatizo kama hilo misimu mitatu iliyopita. Hii si bahati mbaya, bali ni kielelezo cha kushindwa kubadilika.
Timu ikicheza na wachezaji 14 ni dhahiri kwamba mapema au baadaye itafika hatua ambapo mashindano yatakuwa magumu kuyamudu. Wachezaji hawa ni binadamu wanachoka, wanapata majeraha na wanahitaji mbadala.
Kutegemea kundi dogo la wachezaji msimu mzima ni kujitafutia aibu na kushuka daraja mapema. Tayari Fountain Gate imepoteza mechi mbili za mwanzo, na hali ikibaki hivi, ni vigumu kubashiri matokeo bora.
Ni wakati sasa kwa klabu shiriki Ligi Kuu Bara kuacha kufikiri kwa mazoea na kubadilika. Soka la kisasa linahitaji usimamizi wa kisasa. Wachezaji wana haki zao, na klabu zinapaswa kuhakikisha zinawalipa kwa wakati ili kuepusha kesi na kufungiwa usajili. Haiwezekani kila mwaka kusikia timu ikilalamika kwa sababu ya kufungiwa kutokana na madeni. Ni kioja, ni aibu na ni ishara ya kutokua na mafunzo.
Tunazikumbusha timu zetu kwamba enzi za kuomba huruma zimepitwa na wakati. Hakuna huruma kwenye mashindano makubwa kama haya.
Timu inapocheza Ligi Kuu inakubali kwa hiari kufuata kanuni na masharti ikiwemo kuwajibika kifedha. Wachezaji si wahisani wa klabu ni wafanyakazi wanaotumia nguvu, jasho na muda. Kuwalipa ni wajibu, si hiari.
Kwa Fountain Gate na timu nyingine zinazochukulia masuala ya fedha kwa wepesi, huu ni wakati wa kujitazama upya. Tusipojifunza leo, kesho hali itakuwa mbaya zaidi. Mchango wa klabu katika kukuza soka la Tanzania ni mkubwa, lakini hauwezi kuonekana iwapo zinajitumbukiza katika matatizo ya kujitakia.
Hatua ya kufungwa mechi mbili mapema kwa sababu ambazo zingeweza kuepukwa ni tahadhari tosha kwamba bila mipango mathubuti ya kiutawala na kifedha safari ya timu hii inaweza kuwa fupi kwenye Ligi Kuu Bara.
Tunatoa onyo kwa timu kuwa ni lazima ziendeshe shughuli kwa uhalisia wa kisasa. Zinapaswa kulinda heshima ya ndani na wachezaji. Kushindwa kulipa wachezaji na kutegemea miujiza au huruma baadaye siyo suluhisho. Soka letu lina thamani kubwa tusiliweke rehani kwa uzembe unaoweza kuepukika.