Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga wamedhihirisha ukubwa wao kwa Namungo

Rudini tukutane kwa Mkapa

MCHEZO wa juzi Yanga dhidi ya Namungo FC katika Uwanja wa Benjamin ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 umedhihirisha kuwa Yanga imejipanga na inastahili kuwa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Makosa mawili yaliyofanywa na safu ya ulinzi ya Namungo FC yalitosha kutumiwa kwa ustadi na Fiston Mayele na Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuipatia Yanga mabao hayo mawili yaliyoipa pointi tatu zilizoifanya ifikishe jumla ya pointi 54 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi.
Bao la kwanza la Fiston Mayele ni zao la mkimbio mzuri alioufanya nyota huyo pembeni ya beki Abdul Malick ambaye alishindwa kuokoa pasi ya Djuma Shaban iliyopigwa mbele yake na baadaye kuteleza na mpira huo kumkuta Fiston aliyeutuliza vyema na kumtazama kipa David Kisu kisha kupiga shuti la wastani lililojaa nyavuni.
Lile la pili lililopachikwa na Fei Toto lilitokana pia na hesabu sahihi za kiungo huyo kukimbilia pasi ya Khalid Aucho ambayo walinzi wawili wa kati wa Namungo FC walizubaa kuikoa na kumpa mwanya kiungo huyo kujaza mpira kimiani.


Upangaji kikosi uliigharimu Namungo
Silaha kubwa ya Yanga msimu huu ni safu yake ya kiungo ambayo imekuwa ndio inayotengeneza idadi kubwa ya mabao na kuipa balansi timu hiyo katika mechi mbalimbali.
Wakati Yanga ikianza na viungo watatu wenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi sahihi zinazovunja mstari wa wapinzani katikati mwa uwanja ambao kati yao wawili kiasili ni washambuliaji, Namungo ilianzisha viungo wawili tu ambao kati ya mmoja kiasili ni wa ulinzi.
Hilo liliwapa faida Yanga ambao walitawala eneo la katikati mwa uwanja na kutengeneza nafasi nyingi za mabao huku ikiiweka katika wakati mgumu Namungo ambayo wachezaji wake walijikuta wakitumia muda mrefu kuukimbiza mpira na kuwafanya baadhi kuchoka na kushindwa kuwa na ufanisi mkubwa.


Magingi amshukuru refa
Beki Frank Magingi anapaswa kumshukuru refa Ahmed Arajiga kwa kumaliza mchezo huo bila kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na rafu alizocheza mara kwa mara hasa kwa Fiston Mayele.
Alionekana kucheza kwa kupania wachezaji wa Yanga hasa Mayele ambaye kwa sasa ndiye kinara wa ufungaji mabao katika Ligi Kuu.


Chico ushindi, Moloko mmmh
Katika mechi ambayo Yanga ilitawala mchezo, ilitegemewa kiwango cha utulivu kwa wachezaji wake kiwe cha juu lakini hali ilikuwa tofauti kwa Ducapel Moloko na Chico Ushindi.
Kukosa utulivu kwa Moloko kulimnyoma fursa muhimu ya kuifungia Yanga, bao katika kipindi cha pili baada ya kushindwa kutumia vyema pasi ya Fiston Mayele kwa kupaisha mpira akiwa analitazama lango la Namungo.
Lakini Ushindi aliyeingia kipindi cha pili, alionekana kushindwa kucheza kitimu na mara kwa mara alilazimisha kukaa na mpira kwa muda mrefu bila sababu jambo lililowapa urahisi Namungo kumdhibiti.


Ubora silaha Yanga
Kiwango bora cha kundi kubwa la wachezaji wa Yanga ni miongoni mwa siri zinazoifanya timu hiyo kuwa tishio katika Ligi Kuu msimu huu.
Uwepo wa nyota wengi ambao wanafanya vizuri uwanjani kwa sasa unalipa wigo mpana benchi la ufundi la timu hiyo katika upangaji wa mbinu na kikosi kutegemeana na aina ya mpinzani wanayekabiliana naye.
Hilo linajidhihirisha katika mechi ya juzi ambayo licha ya Yanga kuwapumzisha Dickson Job na Saido Ntibazonkiza wachezaji waliocheza katika nafasi zao, yannick Bangala na Feisal Salum walizitendea haki nafasi zao na kuiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi.


Kichuya kalinda heshima
Kabla ya mechi hiyo, mshambuliaji Shiza Kichuya alinukuliwa kuwa anatamani kuifunga Yanga kama ambavyo alifanya kipindi hicho alichokuwa akiichezea Simba.
Kwa upande wake hana deni kwani ndiye aliifungia Namungo FC, bao lao pekee ingawa pia alionyesha kiwango bora katika mchezo huo.