Yanga Princess kitendawili cha ubingwa kila msimu
Muktasari:
- Hili limekuwa moja ya mambo yanayowatesa mashabiki wa timu hiyo, hasa kutokana na mafanikio ambayo mahasimu wao Simba Queens wamekuwa wakiyapata katika soka la wanawake.
MIONGONI mwa mambo ambayo mashabiki wa Yanga wanatamani kuyaona ni timu yao ya wanawake, Yanga Princess ikifanya vizuri na hatimaye kuvunja ukimya wa kutobeba ubingwa wa ligi.
Hili limekuwa moja ya mambo yanayowatesa mashabiki wa timu hiyo, hasa kutokana na mafanikio ambayo mahasimu wao Simba Queens wamekuwa wakiyapata katika soka la wanawake.
Wakati Simba Queens imeendelea kutawala ligi na kutengeneza nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa, Yanga Princess imekuwa ikishuhudia mafanikio hayo kutoka pembeni.
Yanga Princess tangu ilipoanza kushiriki ligi mwaka 2018, haijawahi kubeba taji la ligi wala kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa kutokana na nafasi ya ubingwa.
Kwa upande mwingine, tangu ligi hiyo ianzishwe msimu wa 2017, Simba Queens imebeba mataji matano, JKT Queens mara nne, huku Mlandizi Queens ikiwa imetwaa taji moja.
Sasa swali linabaki, ni nini kinachowazuia Yanga Princess kufikia hatua hiyo? Zipo sababu kadhaa ambazo kama zitapatiwa ufumbuzi, huenda timu hiyo ikawa mshindani mkubwa wa ubingwa.
TATIZO UONGOZI
Tofauti na timu ya wanaume ya Yanga, ambayo katika safari na mechi mbalimbali mara nyingi huonekana viongozi wa juu wakiwa karibu na kikosi, hali imekuwa tofauti kwa Yanga Princess.
Timu hiyo imekuwa ikimuachia zaidi Mratibu wa timu, Kibwana Matokeo, jukumu la kusimamia mambo ya kila siku.
Si kwamba Kibwana hawezi kufanya kazi hiyo, lakini kwa ukubwa wa taasisi kama Yanga, uwepo wa viongozi wa juu kwenye timu ya wanawake unaweza kuongeza morali kwa wachezaji na kuonyesha uzito ambao klabu inaupa mradi huo.
Mara nyingi viongozi wakubwa huonekana kwenye mechi zinazovuta hisia zaidi, hasa Yanga Princess inapocheza dhidi ya Simba Queens au JKT Queens.
Lakini kwenye michezo mingine ya ligi, timu imekuwa ikiachwa zaidi chini ya usimamizi wa Kibwana.
Hapa ndipo klabu inaweza kuangalia uwezekano wa kuongeza nguvu kwenye eneo la uongozi, ikiwezekana kwa kumpa Kibwana msaidizi mwenye uelewa mpana wa soka la wanawake.
Hilo linaweza kusaidia katika masuala ya utafutaji vipaji, usimamizi wa kikosi na kufuatilia maendeleo ya timu kwa karibu.
MUENDELEZO HAUPO
Changamoto nyingine ni kutokuwa na muendelezo mzuri kwenye michezo muhimu.
Kwa misimu kadhaa, Yanga Princess imekuwa ikimaliza nyuma ya Simba Queens na JKT Queens, huku ikishindwa kutumia baadhi ya nafasi zinazojitokeza kwenye mbio za ubingwa.
Mfano mzuri ni msimu uliopita na Yanga Princess ilikusanya pointi nne dhidi ya JKT Queens, lakini ikashindwa kufanya hivyo dhidi ya Simba Queens na kupoteza pointi zote sita.
Kama ingeweza kupata hata pointi mbili dhidi ya Simba, nafasi yake katika mbio za juu ingekuwa nzuri zaidi.
Tatizo halikuwa hapo pekee, kwani timu hiyo pia ilipoteza pointi dhidi ya Tausi FC ikiwa nyumbani.
Hii inaonyesha Yanga Princess inahitaji kuwa na mpango maalumu wa namna ya kukabiliana na timu zenye ushindani mkubwa, pia kuhakikisha haipotezi pointi kwenye michezo ambayo inatarajiwa kuipa nafasi ya kusogea juu ya msimamo.
AHADI KILA MSIMU
Hili ni eneo ambalo limekuwa likiwakera baadhi yamashabiki.
Kila msimu kumekuwa na kauli za viongozi Yanga Princess itafanya vizuri na kupambana kwa ajili ya ubingwa, lakini mwisho wa msimu hali imekuwa ileile.
Ahadi zinatolewa, matumaini yanaongezeka kwa mashabiki, lakini matokeo hayajaendana na matarajio.
Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, aliwahi kutoa kauli kwamba timu hiyo isipobeba ubingwa, awajibishwe yeye.
Kauli kama hizi zinapowekwa hadharani huongeza matarajio kwa mashabiki, hivyo inaposhindikana kutimia, huacha maswali mengi kuhusu mipango na utekelezaji wake.
USAJILI NI CHANGAMOTO
Hapa ndipo penye kazi kubwa zaidi.Kwa namna ambavyo kikosi kimekuwa kikijengwa, kuna wakati inaonekana kocha Edna Lema hana nafasi kubwa ya kuamua aina ya wachezaji anaowahitaji, bali anapokea wachezaji wanaosajiliwa na klabu.
Hilo linaweza kuwa tatizo kama usajili hautaendana na mahitaji ya kiufundi ya timu.
Katika misimu iliyopita, Yanga imekuwa ikisajili wachezaji kadhaa kutoka Simba Queens, ambao baadhi yao walikuwa wameachwa baada ya kutokuwa sehemu ya mipango ya wapinzani wao.
Mfano msimu uliopita, Yanga ilimsajili miongoni mwa wengine Ritticia Nabbosa, Asha Djafar, Diana Mnally na Zubeda Mgunda kutoka Simba.
Hakuna ubaya kusajili wachezaji kutoka timu pinzani, lakini swali kubwa ni moja: Je, wachezaji hao wanaendana na mahitaji halisi ya Yanga Princess?.
Hilo ndilo jambo ambalo viongozi wanapaswa kulijibu kupitia matokeo ya timu.
Msimu huu pia kulikuwa na sintofahamu kuhusu Agnes Pallangyo, ambaye alikuwa mhimili muhimu katika eneo la kiungo.
Pallangyo aliachwa kabla ya baadaye kurejeshwa kikosini, jambo lililoibua maswali kuhusu namna maamuzi ya usajili yanavyofanyika.
Hali kama hiyo pia ilijitokeza kwa kipa Rita Akarekor, ambaye alikuwa amefanya vizuri katika misimu iliyopita, lakini akaachwa huku klabu ikiingia tena sokoni kutafuta walinzi wengine wa lango.
Kwa kifupi, Yanga Princess inaonekana kuanza upya kwenye baadhi ya maeneo kila msimu badala ya kujenga kikosi kinachoboreshwa kutoka msimu mmoja kwenda mwingine.
HAPA WAMEFAULU
Pamoja na changamoto hizo, Yanga Princess ina eneo ambalo imekuwa ikifanya vizuri na kuipa klabu sifa kukuza na kuuza wachezaji.
Katika misimu ya karibuni, timu hiyo imekuwa ikitoa wachezaji wanaoweza kuhamia kwenye ligi kubwa nje ya Tanzania.
Msimu uliopita, Jeanine Mukandayisenga alimaliza akiwa mfungaji bora kwa mabao 20 kabla ya kuondoka na kujiunga na soka la China.
Pia, uhamisho wa Clara Luvanga kutoka Al Nassr kwenda Washington Spirit ya Marekani umeendelea kuonyesha namna wachezaji waliopita kwenye mazingira ya Yanga wanavyoweza kufikia hatua kubwa katika soka la kimataifa.
Aisha Masaka, ambaye kwa sasa anacheza Brighton & Hove Albion, pia aliwahi kupita Yanga chini ya kocha Edna Lema.
Hili ni eneo ambalo Yanga Princess inapaswa kuendelea kulijenga, kwa sababu linaweza kuwa msingi wa kupata wachezaji bora, kuwapa nafasi, kuwaendeleza na baadaye kuwanufaisha klabu na taifa.
WASIKIE VIONGOZI
Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo anasema timu hiyo itafanya maboresho machache msimu huu kutokana na tayari imetengeneza timu yenye ushindani.
"Tumekuwa na tathmini ya timu na kuna baadhi ya maeneo tumerekebisha kuelekea msimu mpya hivyo hatuzungumzi sana lakini kila kitu kitaaonekana msimu huu," amesema Matokeo.