Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

YAKOUB; Upweke, kutocheza mechi kunavyomtesa

YAKOUB Pict


HANA muda mrefu tangu ajiunge na Simba akitokea JKT Tanzania na keshaoja utamu wa kuidakia timu hiyo miongoni mwa kubwa katika soka la Tanzania.


Wakati akipiga hesabu za kuendelea kuuwasha moto Msimbazi ikaja michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 na jina lake likawa mojawapo kati ya wachezaji 28 waliokwenda na Taifa Stars katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Morocco, lakini ghafla akaumia.


Hapa anazungumziwa kipa namba moja wa timu ya taifa (Taifa Stars) kwa sasa, Yakoub Suleiman aliyesajiliwa na Simba msimu huu.

Kipa huyo anasema hajawahi kupitia nyakati ngumu tangu alipopata jeraha kubwa kama sasa hivi, na kukaa nje kwa muda mrefu. Lakini, jambo la msingi anajipa moyo akivumilia anayopita, huku akitarajia kurejea kazini hivi karibuni.

Yakoub aliumia mazoezini kabla ya kuanza michuano na kukosa mechi zote nne za Taifa Stars iliyoishia hatua ya 16 Bora ikipoteza kwa bao 1-0 mbele ya wenyeji Morocco.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, nyanda huyo wa boli anasema mtu aliyezowea kuzungukwa na watu wengi kila wakati anapojikuta ana muda wa kukaa peke yake kitu cha kwanza anakumbana nacho ni upweke na kutocheza.

YAKO 01

KUREJEA FEBRUARI

Yakoub anasema kwa sasa anaendelea kufanya mazoezi chini ya madaktari na kurejea nyumbani na kwamba kiafya anajiona yupo vizuri tofauti na mwanzo alipokuwa anasikia maumivu makali baada ya kuumia siku moja kabla ya mechi dhidi ya Nigeria kule Morocco.

“Niliumia tukiwa katika maandalizi ya mechi dhidi ya Nigeria ya michuano ya AFCON. Ingawa najiona nipo fiti, lakini madaktari wananipa programu kila siku itakayonisaidia kupona kabisa ili nikianza kazi isiwepo mambo ya kutonesha jeraha,” anasema Yakoub.

“Daktari ameniambia nitajiunga na timu Februari Mosi, lakini kila siku nakuwa naangaliwa na kupewa mazoezi. Hilo linanisaidia kuendelea kuimalika zaidi kiafya. Sijawahi kupata majeraha makubwa kama haya tangu nianze kucheza mpira wa miguu.”

Anasema kukaa nje kwa muda mrefu kunamfanya ajisikie mpweke kwani muda mwingi akiwa kambini yupo na wenzake, lakini lipo jambo analodai kwamba amejifunza.

“Kwa mchezaji kukaa nje inakuwa ni kama alosto, kwani mpira wa miguu ni kazi na burudani. Pia imenifunza jambo gumu maisha nje ya kazi yanakuwaje,” anasema.

YAKO 02

SIMBA IMEMBADILISHA

Tangu alipotua Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania alikomaliza na ‘clean sheet’ nane 2024/25 anadai maisha yake yamebadilika na kuachana na baadhi ya vitu ili kulinda chapa ya timu.

“Tofauti na nilipokuwa JKT Tanzania ambako kukaa vijiweni ilikuwa kawaida na kubishana mambo ya mpira wa miguu, ila kwa sasa nimeweka mipaka. Sisi ni binadamu unaweza ukakosea jambo likachukuliwa kivingine,” anasema.

“Nidhamu kama kula hovyo mtaani hiyo tumefundishwa kazini. Huwezi kumkuta askari anakula hovyo kuna miiko ya kazi, lakini kuwepo kwangu Simba yapo mengi ambayo siwezi kuyafanya.”

Mbali na kujipunguzia kwa uhuru binafsi, anazitaja faida za kujulikana katika kupata huduma za kijamii kirahisi na kutokaa katika foleni pamoja na heshima kuongezeka.

“Ninaweza kwenda kununua vitu dukani napunguziwa bei.Nikienda uwanja wa ndege ama  bandarini nabebewa mizigo na silipi pesa. Naweza nikawa nahitaji huduma kuna foleni naondolewa katika foleni na kuhudumiwa kwa uharaka,” anasema.

YAKO 05

MASHABIKI SIMBA

Yakoub anasema mbali na uchezaji ni shabiki mkubwa wa Manchester United na inapofungwa au kutopata ubingwa husikia maumivu makali, hivyo anaelewa kabisa wanachohisi mashabiki wa Simba kipindi hiki.

“Maumivu ya mashabiki yananiongezea morali ya kujituma kwa bidii timu iweze kufanya vizuri. Wanachokihisi nimehisi mara nyingi kupitia timu ya Manchester hivyo hata ikitokea wakatamka maneno makali nitavumilia, ingawa mara nyingi nimeona upendo wao na wakinipa moyo,” anasema.

YAKO 03

FUNZO KWA CAMARA

Anasema kipa namba moja wa klabu hiyo, Moussa Camara aliyemaliza msimu uliopita na clean sheets 19 chini yake vipo vitu vingi alivyojifunza vinavyomuongezea thamani katika majukumu.

“Katika timu ukikutana na kipa namba moja ujue ana vitu vingi. Msimu wake wa kwanza kaibuka na clean sheets 19. Hilo siyo jambo jepesi. Miongoni mwa vitu alivyo navyo ana nidhamu ya juu iliyogawanyika katika maeneo mengi,” anasema Yakoub.

“Anazingatia muda wa mazoezi, kupumzika, chakula, siyo mchezaji anayejivuta na ana bidii ya kufanya mazoezi. Hivyo ninapomwangalia kuna vitu ninavyoongeza vya ziada katika mazoezi ninayofanya ili ninapopata nafasi ya kucheza mechi niweze kuonyesha kiwango cha kuisaidia timu.”

Ukiachana na Camara, anasema maisha ya Simba yamemsaidia kukomaa kiakili na kutambua kwamba hawezi kukaa katika klabu hiyo milele, jambo linalompa nguvu ya kila anachofanya kuzingatia nidhamu.

“Akili yangu nimeijenga, kama nilivyosajiliwa mimi na mwingine akaondoka, inanifunza kuwa na nidhamu na pesa ninayoipata ili kufanya kitu cha maana. Kujulikana kusinifanye nijione wa kipekee kuliko wengine badala yake unyenyekevu kwangu unaongezeka kwani bado nina safari ndefu,” anasema.

“Ingawa ninapokuwa Zanzibar hasa nikipita mtaani ninapoombwa pesa ikitokea nikawa sina, watu hawaamini wanaona nina pesa nyingi. Lakini napaswa kukabiliana na changamoto hiyo.”

YAKO 04

MECHI NGUMU

Yakoub anasema tangu alipojiunga na Simba hajapata mechi ngumu, kwani hajacheza mara nyingi mbele ya Camara.

“Bado sijakutana na ugumu nimecheza mechi za kawaida, ila nakumbuka wakati nipo JKT Tanzania tulifungwa na Simba 1-0 dakika za nyongeza Uwanja wa KMC, ile mechi ilikuwa ngumu sana.”


STARS

Kuhusu Stars anasema: “Kucheza Taifa Stars imeniongezea vitu vingi kwani tunakutana wachezaji kutoka timu tofauti tunaocheza Ligi Kuu na wanaocheza nje ya nchi. Ili uwe mchezaji mkubwa lazima ujue vitu gani unapaswa kufanya na vingine kuviacha. Bado naendelea kujifunza vitu vingi,” anasema.

YAKO 06

AMTAJA KASEJA

Kipa huyo anasema wakati anakua alikuwa anamfuatilia kipa wa zamani wa Simba, Yanga, Kagera Sugar na Taifa Stars, Juma Kaseja kutokana na kiwango pamoja na uhodari wa kuokoa penalti.

“Kaseja alikuwa anajiamini ilikuwa ngumu kumfunga mipira ya karibu ama penalti. Kiwango chake hakiwezi kusahaulika bado jina lake lina heshima kubwa katika jamii ya wanamichezo, hivyo na sisi tunapaswa kufanya makubwa ya kuzungumziwa na watu,” anasema.


ASKARI, SOKA

Yakoub ni askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) na hapa anasema: “Unaposajiliwa na timu mfano mkataba wa miaka miwili (JKU) wanakuacha ufanye kazi hadi umalize mkataba kisha unarejea kwao. Ukija timu nyingine lazima utokee mikononi mwao.”

Anaongeza: “Ndio maana kila unaposaini mkataba lazima ugawane pesa na waajiri wako, mfano Simba iliponisajili JKU ilipata.”

YAKO 07

KAKA’AKE MSAADA

Yakoub anamtaja kaka yake Mohamed Seif Belo,  mchezaji wa zamani wa Amani Fresh, Sharp Boys, Polisi Zanzibar na Polisi Dodoma kabla haijashuka Ligi Kuu Bara namna anavyomsaidia kupambana.

“Kaka yangu anafuatilia kila nachokifanya na wakati mwingine nafanya naye mazoezi. Amekuwa msaada mkubwa katika kazi yangu. Baada ya mechi anaweza akaniambia umepatia hiki na kukosea kile. Nakumbuka wakati nasajiliwa kutoka JKT Tanzania kwenda Simba alinitaka niwe na utulivu mkubwa,” anasema kipa huyo.