Prime
Ya Sowah, Kante na Aucho ni matokeo ya kupora kazi za refa
Muktasari:
- Kamati iliwasimamisha wachezaji wawili wa Simba na mmoja wa Singida Black Stars baada ya kufanya makosa ambayo hayakuadhibiwa na mwamuzi wa kati, ambaye kimpira maoni yake ndio ya mwisho.
JUMANNE Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Kuu, maarufu kama Kamati ya Saa 72, ilitangaza adhabu kwa wachezaji watatu, ikionekana kama inataka kuweka usawa kwa Simba na Yanga kutokana na adhabu ilizowahi kutoa awali.
Kamati iliwasimamisha wachezaji wawili wa Simba na mmoja wa Singida Black Stars baada ya kufanya makosa ambayo hayakuadhibiwa na mwamuzi wa kati, ambaye kimpira maoni yake ndio ya mwisho.
Kamati ya Saa 72 imemfungia kiungo wa Simba, Alassane Maodo Kante, raia wa Senegal kucheza mechi tano na faini ya Sh1 milioni. Kosa lake lilikuwa ni kumpiga teke kiungo wa Azam FC, Feisal Salum baada ya kudondoka chini wakati akiulinda mpira.
Adhabu kama hiyo amepewa mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah, raia wa Ghana, kwa kosa la kumpiga kwa kiwiko kiungo wa Azam, Himid Mao wakati akitaka kumpokonya mpira ndani ya eneo la penalti la lango la matajiri hao wa Chamazi. Ila cha ajabu tukio la Himid dhidi ya Kante aliyekuwa ameshauacha mpira na kumbwaga chini na kumkanyanga pia. Hili halikuonwa na adhabu haijatoka!
Pia kiungo wa Singida Black Stars, Khalid Aucho amepewa adhabu hizo mbili za kukosa mechi tano na kutozwa faini, baada ya kumsukuma mchezaji wa TRA United, Adam Adam.
Sakata la kufungia wachezaji kwa kufanya makosa wakati mchezo haujasimama linaonekana kuendelea kuwa sugu na kwa adhabu hizo za Jumanne, idadi ya wachezaji walioadhibiwa mezani kwa makosa ya kimchezo na ambayo yalitakiwa yaadhibiwe na refa, sasa ni takriban watano. Na idadi hiyo hatujui itaendelea kukua kwa kiasi gani.
Adhabu hizo zilianza kuibua mijadala wakati Kamati ya Saa 72 ilipomuadhibu beki wa Yanga, Ibrahim “Bacca” Abdullah baada ya picha za marudio za video kumuonyesha akimpiga teke mchezaji wa Mbeya City, Ibrahim Ame wakati akiokoa mpira. Refa hakuliona tukio hilo wala kupuliza filimbi kusimamisha mchezo.
Pia mchezaji wa JKT Tanzania, Mohamed Bakari alifungiwa mechi tano na kutozwa faini kama hiyo baada ya picha za marudio kumuonyesha akimkanyaga kwa makusudi beki wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda.
Kwa matukio hayo, utaona kuwa Kamati ya Saa 72 inajaribu kufanya kile kinachoitwa ‘kubalance’ adhabu ili isionekane inapendelea au inafanya kwa njama kuhujumu timu.
Lakini ukweli inavuruga ligi na kupoteza ladha na itafikia wakati italazimika kufanya maamuzi mengi yasiyostahili kwa sababu tu inataka ionekane inatenda haki.
Kwa kawaida mwamuzi anatakiwa afanye uamuzi kwanza na picha za marudio zithibitishe uamuzi wake. Pale ambapo hajafanya uamuzi kwa tukio ambalo hakupuliza filimbi, hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kufanya uamuzi.
Ndio maana hata teknolojia ya Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) inamshauri refa aende katika runinga ya pembeni ya uwanja kuangalia vizuri tukio ambalo ama hakuliona au aliliona lakini hakuliona vizuri. Baada ya hapo, uamuzi unakuwa wake na ndio unakuwa wa mwisho.
Kama tafsiri ya tukio hilo itakuwa na kasoro, refa ndiye atawajibika. Na hata kabla ya kumshauri refa aende kwenye runinga, V.A.R huangalia picha za marudio kwa makini kabla ya kumwambia akajihakikishie au alifanya uamuzi sahihi.
Hivyo tabia ya kutaka kuonyesha kuwa tunaweza kutumia teknolojia ndogo tuliyonayo kufanya uamuzi yaliyotakiwa kuchukuliwa na refa ni kuanza kuvuruga mpira wa miguu. Hii ni kwa sababu kama hiyo ya kutaka ‘kubalance’ adhabu wakati mengine yanatokea wakati mpira umesimamishwa kwa sababu ya tukio hilo.
Kama tukio la Sowah, refa aliliona na kupuliza filimbi, lakini tafsiri yake haikuwa kwamba alimpiga Mao na kiwiko, tofauti na tukio la Bacca ambalo refa hakuliona kabisa. Haya ni matukio mawili tofauti, lakini kwa sababu moja limetokea kwa mchezaji wa Simba na jingine kwa mchezaji wa Yanga, basi Kamati iliona ni lazima adhabu zilingane, kitu ambacho si sahihi.
Na ili kujilinda, Kamati ya Saa 72 hutumia kanuni ya 41:21 kuhusu udhibiti wa wachezaji inayoeleza kuwa adhabu hizo za faini na kufungiwa kuanzia mechi tatu zitatolewa kwa mchezaji ambaye atakataa kujiunga na timu ya taifa, kupiga/kupigana kabla, wakati na baada ya mchezo, kumshambulia mwamuzi, kiongozi au mtazamaji kwa namna yoyote ile, kufanya kitendo chochote cha aibu kama vile kukojoa uwanjani, kukataa kupeana mkono na mgeni rasmi, waamuzi na wachezaji wa timu pinzani au kutoa au kuonyesha ishara ya matusi.
Pia, mchezaji atakayepewa adhabu hiyo ni yule atakayefanya vitendo vinavyoashiria ushirikina au uchawi na kufanya kitendo chochote kile kitakachobainika kuwa ni kinyume cha maadili ya mpira wa miguu.
Ukiangalia makosa hayo utabaini kuwa mengine ni ya kinidhamu yanayostahili kushughulikiwa na Kamati ya Nidhamu, mengine ni ya kimaadili na mengine ni yale yanayotokea wakati refa amesimamisha mchezo.
Ndio maana wenzetu huwashtaki wachezaji walioonyesha ishara inayotafsiriwa kuwa ni matusi na mtuhumiwa hutakiwa kujitetea. Haya ni masuala ya kinidhamu na si ya refa.
Hivi kama mpira ukiwa goli A halafu kipa wa goli B akatoa lugha ya matusi kwa mashabiki hadi wakaanza kumrushia chupa, kamati itathibitishaje kuwa kulikuwa na maneno ya matusi yametolewa na kipa? Ni lazima afikishwe mbele ya Kamati ya Nidhamu kujitetea.
Mfano kupigana ni tofauti na kupiga. Tukio la Sowah sidhani kama linaweza kutafsiriwa kama kupiga au kupigana. Kosa lake ni kucheza mchezo wa hatari kwa kuwa alikuwa akitumia nguvu nyingi kutaka kumpora mpira Mao. Kwa hiyo kosa lilikuwa la mwamuzi kwa kutafsiri vibaya au uzembe kwa kuwa picha za marudio za video zinaonyesha akiangalia na ndio maana akapuliza filimbi kusimamisha mchezo. Hapo adhabu ingeenda moja kwa moja kwa refa.
Tukio la Bacca halikupuliziwa filimbi na refa na hivyo, kamati ya wataalamu wa uamuzi walitakiwa walitathmini kwa kuangalia umbali wa eneo ambalo refa alikuwepo na kama alizingwa asilione na ikijiridhisha kuwa aliliona, adhabu inakwenda moja kwa moja kwa refa. Kama wataalamu watajiridhisha kuwa hakuwa sehemu nzuri ya kuliona tukio, mwamuzi alitakiwa aonywe na mchezaji asiadhibiwe.
Lakini tukio la Lusajo lilitokea wakati filimbi ishapulizwa na hivyo Kamati ya Saa 72 ilikuwa na haki ya kujiridhisha kwa kutumia teknolojia na kuadhibu kwa kadri kanuni zinavyotaka. Kwa hiyo, ni dhahiri kuwa matukio tofauti yameadhibiwa kwa adhabu moja ili kuweka uwiano badala ya kutenda haki. Kuweka uwiano ni kuharibu mpira wa miguu. Kila mchezaji, kiongozi, shabiki, refa au kocha ni lazima aadhibiwe kulingana na kosa lake na si kuangalia siku chache zilizopita aliadhibiwa nani na adhabu ilikuwaje ili ‘kubalance’.
Kama Kamati ya Saa 72 imeadhibu wachezaji watano kwa kuwazuia kucheza mechi tano wakati msimu haujafikia hata nusu, hali itawale wakati duru la kwanza litakapomalizika? Kila tunapoathiri uwezo wa timu kwa maamuzi yanayoepukika, tunaathiri mchezo, tunapoteza ladha kwa mashabiki, tunakimbiza wawekezaji na kuondoa ushindani wa kweli.
Kwa teknolojia tuliyonayo sasa, hatutakiwi kuingilia kazi za waamuzi. Hata wenzetu waliofikia uwezo wa kuwa teknolojia tofauti uwanjani, bado wanamwachia refa afanye jukumu lake kuu katika mpira la kuamua kwa kumuongezea uwezo wa kuona tukio kwa pande tofautti ili afanye uamuzi sahihi kuliko aliofanya awali au ambao hakuufanya.
Ni matukio mengi ambayo refa hayaoni kama lile la Kitambala kuvutwa jezi ndani ya eneo la penalti. Sasa Kamati ya Saa 72 itaamuru timu zirudi uwanjani ili penalti ipigwe? Liko lile la Djigui Diarra la kumsukuma mshambuliaji wa timu ya Mtibwa Sugar refa hakulitolea uamuzi. Kamati itaamuaje katika hilo?
Hivi kama refa hakupuliza filimbi ya kuashiria goli baada ya kutoona mpira uliovuka mstari, Kamati ya Saa 72 itaamua kuwa ni bao? Ndio maana nasema Kamati ijiepushe na matukio yanayotokea wakati mchezo haujasimamishwa. Hayo ni ya mwamuzi hata kama kulikuwa na mchezo wa hatari. Iwawajibishe waamuzi ili wawe makini zaidi.
Kazi ya mwamuzi ibakie kuwa ya mwamuzi na hilo ndilo nasisitiza kila siku. Bado hatuna teknolojia ya kutuwezesha kufanya uamuzi ambao haukufanywa na refa wakati hajapuliza filimbi ya kusimamisha mchezo!