Prime
Kila la kheri Aldof Mtasingwa, hauna baya
WAKUBWA wapo wengi lakini wakubwa zaidi wapo wawili tu pale Afrika Kusini katika ardhi ya Madiba. Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Huyu Mamelodi Sundowns amejitokeza miaka ya karibu kwa sababu ya noti za tajiri anayeitwa Patrice Motsepe. Vinginevyo Mamelodi wangekuwa kama Chippa United tu.
Ni kama tu Azam ilivyojitokeza miaka ya karibuni kuwa timu kubwa baada ya familia ya Bakhresa kuamua kuwekeza katika mpira. Mamelodi ni Azam ya Afrika Kusini ingawa yenyewe imekuwa ikifanya vizuri zaidi katika miaka ya karibuni kiasi cha kuchukua ubingwa wa Ligi kuu mara nyingi na kutwaa ubingwa wa Afrika mara mbili katika miaka ya karibuni.
Kwa hiyo majuzi nimesikia furaha baada ya kijana wetu, Aldof Mtasingwa kutangazwa kuwa mchezaji mpya wa Kaizer Chiefs.
Wachezaji wetu wengi wameenda Afrika Kusini kujaribu bahati zao lakini hakuna aliyecheza timu kubwa kama Mtasingwa. Shukrani kwake kwa kujaribu bahati yake Afrika Kusini halafu katika timu kubwa. Kaizer walishuka kidogo hapa mitaa ya kati lakini sasa wanataka kurudi kwa nguvu.
Kama Aldof akifanikiwa kuingia katika kikosi cha kwanza mara nyingi itakuwa faida kwetu. Mpira wa Afrika Kusini una ushindani mwingi na Kaizer inacheza mechi nyingi za kishindani.
Makocha wa Taifa Stars watapata faida kumwona mara kwa mara katika TV na kuna uwezekano akaitwa na kutusaidia. Tunahitaji wachezaji wanaocheza nje katika ligi za ushindani ili waweze kulisaidia Taifa.
Tayari kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Novatus Dismas, Himid Mao na wengineo wamewahi kufanya hivyo. Hata sasa hivi Alphonce Mabula ameingia katika kikosi cha kwanza cha Taifa Stars na analeta tofauti kubwa uwanjani. Mpira wa Ulaya umemsaidia kwa kiasi kikubwa.
Tetesi za kwamba anataka kurudi nchini kucheza Yanga hazinifurahishi sana. Bila ya kuwakosea heshima ambao wamekuwa wakicheza mpira wa ushindani miaka ya karibuni, lakini nadhani Mabula anacheza mpira wa ushindani zaidi alipo.
Hongera kwa Mtasingwa kukubali ofa ya kucheza Kaizer Chiefs. Tumewahi kusikia mara kadhaa wachezaji wetu walihitajika kucheza timu kubwa za Afrika lakini wanazipiga chini hizo ofa. Sababu tunaijua.
Wachezaji wetu wanapenda kucheza nyumbani. Nawajua wachezaji waliozipiga chini ofa za klabu mbalimbali za Afrika Kusini, TP Mazembe na klabu za Afrika Kaskazini.
Wachezaji wetu, hasa wa timu kubwa, wanapenda sifa za nyumbani. Hakuwi na msukumo mkubwa wa kucheza nje pindi zinapokuja ofa mbalimbali huku pia wakionekana kupata sifa nyingi nchini.
Mpira unapotoweka miguuni ndio wanajidai wanasaka ofa za kwenda nje. Imewahi kutokea mara kadhaa. Wakati wakiwa katika ubora wao wanakuwa na visingizio vingi vya kutoenda nchini.
Mtasingwa anaungana na kaka zake ambao wamewahi kukipiga Afrika Kusini. Hata hivyo hawakuwahi kugusa timu mbili kubwa za kitamaduni za Afrika Kusini. Hawa ni pamoja na Selemani Matola (Supersport United), Mrisho Ngassa - (Freestate Stars) Abdi Banda -Baroka Fc,Highlands Park
Abdulrazack Hamza (Supersport United) Ally Msengi (Stellenbosch) Gadiel Michael (Cape Town Spurs).
Wengine ni kina Baraka Majogoro (Chippa United) Abdulhalim Humoud (Jomo Cosmos), Uhuru Seleman (Royal AM), Yussuf Macho (Vaal Proffesionals & Jomo Cosmos), Bakari Malima- Vaal Proffesionals (Alikaa Muda mfupi na kurudi Tanzania), Nteze John -(QuaQua Stars) shukrani kwao. Walijaribu kupambania bendera ya taifa ugenini.
Kwa Mtasingwa nadhani imekuwa rahisi kwake kwa sababu ni mchezaji ambaye amezoea kucheza nje. Hata Azam walimchukua kutoka nje.
Ana 'exposure' ya kutosha hata ya kucheza Ulaya. Nadhani ndiyo maana kwake yalikuwa maamuzi rahisi kuliko kusubiri ofa za wakubwa wa nchi yetu Simba na Yanga ambao wamekuwa ndoto ya kila mchezaji wetu hapa nchini.
Wasiwasi kuhusu Mtasingwa? Nina wasiwasi mmoja tu. Amekuwa nje kwa muda mrefu. Hata Azam hakuitumikia vema. Je amepona kikamilifu au ana 'fitness' ya kutosha kuweza kuitumikia Kaizer Chiefs? Kwa Mtasingwa ninayemfahamu, kama yupo fiti basi anacheza Kaizer Chiefs bila ya wasiwasi. Kipaji kipo. Kipaji kizuri tu cha kuzima dimba la kati kwa wababe hawa wa Soweto.
Wasiwasi mwingine? Ni namna ambavyo anaweza kukabiliana na presha ya kucheza timu kubwa ya nje ya nchi yako. Hata hivyo, najikumbusha tu Samatta na Msuva wamewahi kucheza katika timu kubwa nje ya nchi yao na walimudu presha ya kucheza katika mazingira hayo. Sidhani kama Mtasingwa atashindwa.
Ninachosubiri kwa hamu? Ni kama ataweza kuwa Mtanzania wa kwanza kuzima dimba katika pambano la watani wa Soweto (SOWETO DERBY).
Kitakuwa kitu cha kusisimua. Waafrika Kusini wanaipenda hii mechi kama ambavyo Watanzania wanaipenda mechi ya Simba na Yanga. Itapendeza Mtanzania kucheza Soweto Derby na ataashiria namna ambavyo tunaendelea kupambana kujipambanua katika soka.
Bahati nzuri kwake pia ni kama akizima vizuri dimba la Kaizer Chiefs basi muda si mrefu tutaona namna ambavyo atakuwa anapambwa na vyombo vya habari vya Afrika Kusini.
Waafrika Kusini wapo kama sisi hawajambo kwa kuwapamba wachezaji wanaocheza katika ligi yao. Wapo kama Waingereza. Hawajambo kwa kuwapamba wachezaji wao wanaocheza katika timu kubwa.
Kama akizima vema katika dimba anaweza kujikuta pia katika mshahara mzuri siku za usoni. Au akajikuta akitamaniwa na wakubwa wengine wa Afrika Kusini.
Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns. Huwa inatokea mara nyingi. Wachezaji wa hizi klabu huwa ni matajiri. Wanalipwa hela nzuri na wanaishi kifahari. Ni tofauti na wachezaji wa timu za kawaida kina Chippa United.
Kama Mtasingwa pia atacheza mpira maridadi basi ataingja katika mioyo ya mashabiki wa Afrika Kusini. Na kwa mujibu wa takwimu Kaizer Chiefs ndio timu yenye mashabiki wengi zaidi kuliko Orlando Pirates na wengineo. Mashabiki wao ni wepesi pia kuwasifia wachezaji wao na kuwapachika majina ya utani.
Tumwombee afanikiwe. Tusisahau pia kumweka katika maombi yetu. Hawa ndio wachezaji ambao wanaweza kutubeba katika michuano ya Afcon ambayo itafanyika katika ardhi ya Afrika Mashariki Desemba mwakani. Tunahitaji wachezaji wenye 'exposure' kama yeye. Kila la kheri kwa Aldof. Hana baya.