Prime
Soka la vijana hatarini, TFF ishtuke
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ametangaza nia yake ya kufuta mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 kwa maelezo udanganyifu wa umri umekithiri.
Amesema tatizo la udanganyifu ni kubwa hivyo anaona ni bora aanzishe mashindano kwa ajili ya wachezaji wa akiba ili klabu badala ya kudanganya umri zitumie mashindano hayo kwa wachezaji ambao hawapati nafasi na kuchanganya na hao vijana wanaodaiwa kuwa na umri bandia.
Ni kweli tatizo la udanganyifu wa umri ni kubwa katika nchi ambayo cheti cha kuzaliwa kinaweza kubadilishwa ndani ya saa chache na mtu akawa na umri tofauti siku inayofuata.
Tatizo hili limesababisha wachezaji wengi ambao huonekana wanang’aa kwenye timu za vijana kutoweka ghafla wasieleweke wamepotelea wapi. Wengi wanakuwa wameshatumika sana ila kwa sababu ya maumbile yao hugeuzwa chipukizi.
Wanapofikia umri wanaodhaniwa ndiyo watakuwa wamekomaa, kumbe wanakuwa tayari wameshachoka na ndiyo maana uzalishaji wa nyota wazawa umekuwa ni mgumu sana.
Wale waliopitia kwenye timu za umri kwa usahihi hudumisha kiwango chao kwa muda mrefu. Angalia wachezaji kama Mohamed “Tchabalala” Hussein, Farid Mussa, Mudathir Yahya na Aishi Manula walitokea mashindano ya Coca Cola ya U17 wakati Si Yanga, wala Azam FC wala Simba walikuwa wanawajua. Katika umri mdogo wakapikwa na Kim Poulsen.
Poulsen alisisitiza wakati huo Manula atakuja kuwa hazina ya taifa, na akawa. Wote bado wako kwenye klabu kubwa na wanacheza kwa kiwango cha juu zaidi ya miaka 14 tangu washiriki Coca Coca.
Maana yake ni kwamba bado kuna wachezaji wenye umri sahihi wanaoweza kunufaika na mashindano ya umri, ila inatakiwa kuendelea kutafuta suluhisho la kupambana na hao wengine wanaokuwa na umri bandia.
Suluhisho la tatizo si kulikimbia bali kupambana nalo. Na kama tunakiri kuwa udanganyifu ni mkubwa katika mashindano ya U20, basi tujue tatizo ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria kwa kuwa hao U20 hawatoki hewani. Ni haohao ndio waliotoka kucheza timu za U17. Inawezekanaje kukawa na udanganyifu kwenye timu za U20 halafu kukawa hakuna tatizo kwenye U17?
Tunaelewa hata timu ya taifa ya vijana ya U17 iliyofanya vizuri mashindano ya Afrika hivi karibuni ina wachezaji ambao umri wao una shaka kwa kuangalia rekodi zao katika klabu walizopitia. Hivyo tatizo ni kubwa kuliko tunavyolielezea ili kuhalalisha maamuzi yasiyo ya kimpira.
Sidhani kama kufuta mashindano ya U17 kutakuwa ni suluhisho la tatizo la udanganyifu wa umri. Ni lazima tujitume kutafuta suluhisho sahihi ili kuendelea kutumia program za umri ambazo zimeshajaribiwa duniani kote na kutoa matunda mazuri.
Isitoshe hivi sasa kuna mwamko mkubwa wa kuanzisha timu za watoto katika maeneo mbalimbali nchini. Taasisi, watu binafsi na klabu zimeamua kuanzisha timu za watoto, kitu ambacho ni chanya kwa shirikisho.
Kinachotakiwa ni shirikisho kubuni mbinu za uratibu na kuwawekea jukwaa la kushindana katika mikoa, kanda na taifa. Hili likishakaa vizuri, tatizo la udanganyifu wa umri litapungua sana kwa kuwa itakuwa rahisi kufuatilia taarifa za mchezaji kutoka alikoanzia na wenzake watakuwa wanamjua.
Jitihada hizi za wananchi zafaa zienziwe ili kuwapa moyo na kuhamasisha watu wengi zaidi waanzishe ili kutengeneza kundi kubwa la wachezaji waliokuzwa kwenye vituo vya soka na kupata mafunzo sahihi.
Ni kwa jinsi hiyo, ni lazima TFF itengeneze sera ya uendeshaji wa shule hizo, ikiwa ni pamoja na kulazimisha ziwe na walimu sahihi waliothibitishwa, ufuatiliaji wa elimu yao, afya na mambo mengine ya msingi kwa watoto. Hilo litatengeneza vijana bora wa baadaye walio na umri sahihi kiasi kwamba wale vijeba wataona aibu kujumuika na vijana sahihi.
Mbali na hayo, program ya kuwapa wananchi kitambulisho cha taifa itasaidia kutunza taarifa za watu kwa kuwa wataingia kwenye kanzidata kwa kupitia utambulisho wa wazazi au ndugu zao.
TFF pekee haiwezi kupambana na tatizo la udanganyifu wa umri bali kwa kuunganisha nguvu za wadau wote, ikiwemo serikali. Ikiwa mchezaji atabainika kughushi cheti cha kuzaliwa, ni lazima awajibishwe kama mhalifu. Hilo litaihusu serikali na litakimbiza vijeba wengi kwa kuwa kosa la kughushi ni jinai.
Ni wakati sasa wa TFF na wanachama wake katika ngazi ya mikoa na wale wa wilaya kuanza kufikiria wataunganisha jitihada zinazofanywa na wananchi kuanzisha shule za soka na ni vipi itazitumia kutengeneza kundi kubwa la wachezaji wa baadaye ambao wana umri sahihi na wamepata mafunzo sahihi na si kufuta mashindano kwa sababu ya tatizo.