Wikiendi ya shughuli Ligi Kuu England
Muktasari:
- Manchester City bado inaongoza ligi kwa tofauti ya mabao baada ya kucheza mechi nane, ingawa mwanzo wake mzuri wa msimu ulisitishwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufungwa mabao 2-1 na Aston Villa, ambayo imekuwa ikionyesha kiwango kinachozidi kuimarika.
LONDON, ENGLAND: WIKIENDI nyingine ya moto! Raundi ya tisa ya Ligi Kuu England inaanza kupigwa leo Jumamosi, kesho Jumapili na keshokutwa Jumatatu katika viwanja tofauti, ambapo wakubwa watakuwa wakisaka kujitetea mbele ya wadogo zao.
Manchester City bado inaongoza ligi kwa tofauti ya mabao baada ya kucheza mechi nane, ingawa mwanzo wake mzuri wa msimu ulisitishwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufungwa mabao 2-1 na Aston Villa, ambayo imekuwa ikionyesha kiwango kinachozidi kuimarika.
City ina mtihani mwingine mgumu mwishoni mwa wiki hii itakapoikaribisha Brighton kwenye Uwanja wa Etihad, siku tatu tu baada ya kuiondoa timu hiyo kwa mikwaju ya penalti katika Kombe la Carabao.
Arsenal ilitolewa katika mashindano hayo kwa namna ya kushangaza, baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti na Fleetwood Town, na sasa itasafiri kwenda Liverpool katika mchezo mwingine mkubwa wa kesho, Jumapili.
Katika mchezo mwingine unaowakutanisha vigogo, Manchester United itaitembelea Chelsea. Kibarua cha kocha Michael Carrick kinaonekana kuwa hatarini zaidi Man United huku timu yake ikiwa haijashinda katika mechi nane mfululizo. Kabla ya kuanza kwa kundi jingine la mechi zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, hebu tuangalie utabiri Opta ulivyo.
CHELSEA VS MAN UNITED
Mchezo wa kwanza wa mwisho wa wiki utachezwa Stamford Bridge, na unaweza kuwa wa kuamua hatma ya Michael Carrick, ambapo kabla ya safari ya kwenda Chelsea, Manchester United haijashinda katika mechi nane za mashindano yote (sare 3, vipigo 5). Huo ni mwenendo wao mbaya zaidi tangu Oktoba na Novemba 1988, walipokuwa na mfululizo wa mechi tisa bila ushindi.
Tofauti na wachezaji wake ambao walizomewa na mashabiki wa Old Trafford baada ya kufungwa 3-0 nyumbani na Bournemouth wiki iliyopita, Carrick bado anaungwa mkono na baadhi ya mashabiki.
Hata hivyo, kipigo kingine kinaweza kufanya nafasi yake kuendelea kuwa kocha iwe shakani. Baada ya kufungwa 4-1 na Como katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya mchezo dhidi ya Bournemouth, United imepoteza mechi mbili mfululizo kwa tofauti ya mabao matatu.
Mara ya mwisho ilipofungwa mechi tatu mfululizo kwa tofauti ya mabao matatu au zaidi ilikuwa Novemba na Desemba 1961 na kwa maana hiyo haipewi nafasi kubwa ya kushinda mchezo huu. Ina uwezekano wa asilimia 23.7 wa kupata ushindi na 24.5 kuambulia pointi moja kwa sare huku Chelsea ikipewa asilimia 51.8 za ushindi.
Kocha wa Chelsea, Xabi Alonso, alipoteza mechi tano kati ya saba za Ligi Kuu England dhidi ya United akiwa mchezaji wa Liverpool (ushindi 1, sare 1). United ni miongoni mwa wapinzani ambao Alonso amepoteza mechi nyingi zaidi dhidi yao, sawa na Chelsea.
Mchezo wake wa mwisho dhidi ya United akiwa mchezaji alipokuwa Real Madrid, Machi 2013, ulimkuta akicheza katika safu ya kiungo. Chelsea inatarajia kurejea kwenye ushindi baada ya kufungwa 2-0 na Tottenham Hotspur, Jumamosi iliyopita. Pia ilitolewa katika Kombe la Caraba kwa penalti dhidi ya Liverpool Jumatano.
BOURNEMOUTH VS LEEDS UNITED
Baada ya kuifanya Manchester United ishindwe kuhimili mashambulizi yake mwishoni mwa wiki iliyopita, Bournemouth inayopewa asilimia 50.6 kushinda leo, inatarajiwa kuwa na morali kubwa kuelekea mchezo wa nyumbani dhidi ya Leeds United (asilimia 24.4) katika Uwanja wa Vitality.
Baada ya mfululizo wa mechi nane bila ushindi, Bournemouth imeshinda mbili mfululizo za ligi hiyo bila kuruhusu bao. Haijawahi kushinda mechi tatu mfululizo za mashindano hayo bila kufungwa.
Leeds, kwa upande mwingine, haijashinda katika mechi nne zilizopita, ingawa tatu kati ya hizo ziliisha kwa sare. Bournemouth (13) na Leeds (14) ni miongoni mwa timu tatu zilizo na sare nyingi zaidi katika Ligi Kuu England mwaka 2026. Brentford pia ina sare 14. Kwa hiyo, uwezekano wa asilimia 25 wa mchezo huo kuisha kwa sare haupaswi kupuuzwa.
Hata hivyo, huenda mchezo ukawa na matukio ya kusisimua mwishoni, kwa kuwa mechi tatu kati ya nne zilizopita za ligi kati ya timu hizo zilikuwa na bao lililofungwa dakika ya 90. Mechi zote mbili za msimu wa 2025/26 zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2, huku timu ya ugenini ikisawazisha dakika za mwisho.
BRENTFORD VS NOTTINGHAM
Brentford (asilimia 50.3) na Nottingham Forest (asilimia 24.5) zote zinatafuta kurejea kwenye ushindi wa ligi baada ya kupitia vipindi vigumu.
Brentford imepoteza mchezo mmoja msimu huu (ushindi 2, sare 5), lakini haijashinda katika mechi tatu zilizopita. Hata hivyo, ina rekodi nzuri nyumbani katika Uwanja wa Gtech Community, ikiwa imepoteza mchezo mmoja kati ya tisa za mwisho katika ligi (ushindi 3, sare 5). Kipigo hicho kilitokea mara ya mwisho walipocheza nyumbani dhidi ya Liverpool.
Forest, kwa upande mwingine, ilisitisha mfululizo wa vipigo vitatu kwa sare dhidi ya Ipswich Town wiki iliyopita, lakini haitegemei kupata matokeo bora zaidi leo. Imepoteza mechi tano za mwisho za ligi zilizochezwa Oktoba 31.
Mfululizo huo ulianza katika msimu wa kwanza wa ligi hiyo 1992/93 ilipofungwa 1-0 na Ipswich. Hata hivyo, Forest ina rekodi nzuri karibuni dhidi ya Brentford ikishinda mechi tatu kati ya nne zilizopita, huku ikipigwa mara moja.
Imeshinda mechi mbili za mwisho dhidi ya timu ya hiyo, lakini imewahi tu kushinda mechi tatu mfululizo katika pambano hilo mara moja wakati huo zikiwa Championship kati ya Februari 2019 na Januari 2020.
COVENTRY CITY VS SUNDERLAND
Timu mbili za mwisho kwenye msimamo zinatafuta kupunguza presha ya mwanzo wa msimu, huku Coventry City ikiikaribisha Sunderland.
Coventry, ambayo imepoteza mechi mbili za mwisho za ligi ina uwezekano wa asilimia 43.2 wa kushinda. Haijapoteza katika mechi 10 za ligi dhidi ya Sunderland (ushindi 5, sare 5), huku matokeo yakibadilishana kati ya sare na ushindi katika kila mchezo.
Sunderland, ambayo ina uwezekano wa asilimia 30.1 wa kushinda haijashinda katika mechi sita za ligi (sare 2, vipigo 4). Imeshindwa kufunga bao katika kila moja ya mechi zake tatu zilizopita, baada ya kutoka suluhu (0-0) na Leeds United mara ya mwisho.
Kuna uwezekano wa asilimia 26.7 wa mchezo huu kuisha kwa sare nyingine, na huenda pia mabao yakawa magumu kupatikana. Timu hizo zina idadi ndogo zaidi ya mabao katika ligi msimu huu zikiwa zimefunga mara sita kila moja. Coventry pia imefunga mabao machache zaidi katika kipindi cha kwanza, ikiwa na bao moja, huku Sunderland ikifunga mabao machache zaidi katika kipindi cha pili ikiwa na matatu.
HULL CITY VS IPSWICH TOWN
Baada ya kushinda mechi mbili za mwanzo wa msimu, Hull City imeshindwa kupata pointi zote tatu katika mechi sita zilizofuata za ligi (sare 4, vipigo 2) na sasa itajaribu kubadilisha hali hiyo itakapocheza dhidi ya Ipswich Town, timu nyingine iliyopanda daraja. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana katika ligi ya daraja la juu.
Ingawa Hull inapewa nafasi kubwa ya asilimia 45 kushinda, lakini haijashinda katika mechi tano za ligi dhidi ya Ipswich (sare 1, vipigo 4).
Ipswich Town ina uwezekano wa asilimia 28.1 wa kushinda na inajua kuwa ushindi utaifanya kuipita Hull kwenye msimamo wa ligi. Kumbuka kwamba Ipswich imeshinda mechi mbili kati ya tatu za mwisho za ligi ilizocheza ugenini dhidi ya Hull, huku nyingine ikiisha kwa sare.
Changamoto za Ipswich katika ulinzi zinaweza kuigharimu kwa kuwa imefungwa bao katika kila moja ya mechi 27 za mwisho za Ligi Kuu.
Hull, kwa upande mwingine, iko katika mfululizo wa kutoshinda mechi sita za ligi sawa na Man United na Sunderland. Kwa hiyo, uwezekano wa asilimia 26.9 wa mchezo kuisha kwa sare unaweza kutimia. Huo ndio mchezo unaotabiriwa zaidi kuisha kwa sare wiki hii.
MAN CITY VS BRIGHTON
Baada ya mechi ya raundi ya nne ya Kombe la Carabao kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, Manchester City na Brighton zitakutana tena haraka katika Uwanja wa Etihad, ambapo wenyeji wanapewa asilimia 56.3 kushinda, ikilinganishwa na asilimia 21.1 za Brighton.
City (16.7) na Brighton (16.2) ndizo timu mbili zinazoongoza kwa takwimu za mabao yanayotarajiwa kufungwa katika ligi hiyo msimu huu. Pia ndizo timu zilizofunga mabao mengi zaidi, Brighton ikiwa na 23 na City 20. Kwa hiyo, mchezo huu unatarajiwa kuwa na mabao mengi na matukio ya kusisimua. Erling Haaland atakuwa na hamu ya kuboresha rekodi dhidi ya Brighton, baada ya kuifunga timu hiyo mara kwa mara.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway amefunga mabao saba katika mechi saba za ligi hiyo dhidi ya Brighton, ambapo ametupia bao katika kila moja ya mechi nne za mwisho, lakini hajashinda mchezo wowote kati ya hiyo (sare 2, vipigo 2).
Haaland ni mmoja kati ya wachezaji watatu waliowahi kufanya hivyo katika historia ya Ligi Kuu England pamoja na Jimmy Floyd Hasselbaink dhidi ya Man United (Novemba 1998 hadi Februari 2001) na Charlie Austin dhidi ya Arsenal (Desemba 2014 hadi Aprili 2018).
SPURS VS CRYSTAL PALACE
Kuna mechi mbili za mwisho Jumamosi; ya kwanza ni pambano la London kati ya Tottenham Hotspur ya Roberto De Zerbi, ambayo imekuwa ikirejea kwenye kiwango kizuri, na Crystal Palace ya Pierre Sage ambayo imekuwa ikisuasua.
Spurs imeshinda mechi mbili za mwisho za ligi hiyo ikiwa ni ushindi mmoja tu pungufu ya ule ilioupata katika mechi 26 zilizotangulia (ushindi 3, sare 10, vipigo 13). Mara ya mwisho iliposhinda mechi tatu mfululizo ilikuwa Februari 2025.
Palace, kwa upande mwingine, iko juu kidogo ya eneo la kushuka daraja baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo. Ina uwezekano wa asilimia 22.3 tu wa kushinda. Tangu ilipoifunga Fulham 2-1, Desemba 7, 2025, matokeo yaliyoiweka nafasi ya nne katika ligi imepoteza mechi nyingi zaidi (17) na kuruhusu mabao mengi zaidi (58) kuliko timu nyingine yoyote katika mashindano hayo.
Hata hivyo, ilifanikiwa kuifunga tena Fulham, Jumatano, katika Kombe la Carabao kwa bao 1-0, na kupata kiasi cha kujiamini kuelekea mchezo huu. Spurs inapewa uwezekano wa asilimia 54.2 wa kupata ushindi mwingine, kwani baada ya kuifunga Coventry na Chelsea, inaweza kuwa timu ya kwanza kushinda mechi tatu mfululizo za ligi dhidi ya timu ambazo majina yake yote yanaanza na herufi moja tangu 2018. Mwaka huo, Burnley iliifunga West Ham, West Brom na Watford.
ASTON VILLA VS FULHAM
Mchezo wa mwisho leo utaikutanisha Aston Villa, ambayo ndiyo timu yenye nafasi kubwa zaidi ya kushinda katika raundi ya tisa kwa asilimia 57.9, na Fulham ambayo ina uwezekano wa asilimia 20.2 wa kupata ushindi.
Villa imekuwa na tabia ya kuanza msimu kwa kusuasua kabla ya kuimarika katika miaka michache iliyopita. Imeshinda mechi mbili kati ya 12 za mwisho za Ligi Kuu katika miezi ya Agosti na Septemba (sare 5, vipigo 5). Hata hivyo, imeshinda mechi nane kati ya 10 za mwisho kati ya Oktoba na Novemba (sare 1, kipigo 1).
Kwa upande wake Fulham inatafuta kushinda mechi tatu mfululizo za ligi kwa mara ya kwanza tangu Desemba 2025. Takwimu zake za msingi chini ya Alvaro Arbeloa zimekuwa nzuri.
Wastani wa umiliki wa mpira wa Fulham (asilimia 58), pasi zilizofanikiwa kwa kila mchezo (505) na usahihi wa pasi (asilimia 86.7) msimu huu ni viwango vyake bora zaidi katika historia ya timu hiyo kwenye ligi hiyo tangu 2003/04. Hata hivyo, ushindi wake wote mar mbili ulipatikana dhidi ya timu zilizopanda daraja.
Kocha wa Unai Emery anayeifundisha Villa kwa sasa ameshinda mechi nane kati ya tisa za Ligi Kuu England dhidi ya Fulham, akiwa na wastani wa pointi 2.67 kwa kila mchezo dhidi yao.
Kati ya makocha waliowahi kusimamia mechi tano au zaidi dhidi ya Fulham, ni Pep Guardiola pekee (mechi tatu, ushindi 12 kati ya 12) na Mauricio Pochettino (mechi tatu, ushindi 6 kati ya 6) walio na wastani wa ushindi mkubwa zaidi.