Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

WAMOTO SI MCHEZO: Messi, Ronaldo wanavyoburuzwa na Giggs Ligi ya Mabingwa Ulaya

WAMOTO Pict

Muktasari:

  • Kabla ya Messi na Ronaldo kutawala tuzo ya soka za Ballon d’Or, Mfaransa huyo alikuwa mtengenezaji bora wa asisti na mchezaji bora zaidi barani Ulaya. Zidane pia alikuwa wa kwanza kufikia asisti 20 akimshinda David Beckham katika hatua zote hizo.

MADRID, HISPANIA: NUSU fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inapigwa leo, ambapo PSG itaikaribisha Bayern Munich katika dimba la Parc des Princes lililopo Paris, Ufaransa lenye uwezo wa kuchukua watu 47,929.

Wakati ukisubiri bonge la mechi inayokutanisha timu hizo mbili za moto kwa sasa Ulaya, kuna mastaa wawili waliowahi kuwa maarufu zaidi Ulaya katika kipindi cha miaka 30 iliyopita ambao ni Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, na wamekuwa wakishindana kuwa wafungaji bora na pia watengenezaji bora wa mabao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa sasa wote hawapo Ulaya, Messi akiwa zake Marekani anakoichezea Inter Miami ilhali Ronaldo yupo Saudi Arabia akichezea kikosi cha Al Nassr.

Hata hivyo, mjadala mkubwa unaoendelea unahusu nani ndiye mchezaji bora wa muda wote (GOAT) kati yao. Ingawa kila mtu anajua idadi ya mabao waliyoifunga katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hadi hivi karibuni hakuna aliyekuwa akijua nani ana pasi nyingi za mwisho (asist), kwa sababu hakuna chanzo kilichokuwa kimekusanya takwimu zote tangu Kombe la Ulaya lilipobadilishwa kuwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kutokana na juhudi kubwa za uchunguzi na utafiti wa kina wa timu ya Opta, inaweza kufichua kwa kipekee mchezaji mwenye pasi nyingi zaidi za mabao katika historia ya Ligi ya Mabingwa, ambapo na siyo Messi wala Ronaldo, ingawa wanakaribia sana.

Opta hutumia ufafanuzi unaokubalika zaidi wa asisti na mara zote huwa haijumuishi penalti zilizotengenezwa, wala kuhesabu pasi za mwisho kwa mabao yaliyotokana na mipira iliyookolewa, mipira ya kurudi (rebounds) au mipira iliyobadili mwelekeo kwa kiasi kikubwa.

Mara zote huchunguza video za mwendo wa polepole na ripoti rasmi ili kutengeneza hifadhi ya takwimu sahihi na thabiti zaidi duniani, na tofauti na vyanzo vingine, ufafanuzi wa watafiti hao hubaki kuwa uleule kila msimu na kila mashindano.

Kutokana na hali hiyo kuna wachezaji wanane waliofikisha asisti 30 au zaidi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo mchezaji wa kwanza kufikia asisti 10 alikuwa Zinedine Zidane.

Kabla ya Messi na Ronaldo kutawala tuzo ya soka za Ballon d’Or, Mfaransa huyo alikuwa mtengenezaji bora wa asisti na mchezaji bora zaidi barani Ulaya. Zidane pia alikuwa wa kwanza kufikia asisti 20 akimshinda David Beckham katika hatua zote hizo.

Manahodha wa zamani wa Ufaransa, Zidane na England, David Beckham walishindana walipokuwa wakicheza Juventus na Manchester United mtawalia, na baadaye walipokuwa pamoja Real Madrid kama sehemu ya “galacticos”. Theluthi moja ya asisti za Beckham zilitokana na mipira ya adhabu (set-pieces), wakati ni asilimia 16 tu ya Zidane zilizotokana na mipira ya kona au faulo.

Hata hivyo, Zidane hayupo katika 10 bora, akishika nafasi ya 12 kwa pamoja. Beckham alifanya vizuri zaidi kidogo kama utakavyoona. Hivyo basi, ni kina nani wachezaji watano bora wa muda wote kwa asisti katika Ligi ya Mabingwa Ulaya?

WAMO 06

5. DAVID BECKHAM (36)

David Beckham bila shaka ni mmoja wa wataalamu bora wa mipira ya adhabu kuwahi kuonekana katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Manchester United kilichoshinda mataji matatu (treble) na alishikilia rekodi ya asisti nyingi hadi mwaka 2011. Ni Luis Figo pekee aliye na asisti nyingi zaidi kutokana na mipira ya adhabu kuliko Beckham.

Asisti ya Beckham ya kwanza ilikuwa 1994 alipomsaidia Roy Keane kufunga dhidi ya Galatasaray. Alimaliza akiwa na asisti 29 alipokuwa  Manchester United kabla ya kuhamia Real Madrid na kuongeza nyingine saba. Dwight Yorke ndiye aliyenufaika zaidi na asisti zake sahihi, akifunga mabao sita kutokana na mipira ya Beckham. Hakuna mchezaji aliyechangia mabao mengi ya vichwa kuliko Beckham - 18 kati ya aliyotengeneza yalifungwa kwa kichwa.

WAMO 01

4. ANGEL DI MARIA (38)

Winga huyo wa Argentina amecheza katika ligi tano kati ya saba bora Ulaya kulingana na viwango vya UEFA. Asisti yake ya kwanza ilikuja akiwa Benfica dhidi ya Celtic 2007, kabla ya kuhamia Real Madrid ambako alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2013-14.

Baada ya muda mfupi Manchester United alihamia Paris Saint-Germain (PSG) ambako alitoa asisti 18 kati ya 36. Alimsaidia zaidi Kylian Mbappe kuliko mchezaji mwingine yeyote (mara tano). Baadaye aliongeza asisti nyingine Juventus kabla ya kurejea Benfica 2023. Asisti zake mbili dhidi ya Monaco zilimfikishia 38, akimpita Beckham. Kwa sasa naichezea Rosario Central ya Argentina.

WAMO 03

3. LIONEL MESSI (39)

Messi alisubiri hadi mechi yake ya sita katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kupata bao na asisti yake ya kwanza. Hii ilitokea dhidi ya Panathinaikos msimu wa 2005-06 katika ushindi wa Barcelona wa mabao 5-0. Asisti yake ya mwisho ilikuja alipomsaidia Kylian Mbappe kufunga dhidi ya Juventus walipokuwa wakicheza pamoja katika kikosi cha PSG. Mchezaji aliyempa asisti nyingi zaidi ni Neymar akifanya hivyo mara tano (nne Barcelona, moja PSG).

WAMO 04

2. CRISTIANO RONALDO (40)

Watu wengi hawajui kwamba Ronaldo hakufunga katika mechi zake 26 za kwanza za Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wakati huo alionekana zaidi kama mtengenezaji wa mabao kuliko mfungaji. Katika mechi yake ya 27 dhidi ya Roma, alitoa asisti kwa Michael Carrick walipokuwa wakikipiga pamoja Manchester United, kabla ya kufunga mabao mawili. Carrick ndio kocha wa muda kwa sasa wa timu hiyo. Baadaye alibadilika na kuwa mashine ya mabao. Asisti ya Ronaldo ya kwanza ilikuja dhidi ya Lyon 2004-05. Ana mchango mkubwa zaidi wa mabao katika fainali za Ligi ya Mabingwa (asisti tano).

WAMO 05

1. RYAN GIGGS (41)

Uwezo na kudumu muda mrefu vilimsaidia Ryan Giggs kuandikisha rekodi hii akiwa na Mashetani Wekundu (Manchester United). Alicheza kwa miaka 20 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kushinda mataji mara mbili. Asisti yake muhimu zaidi ilikuwa katika fainali ya 1999 aliyompatia Teddy Sheringham kusawazisha bao kabla ya ushindi wa dakika za mwisho. Pia alitoa asiist katika fainali ya 2011 dhidi ya Barcelona. Asisti yake ya mwisho ilikuja dhidi ya Bayer Leverkusen 2013. Pia ni mmoja wa wachezaji wachache waliotoa asisti nne katika mechi moja. Itakumbukwa kwamba katika maisha yake ya soka alichezea timu moja tu - Manchester United.


MASTAA WENYE ASISTI NYINGI LIGI YA MABINGWA ULAYA

Ryan Giggs   (41)

Cristiano Ronaldo  (40)

Lionel Messi (39)

Ángel Di María       (38)

David Beckham      (36)

Luís Figo                (34)

Xavi Hernandez     (31)

Neymar                 (30)

Kevin De Bruyne    (27)

Raul Gonzalez        (27)

Karim Benzema     (27)

Zinedine Zidane      (26)

Andrés Iniesta       (26)

Vinícius Junior       (26)

Thierry Henry        (25)

Dani Alves    (25)

Thomas Müller       (25)

Kylian Mbappe        (25)