Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joto la 33°c na zaidi, tahadhari kwa wachezaji na mashabiki

Muktasari:

  • Katika mechi hiyo, ambayo Azam ilishinda kwa mabao 2-1, kulikuwa na makundi ya mashabiki wengi jukwaani, wakiwa wamevua mashati, wakijipepea huku wakitokwa na jasho kwa wingi.

NIKIWA mmoja wa watazamaji wa mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Azam FC na JKT Tanzania iliyochezwa Jumamosi iliyopita katika Uwanja wa Jenerali Isamuyo jijini Dar es Salaam, nilishuhudia hali ya joto kali kwa mashabiki na wachezaji.

Katika mechi hiyo, ambayo Azam ilishinda kwa mabao 2-1, kulikuwa na makundi ya mashabiki wengi jukwaani, wakiwa wamevua mashati, wakijipepea huku wakitokwa na jasho kwa wingi.

Vilevile, kwa upande wa wachezaji, wengi hasa waliokuwa wakicheza uwanjani walikuwa wakivuja jasho lililowalowesha miili yao. Hali hii iliwafanya wachezaji wa pande zote mbili kunywa maji kiasi pale mpira uliposimama.

Pamoja na joto kuwa kali katika maeneo mengi ya Tanzania, hasa maeneo ya Pwani, bado wachezaji waliweza kucheza bila kupata athari zitokanazo na joto kali, ikiwamo kubanwa kwa misuli, kuhisi kupoteza nguvu, kuumwa kichwa na kupoteza fahamu.

Ukweli ni kwamba mchezaji ambaye amezoea kucheza kwa muda mrefu katika mazingira ya hali ya baridi hupata hali ngumu kimwili katika mazingira ya hali ya joto kali. Hii ni kwa sababu mwili haujabadilika na kujihami dhidi ya mazingira hayo.

Mwili wa mwanadamu huwa na uwezo mkubwa na ustahimilivu wa ziada. Hata unapokuwa katika hali ngumu, hujibadilisha ili kuweza kukabiliana na hali hiyo na hatimaye kuishinda. Kwa hali ilivyo sasa, hata ukitazama utabiri wa hali ya hewa katika maeneo ya ukanda wa pwani na baadhi ya mikoa, kuna joto kali linalofikia nyuzi joto 33 na zaidi.

Hali hii inaweza kumwathiri mtu yeyote, iwe ni mchezaji anayecheza uwanjani au shabiki aliye uwanjani au katika mabanda ya kutazamia mpira.

Hali hiyo inaweza kuambatana na kupoteza maji mengi mwilini na kusababisha upungufu wa maji.

Endapo hakutakuwa na mbadala wa kukabiliana na hali hii, mtu yeyote anaweza kupatwa na athari za upungufu wa maji. Hii ni kutokana na kwamba mtu mwenye upungufu wa maji mwilini hupata athari za kimwili na kiakili.

Upungufu wa maji na chumvichumvi mwilini huathiri utendaji kazi wa ubongo. Hivyo, mchezaji anaweza kukosa umakini na kubabaika katika kufanya uamuzi. Joto linapokuwa kali huambatana na kupoteza maji na chumvichumvi mwilini kwa njia ya jasho na wakati wa kupumua. Hali hii huathiri moja kwa moja utendaji wa mwili mzima. Mwili unapopata upungufu wa maji, ubongo hushindwa kufanya kazi vizuri, ikiwamo kuratibu maamuzi na kazi nyingine za mwili, huku misuli nayo ikikakamaa na kukosa wepesi. Ndiyo maana wachezaji wanashauriwa kujihami kipindi hiki kwa kunywa maji mengi kabla, wakati na baada ya mechi.

ATHARI ZA UPUNGUFU WA MAJI

Yapo madhara yanayoweza kumpata mtu yeyote aliye katika mazingira ya joto, ikiwamo mchezaji au shabiki anayetazama mpira katika misongamano ya watu kwenye mabanda ya kuonyesha mpira. Upungufu wa maji mwilini ni jambo la kawaida kujitokeza kipindi hiki cha joto kali. Kwa kawaida, mwili huhitaji maji na chumvichumvi kwa ajili ya kazi mbalimbali, ikiwamo msukumo wa damu na kazi za seli mbalimbali. Wachezaji au mashabiki wanapokuwa katika mazingira ya joto huku wakifanya mazoezi, kucheza au kufanya mambo yanayoushughulisha mwili, hutokwa na jasho sana, hivyo kupoteza maji na chumvichumvi.

Kadiri joto linavyozidi kuwa kali, ndivyo mwili unavyotoa jasho zaidi. Lengo ni kupunguza joto la ndani ya mwili lisizidi kiwango chake cha kawaida, ambacho ni nyuzi joto 36.9. Matatizo mbalimbali ya kiafya yanaweza kujitokeza endapo mchezaji atapata upungufu mkali wa maji mwilini na chumvichumvi kutokana na kutokwa na jasho jingi. Hali hii inaweza kuambatana na madhara, ikiwamo maumivu na kubana kwa makundi ya misuli, ikiwamo misuli ya nyuma ya paja, ambayo ni muhimu kwa mchezaji wa soka. Upungufu wa maji usipokabiliwa unaweza kuleta madhara makubwa kiafya, ikiwamo kuumwa kichwa, kupoteza fahamu, kuchoka, kupata degedege au kiharusi.

Madhara mengine ni pamoja na uoni hafifu au kuona mawimbi, mwili kuwa dhaifu, kushindwa kutulia, kukosa umakini mazoezini au mchezoni, kuchanganyikiwa, kuumwa kichwa na mwili kuuma.

Tatizo hilo la upungufu wa maji kutokana na joto kali linaweza kumfanya mchezaji ashindwe kucheza kwa kiwango chake au acheze lakini achoke mapema.

Mara nyingi, wachezaji au watu wa kawaida wanaopata madhara haya kwa urahisi ni wale ambao hawanywi maji ya kutosha.


KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MAJI

Kanuni ya msingi ni kwamba kiasi cha maji kinachotoka nje ya mwili kwa njia ya jasho kirudishwe zaidi ndani ya mwili.

Angalau kwa siku  mchezaji mwenye uzito wa kilo 65 au zaidi anywe lita 2-3 au siku mbili kabla ya mechi kali anywe lita 3-5 kwa siku, na kwa mashabiki wao ni glasi 8-10 kwa siku.

Vilevile tumia zaidi matunda na mbogamboga mbichi kwa wingi kila baada ya mechi, kwani vyakula hivi huwa na maji na chumvichumvi kwa wingi.

Mchezaji anywe maji ya kutosha kabla ya kuingia mazoezini, katika mechi au katika majukumu ya siku. Vilevile, anywe maji kila baada ya nusu saa au wakati wa mapumziko na baada ya mechi au mazoezi. Epuka vinywaji vya kuongeza nguvu na kusisimua au kuchangamsha mwili, maarufu kama Energy drinks. Hivi si vinywaji sahihi kutumia kurejesha maji mwilini. Vilevile, usitumie pombe, soda na kahawa.

Kipindi hiki, wachezaji waepuke kukaa au kutembelea maeneo yenye joto na msongamano na badala yake wakae maeneo ya wazi yenye kivuli, hasa kabla ya mechi. Ni muhimu kipindi cha joto kali kuupumzisha mwili kwa kulala katika eneo tulivu lisilo na joto, lenye hewa ya kutosha, na kulala angalau saa nane kwa usiku mmoja. Kama joto litakuwa kali sana, ni vizuri mechi kuchezwa wakati joto au jua kali linapokuwa limepungua, badala ya kucheza mchana wakati joto ni kali zaidi.