Waamuzi wa ligi za Ulaya wanavyolipwa kibabe
Muktasari:
- Kutokana na hilo, ndiyo maana waamuzi wa ligi mbalimbali za Ulaya, hasa zile tano kubwa za EPL, Bundesliga, Ligue 1, La Liga na Serie A, zimekuwa zikilipa marefa wao mikwanja ya kibabe kabisa.
LONDON, ENGLAND: NANI hapendi kufanya kazi isiyolipa vizuri, hasa kazi yenyewe ikiwa ya lawama nyingi kama ya urefa wa soka.
Kutokana na hilo, ndiyo maana waamuzi wa ligi mbalimbali za Ulaya, hasa zile tano kubwa za EPL, Bundesliga, Ligue 1, La Liga na Serie A, zimekuwa zikilipa marefa wao mikwanja ya kibabe kabisa.
Marefa kwenye ligi hizo pamoja na wale wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, nao wanavuna mkwanja mrefu.
Makala haya yanahusu mishahara wanayolipwa waamuzi wanaopiga mzigo mrefu kwenye nchi za England, Hispania, Ujerumani, Ufaransa, Italia na Ureno.
Tofauti na ilivyo kwa wanasoka wa Ulaya, ambao mishahara yao wanalipwa kwa wiki – kwa upande wa waamuzi, huwa wanalipwa kwa mwezi na wengine kwa mwaka, lakini pia wakilipwa posho za kuchezesha mechi za ligi za ndani na zile za Ulaya.
Na wamekuwa walipwa ada ndogo kwa wale waamuzi wanapangiwa majukumu ya VAR.
Waamuzi wanalipwaje?
Si kazi nyingi sana ambao waajiriwa wake wanakumbana na maneno mengi ya kudhalilishwa kuzidi hii ya urefa. Ni kawaida kwa mwamuzi kukumbana na lugha chafu, anapochezesha mechi, hasa ya soka.
Hata hivyo, baadhi ya lugha chafu zaidi zinapoelekezwa kwa waamuzi, wahusika wake wamekuwa wakiwekwa kwenye hatia, ikiwamo kufungiwa au kupigwa faini.
Cheki mishahara ya waamuzi wa soka wanavyolipwa kwenye ligi za Ulaya na kufanya maisha yao kuwa poa.
LIGI KUU ENGLAND
Mwezi: Pauni 3,246
Mechi: Pauni 1,140
VAR: Pauni 878
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara wa mwaka kwenye Ligi Kuu England ni Pauni 96,634, huku wengine wakilipwa kiwango kikubwa zaidi ya hicho kutokana na hadhi yao. Na kwa mwaka mwamuzi muhimu zaidi anaweza kuchezesha mechi kati ya 27 au 28. Kwa kipindi cha hivi karibuni, waamuzi wa England wamekuwa kwenye mzozo mkubwa kutokana na kuchezesha mechi chini ya viwango. Kwa wastani, wamelipwa Pauni 1,140 kwa kila mechi na Pauni 3,246 kwa mwezi. Na kwa waamuzi wenye majukumu ya kuchezesha michuano kimataifa, hasa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wana wastani wa Pauni 6,147, hivyo kufanya wastani wa mshahara wa mwaka wa Pauni 96,634.
LA LIGA
Mwezi: Pauni 10,978
Mechi: Pauni 3,688
VAR: Pauni 1,844
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara wa mwamuzi wa La Liga kwa mwaka ni Pauni 219,619 – hiyo ikiwa ni wastani wa kwenye mechi 20. Mwaka 2020, waamuzi wa La Liga walifanywa kuwa profesheno, hivyo mishahara yao ilipanda na kulipwa kiwango kikubwa kuliko marefa wengine wa Ulaya. Wanalipwa zaidi mara tatu zaidi ya viwango vinavyolipwa kwenye Ligi Kuu England, Pauni 3,688 kwa mechi.
Hiyo ni sawa na Pauni 10,978 kwa mwezi na mshahara wa mwaka kwa mwamuzi wa La Liga ni Pauni 219,619. Si mshahara mdogo hakika. Mambo ni mazuri.
BUNDESLIGA
Mwezi: Pauni 2,194, Pauni 3,511 au Pauni 5,268
Mechi: Pauni 3,159
VAR: Pauni 965
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara wa waamuzi wa Bundesliga kwa mwaka ni Pauni 109,679 – na kinachoelezwa ni kwamba hakuna mwamuzi anayezidi mechi 20 kuchezesha.
Licha ya Ligi Kuu England kuwa na pesa nyingi, lakini mwamuzi wa Bundesliga analipwa vizuri kuliko waamuzi wa kwenye ligi hiyo inayotamba kwamba ni maarufu. Kila mechi, mwamuzi wa Ujerumani analipwa Pauni 3,159) – karibu mara tatu ya kiwango anacholipwa mwamuzi wa England kwa mechi. Kwenye Bundesliga kuna uwezekano wa mishahara mitatu kwa mwezi, ambapo kuna waamuzi wanalipwa Pauni 2,194, Pauni 3,511 au Pauni 5,268. Kwa mwaka, waamuzi hao wanaweza kulipwa Pauni 109,679.
LIGUE 1
Mwezi: Pauni 5,268
Mechi: Pauni 2,545
VAR: Pauni 790
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara kwa mwaka wanaolipwa waamuzi wa soka wa Ligue 1 ya Ufaransa ni Pauni 105,286 – huku mwamuzi anaweza kuwa na nafasi ya kuchezesha mechi 23 au 24. Hata waamuzi wa kwenye ligi ya Ufaransa, ambao kwa wale wa England wakiikejeli kuwa ni ligi ya wakulima, waamuzi wake wanalipwa mshahara mkubwa kuzidi wale wa Ligi Kuu England.
Kwenye Ligue 1, marefa wanalipwa Pauni 2,545 kwa kila mechi na Pauni 5,268 kwa mwezi. Hiyo ni sawa na Pauni 105,286 kwa kila mwaka, ikiwa ni mshahara wanaolipwa waamuzi wanaopiga mzigo kwenye Ligue 1.
SERIE A
Mwezi: Pauni 3,422 - 5,703
Mwezi: Pauni 2,985
VAR: Pauni 1,317
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara wa mwamuzi kwenye Serie A kwa mwaka ni Pauni 122,905 – huku wastani wa refa mahiri, mechi anazoweza kuchezesha ni kati ya 15 au 16.
Waamuzi wa soka huko Italia wamekuwa wakizingatiwa sana kuhusu mishahara yao, ambapo Pauni 2,985 kwa kila mechi. Kwa kipindi cha mwaka mmoja, mwamuzi wa soka kwenye mikikimikiki hiyo ya Serie A, ambapo mabingwa wao ni Napoli, waamuzi mishahara yao kwa mwaka inafikia Pauni 122,905.
PRIMEIRA LIGA
Mwezi: Pauni 658, Pauni 1,317 au Pauni 2,194)
Mechi: Pauni 1,317
VAR: Pauni 421
Ligi ya Mabingwa Ulaya: Pauni 6,147
Wastani wa mshahara wa mwaka anaolipwa mwamuzi wa soka wa Ureno ni Pauni 26,332 – huku waamuzi wake wakidaiwa kwamba si wa kulipwa rasmi, lakini wamekuwa wakipewa siku tatu za kujiandaa kwa ajili ya kujiandaa kwa mechi kila wiki.
Huko Ureno, waamuzi bado hawahesabiki kama ni wa kulipwa halisi, lakini bado wanalipwa Pauni 1,317 kwa kila mechi. Waamuzi kwenye Primeira Liga wanafanya kazi siku tatu kwa wiki na ndio maana mshahara wao kwa mwaka ni Pauni 26,332. Hata hivyo, kiwango hicho cha pesa wanazolipwa si kibaya, kwa sababu wamekuwa wakijishughulisha na kazi nyingine pia.