Viwanja vyaibeba Tanzania AFCON 2027
Muktasari:
- Badala ya kusubiri hadi miezi ya mwisho, Tanzania imetumia muda uliopo kukamilisha ujenzi, kufanya majaribio ya miundombinu na kushughulikia mahitaji ya kiufundi kabla ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19, 2026 hadi Julai 18, 2027.
IKIWA imesalia takribani miezi tisa kabla ya Tanzania kuungana na Kenya na Uganda kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, maandalizi hapa nchini yameingia katika hatua muhimu, huku miradi mikubwa ya viwanja, maeneo ya mazoezi na miundombinu saidizi ikiwa imekamilika au ikielekea kukamilika.
Badala ya kusubiri hadi miezi ya mwisho, Tanzania imetumia muda uliopo kukamilisha ujenzi, kufanya majaribio ya miundombinu na kushughulikia mahitaji ya kiufundi kabla ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19, 2026 hadi Julai 18, 2027.
Hatua hiyo imeongeza matumaini ya Tanzania kuwa mwenyeji bora wa michuano hiyo, baada ya ukaguzi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuonyesha kuwa Tanzania ilikuwa katika nafasi nzuri zaidi kimuundo ikilinganishwa na nchi nyingine mbili wenyeji, Kenya na Uganda.
Hata hivyo, baadhi ya viwanja bado vinahitaji maboresho ya kiufundi na kiutendaji kabla ya kutangazwa kuwa vimetimiza kikamilifu vigezo vya CAF.
Sasa changamoto kubwa ni kubadili maendeleo ya ujenzi yaliyofikiwa kuwa utayari kamili wa mashindano.
UWANJA MPYA ARUSHA
Katika maandalizi hayo, Uwanja mpya wa Arusha uliopo Olmoti ni miongoni mwa miradi mikubwa inayosubiriwa kwa hamu.
Uwanja huo uliopangwa kuwa na uwezo wa kuchukua takribani watazamaji 30,000, umefikia hatua za juu za ujenzi. Takwimu za Serikali zilizotolewa mapema mwaka huu zilionyesha kuwa ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 88, wakati uwanja maalumu wa mazoezi unaojengwa ndani ya eneo hilo ulikuwa umevuka asilimia 60.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, alisema uwanja huo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni, hatua ambayo itatoa muda wa kutosha kwa mamlaka kufanya majaribio na maandalizi ya mwisho kabla ya AFCON.
Mradi huo hauishii kwenye uwanja pekee. Barabara zinazoelekea eneo la uwanja zinaendelea kuboreshwa, huku miundombinu ya jirani ikiimarishwa kwa ajili ya kurahisisha usafiri wa mashabiki, timu na viongozi.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Boniface Tamba, alisema maandalizi ya Tanzania hayapaswi kuangaliwa kama maandalizi ya mashindano hayo pekee, bali kama uwekezaji wa muda mrefu katika michezo nchini. “Hatuandai tu kwa ajili ya mechi. Tunaandaa miundombinu ambayo itaendelea kuwa na matumizi katika michezo ya Tanzania hata baada ya AFCON 2027,” alisema Tamba.
Alisema maendeleo yaliyofikiwa yanaipa Serikali matumaini kuwa Tanzania itakuwa na miundombinu inayohitajika kabla ya mashindano kuanza.
Kwa mujibu wa Tamba, kukamilisha miradi mapema kutatoa nafasi ya kufanya majaribio, kupata vyeti vinavyohitajika na kushughulikia mapendekezo yoyote ya mwisho kutoka CAF.
“Viwanja vya mazoezi ni muhimu pia kwa sababu kila timu itakayokuja Tanzania itahitaji eneo zuri la kufanyia mazoezi. Ndiyo maana tunaboresha miundombinu Dar es Salaam na maeneo mengine ya wenyeji,”
BENJAMIN MKAPA
Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar es Salaam, unaendelea kuwa nguzo muhimu katika maandalizi ya Tanzania ya AFCON. Uwanja huo mkubwa zaidi wa mpira nchini umefanyiwa ukarabati mkubwa unaolenga kuufikisha karibu zaidi na viwango vinavyohitajika na CAF.
Takwimu za Serikali zilizotolewa awali ziliweka kiwango cha ukarabati wa jumla wa uwanja huo kufikia takribani asilimia 95.
Kwa sasa, kazi kubwa inayofanyika ni ukarabati wa eneo la kuchezea. Sehemu ya zamani ya nyasi na tabaka zake za chini imeondolewa ili kuweka mfumo mpya unaolenga kuboresha mfumo wa upitishaji maji na kuhakikisha uwanja unafikia viwango vya kimataifa.
Ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa ukarabati wa eneo la kuchezea ulikuwa umevuka asilimia 50 kufikia Agosti, jambo linaloashiria kuwa moja ya kazi muhimu zilizobaki katika uwanja huo inaendelea vizuri. CAF awali ilibainisha maeneo kadhaa yaliyohitaji maboresho, yakiwemo eneo la kuchezea, mfumo wa taa, umeme wa dharura, huduma za wageni maalumu, mfumo wa kuingia na kutoka kwa watazamaji pamoja na usalama.
UWANJA WA FUMBA
Zanzibar nayo imepiga hatua kubwa katika maandalizi yake, yakiongozwa na ujenzi wa Uwanja wa Fumba, ambao ni sehemu ya mradi mpana wa michezo na utalii wa Fumba.
Uwanja huo unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua takribani watazamaji 36,500 na ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya miundombinu ya michezo kuwahi kutekelezwa Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kutumia takribani dola milioni 150, sawa na Sh389.2 bilioni, katika awamu ya kwanza ya Mradi wa Zanzibar AFCON Sports Complex. Mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2026, hatua itakayoacha miezi kadhaa kwa ajili ya majaribio na maandalizi ya kiutendaji.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dk Riziki Pembe Juma, alisema maandalizi ya Zanzibar yamefikia asilimia 81, huku kazi kubwa zikitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026.
Alisema kwa sasa mkazo mkubwa umewekwa kwenye Uwanja wa Fumba, ambapo wakandarasi wanafunga paa, hususan katika eneo la VVIP.
NEW AMAAN MUHIMU
Uwanja wa New Amaan Complex nao unaendelea kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Zanzibar.
Uwanja huo uliopo tayari unafanyiwa maboresho, hasa eneo la kuchezea, huku mamlaka zikijadili nafasi yake ya muda mrefu katika mpango wa viwanja vitakavyotumika kwenye AFCON. CAF imeitaka Zanzibar kutoa uamuzi rasmi kuhusu iwapo New Amaan utaendelea kutumika kama uwanja wa mashindano au utatengwa kwa ajili ya mazoezi.
Iwapo utaendelea kuwa uwanja wa mashindano, maboresho zaidi ya usanifu na mifumo ya uendeshaji yatahitajika ili kufikia viwango vinavyotakiwa.
Hata hivyo, bila kujali uamuzi wa mwisho kuhusu matumizi yake wakati wa AFCON 2027, New Amaan inatarajiwa kubaki na umuhimu mkubwa katika programu za mazoezi na maendeleo ya soka Zanzibar hata baada ya mashindano hayo.