Vitu saba vya kuepuka kwenye mtoko wa Wikiendi
Muktasari:
- Rangi hazielewani, viatu vina vita na nguo, halafu bado anajiamini kabisa. Fashion siyo kuvaa kila kilichopo kabatini, ni kujua nini kinafaa kwa sehemu unayokwenda.
Jamani, kuna watu ukikutana nao wikiendi unaweza ukaapa wamevaa nguo zote walizonunua mwaka mzima kwa siku moja.
Rangi hazielewani, viatu vina vita na nguo, halafu bado anajiamini kabisa. Fashion siyo kuvaa kila kilichopo kabatini, ni kujua nini kinafaa kwa sehemu unayokwenda.
Unaweza kuwa na nguo za bei ghali, lakini ukizichanganya vibaya ukapoteza kabisa mvuto. Kama unapanga kutoka wikiendi hii, kuna baadhi ya mavazi ni bora uyaache kabatini kuliko yakuharibie muonekano wako.
Wikiendi ni muda wa kupumzika, kukutana na marafiki, kwenda dinner, beach, shopping au matembezi. Kila sehemu ina mtindo wake wa mavazi, hivyo uchaguzi wa nguo una mchango mkubwa katika muonekano wako.
1. NGUO ZILIZOKUNJAMANA
Hata kama umevaa nguo ya gharama kubwa, ikiwa imejaa mikunjo itaonekana kama umeitoa moja kwa moja kwenye kikapu cha kufulia.
Dakika chache za kupiga pasi zinaweza kubadilisha kabisa muonekano wako. Nguo iliyonyooka huonyesha nadhifu na huongeza kujiamini unapokuwa mbele za watu.
2. NGUO ZINAZOKUBANA KUPITA KIASI
Wengine huamini kadiri nguo zinavyobana ndivyo zinavyopendeza. Ukweli ni kwamba nguo zinazokubana kupita kiasi hukufanya ushindwe kutembea au kukaa kwa uhuru.
Mbali na kupunguza urembo, zinaweza pia kufanya uonekane huna uhakika wa ukubwa unaokufaa. Chagua nguo zinazokaa vizuri mwilini bila kukubana.
3. NGUO ZILIZOCHANIKA
Mitindo ya nguo zilizochanika bado ipo, lakini kuna tofauti kati ya fashion na nguo zinazofanana na zilizopitia ajali.
Jeans yenye michaniko michache inaweza kupendeza, lakini ikiwa karibu kila sehemu imechanika, muonekano unaweza kupoteza mvuto, hasa ukienda sehemu zinazohitaji mwonekano wa heshima.
4. VIATU VICHAFU AU VILIVYOCHAKAA
Unaweza ukachagua outfit nzuri sana, lakini viatu vibovu vikaharibu kila kitu.
Viatu ndivyo watu wengi huvitazama bila wewe kujua. Hakikisha ni visafi, havijachanika na vinaendana na aina ya mtoko wako. Sneakers safi au loafers nadhifu vinaweza kubadilisha kabisa muonekano wako.
5. MAVAZI YENYE MAANDISHI AU PICHA ZINAZOKERA
Baadhi ya T-shirt huwa na maandishi au michoro ambayo wakati mwingine huleta tafsiri mbaya au zisizofaa.
Kabla hujavaa, angalia ujumbe uliopo kwenye nguo yako. Ni vizuri kuhakikisha hauwezi kumkwaza mtu au kukuweka kwenye hali ya aibu bila sababu.
6. ACCESSORIES NYINGI KWA WAKATI MMOJA
Mkufu mkubwa, hereni kubwa, saa kubwa, miwani kubwa na bangili nyingi kwa wakati mmoja vinaweza kufanya outfit ionekane imeelemewa.
Fashion nzuri mara nyingi hutegemea uwiano. Chagua accessories chache zinazokamilisha muonekano badala ya kushindana zenyewe.
7. NGUO ZISIZOLINGANA NA SEHEMU UNAYOKWENDA
Hili ndilo kosa linalofanywa na watu wengi. Unaweza kuvaa vizuri, lakini ukawa umevaa nguo zisizofaa kwa tukio.
Kwa mfano, outfit inayofaa beach inaweza isiwe sahihi kwa dinner ya kifahari. Vivyo hivyo, mavazi ya gym siyo chaguo bora kwa matembezi ya kawaida mjini. Kabla ya kutoka, jiulize unaenda wapi na mazingira yanahitaji muonekano gani.
SIRI NI HII
Watu wengi hudhani lazima uwe na nguo nyingi ili uonekane stylish. Ukweli ni kwamba unaweza kuwa na mavazi machache lakini ukajua kuyapangilia vizuri.
Nguo safi, zinazotosha mwili wako, viatu vinavyong’aa na accessories chache vinatosha kukupa muonekano wa kuvutia kuliko kabati lililojaa nguo ambazo hazipatani.
KUJIAMINI HUKAMILISHA KILA KITU
Baada ya kuchagua mavazi sahihi, usisahau jambo muhimu zaidi, kujiamini.
Tembea kwa utulivu, tabasamu na vaa kile kinachokufanya ujisikie vizuri. Fashion siyo mashindano ya kuvaa nguo ghali, bali ni uwezo wa kuonyesha haiba yako kupitia mavazi.
USHAURI
Wikiendi ni muda wa kufurahia maisha, si wa kujutia uchaguzi wa mavazi. Kabla hujatoka nyumbani, jipatie dakika chache za kujiangalia kwenye kioo.
Jiulize kama nguo ulizochagua zinaendana na sehemu unayokwenda, kama ni safi na kama zinakufanya ujisikie vizuri.
Ukizingatia mambo hayo machache, utaonekana nadhifu, wa kisasa na mwenye mvuto bila kulazimika kutumia fedha nyingi.