Out na mpenzi, vaa hivi wikendi hii
Muktasari:
- Sasa kama una mpango wa kutoka na mtu unayempenda wikiendi hii, usikimbilie kuvaa kila kitu kizuri ulicho nacho kwa wakati mmoja. Mavazi yanahitaji kuendana na sehemu unayokwenda, muda wa kutoka na muhimu zaidi hali ya hewa. Hapa ndipo unaweza kuonekana nadhifu bila kuonekana kama umepania kupita kiasi.
WIKIENDI ikifika, kuna watu wanabadilika ghafla kana kwamba wamepata mwaliko wa kwenda Ikulu. Simu inashikwa mara kwa mara, kioo kinakuwa rafiki mkubwa na nguo zote zilizopo kabatini zinaanza kufanyiwa usaili. Sababu ni moja tu, kuna mtu amewaita out na huyo mtu si wa kawaida, ni yule ambaye akikuambia “leo unatoka?” moyo nao unaanza kwenda speed kuliko kawaida.
Sasa kama una mpango wa kutoka na mtu unayempenda wikiendi hii, usikimbilie kuvaa kila kitu kizuri ulicho nacho kwa wakati mmoja. Mavazi yanahitaji kuendana na sehemu unayokwenda, muda wa kutoka na muhimu zaidi hali ya hewa. Hapa ndipo unaweza kuonekana nadhifu bila kuonekana kama umepania kupita kiasi.
KAMA NI JUA, MWANGA NA MATEMBEZI
Kama outing yako ni mchana na hali ya hewa ikiwa ya joto, nguo nyepesi ndiyo jibu. Wanawake wanaweza kuchagua gauni la kitambaa chepesi, sketi na blauzi au suruali pana iliyochanganywa na shati au blauzi yenye mwonekano wa kuvutia.
Kwa mwanaume, suruali ya kitambaa nyepesi na shati safi lenye mikono mifupi inaweza kufanya kazi vizuri. T-shirt nzuri yenye suruali ya jeans nyepesi nayo inaweza kuwa chaguo rahisi, hasa kama sehemu mnayokwenda inawatu wengi.
Usisahau viatu. Hapa si wakati wa kuvaa viatu ambavyo vitakufanya uanze kulalamika miguu kabla hata chakula hakijafika, usivae viatu virefu binti wakati umetumia boda boda kama usafiri wa kukutana na huyo mhalifu mwenzio.
GAUNI LINAPOINGIA, KAZI IMEISHA
Kwa mwanamke anayekwenda dinner au sehemu yenye utulivu zaidi, gauni zuri linaweza kufanya kazi kubwa bila kuhitaji mapambo mengi. Chagua gauni linalokaa vizuri mwilini na linalokupa uhuru wa kutembea na kukaa.
Kama hali ya hewa ni ya joto, epuka mavazi mazito yatakayokufanya utoke jasho kuliko hata chakula kilichopo mezani. Gauni la wastani lenye kitambaa kinachopitisha hewa linaweza kuwa chaguo zuri.
Kwa mwanaume, shati safi, suruali inayokaa vizuri na viatu safi vinaweza kutosha. Si lazima uvae suti ili kumshawishi mtu anayekupenda; wakati mwingine usafi, mpangilio na kujiamini vinatosha.
JIONI IKIPOA
Hali ya hewa ikianza kuwa ya baridi wakati wa jioni, usifanye kosa la kutoka ukiwa umejipanga kwa joto la mchana pekee. Mwanamke anaweza kuvaa gauni au suruali pamoja na koti jepesi au sweta nyembamba.
Mwanaume anaweza kuvaa shati pamoja na koti jepesi au sweta, kulingana na sehemu anayokwenda. Hii pia inatoa nafasi ya kuongeza chaguo la nguo bila kuharibu muonekano.
Kama unajua mnatoka jioni na mnaweza kurudi usiku, ni vizuri kuwa na nguo inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya joto, lakini pia zingatia na eneo unaloenda kama linautulivu vaa koti kama changanyikeni linaweza kukusumbua.
JEANS KOKOTE TU
Kuna siku hujui kabisa uvae nini, hapo jeans inaweza kuwa rafiki yako. Kwa mwanamke, jeans nzuri inaweza kuvaliwa na top, shati au blauzi pamoja na viatu vya kisigino kifupi, sandals au sneakers.
Mwanaume anaweza kuichanganya jeans na shati au T-shirt safi pamoja na sneakers. Hii ni aina ya mavazi inayoweza kukufaa kwa outing isiyo rasmi kama kwenda kula, kutembea au kukaa sehemu ya burudani.
Lakini hakikisha jeans hiyo iwe inakutosha vizuri. Usivae inayokufanya ushindwe kukaa kwa sababu ya kubana kupita kiasi.
KAMA MVUA INATISHIA
Wikiendi yenye dalili za mvua inahitaji mipango. Mwanamke anaweza kuchagua suruali badala ya gauni refu linaloweza kulowana chini, huku koti jepesi likiwa karibu.
Mwanaume naye anaweza kuwa na koti la mvua au koti jepesi ambalo halimsumbui akikutana na mvua ya ghafla. Viatu pia viangalie, si kila kiatu kizuri kinapenda maji.
USIJIPAKE KILA KITU
Mavazi mazuri hayamaanishi uwe na mwonekano wenye vitu vingi vilivyopitiliza. Ukiamua kuvaa nguo yenye rangi kali, punguza mapambo au vitu vingine ili muonekano wako usiwashangaze watu huko unakokwenda.
Mwanamke anaweza kutumia mkoba mdogo sio pochi kubwa kama unaenda kupanda SGR, hereni au mkufu mmoja unaoendana na mavazi.Kama nguo yako unaonyesha sana shingo basi cheni yako iwe ndogo nzuri na kama nguo yako inaziba shingo vaa hereni ndefu kidogo zisizo na mambo mengi.
Mwanaume anaweza kuongeza saa, mkanda mzuri au viatu vinavyokamilisha muoneekano wake ili mambo yasiwe mengi.
HARUFU NAYO NI MAVAZI
Unaweza kuvaa vizuri, lakini ukasahau manukato. Hapo umeacha nusu ya kazi. Chagua manukato yenye harufu nzuri lakini usimwage chupa nzima mwilini kana kwamba unaenda kuua mbu.
Harufu nzuri inapaswa kuwa ya kuvutia, si kumfanya mtu anayekaa meza ya jirani aanze kugeuka kutafuta chanzo au ikaanza kupalia wengine kifuani.
MWISHO, VAA UNACHOKIAMINI
Unapenda kukutana na mtu hasa umpendaye maeneo ya watu kama mgahawa, hotelini au sehemu za starehe muonekano wako tu unaweza kutyoa tafsiri ni mtu wa aina gani na anajielewa au bomu.
Lakini kama mmoja wenu atapania sana kuliko mwenzake akavaa nguo zenye mambo mengi pia inapoteza muunganiko ambao ungewafanya muonekane kama mnaupendo na mko pamoja, zaidi mtakuwa kama mfanyakazi na bosi wake.
Usisahau muonekano wa mwenzi wako unaweza ukakuharibia siku kama tu mmoja wenu atakosea hasa linapokuja swala la mavazi, kwani unaweza kuhisi kama umeaibika hivi au watu wanawaangalia nyie tu kwa namna mlivyopuyanga kama wanyasa.
Kama unaona kabisa humwelewi mpenzi wako kwenye swala la muonekano sio kosa kumwambia akutumie picha ya kile atakachovaa au mpange kabisa mapema ili msije mkashtuana kama watu msiofahamiana au mliokutana ghafla.
USIJEKUSEMA SIKUKWAMBIA.