Prime
Vigogo hawa watatoboa Kimataifa
TIMU za Simba, Yanga kuanzia Agosti 18 zitaanza mtihani mpya wa kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam na Singida zikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Hii ni michuano mikubwa Afrika ndiyo huwa inaonyesha ni nani mwamba kwenye bara hili, kwa timu tatu za Simba, Yanga, Azam huku wao sio wageni.
Lakini kwa Singida itakuwa mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo na watatakiwa kutumia muda wao wa sasa kujifunza kwa wakongwe.
Hata hivyo, pamoja na michuano hiyo kubakiza wastani wa miezi miwili tu kabla ya kuanza, ni dhahiri kuwa bado timu zote zinaonekana kulala na hakuna inayoonyesha kuwa imeanza maandalizi rasmi kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa.
Julai 1, ndio tarehe rasmi ambayo vita ya usajili itaanza kwa hapa nchini na mashabiki wa soka wanasubiri kuona timu zao zitafanya usajili gani kuelekea kwenye michuano hiyo pamoja na Ligi Kuu.
Mashabiki wanazitazama timu hizo kwenye usajili wakifikiri zaidi kuhusu michuano ya Afrika na sio Ligi Kuu Bara kama ambavyo ilikuwa miaka kadhaa hapo nyuma.
Wanaamini kuwa majembe yanayotakiwa kusajiliwa hapa ni yale ambayo yanaweza kuwatikisa wakongwe kwenye soka la Afrika kama Mamelodi Sundowns, Al Ahly, Esperance, Wydad Casablaca na wengine wengi.
Hakuna anayefikiri kuhusu ubingwa wa ASFC kwenye usajili huu kwa kuwa wameshaamini kuwa huu unaweza kupatikana kwa timu iliyo makini, je kwa hali ilivyo vigogo hivyo vitatoboa au havitoboi? Endelea nayo...!
SIMBA
Tayari Simba wameshaacha wachezaji wanne hadi jana jioni, lakini wanaonekana kuwa wanaweza kuwaacha wengine wengi kutokana na mafanikio waliyopata msimu uliopita.
Mastaa hao wote ni wa kigeni ambao ni Victor Akpan, Nelson Okwa, Agustine Okrah na Mohamed Ouattara picha hii inaonyesha kuwa Simba wana nafasi nne za kimataifa za kujaza.
Inaelezwa kuwa tayari imeshamsajiliwa Willy Esomba Onana raia wa Cameroon ambaye anacheza kwenye eneo la kiungo na beki wa kati.
Huyu anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wenye uzoefu na kiwango chake kinaweza kupunguza tatizo la kiungo kwenye kikosi cha Simba, Onana ambaye anatokea Rayon Sports ya Rwanda inaelezwa kuwa ni chaguo la kocha wa timu hiyo, Olivier Robert Robertinho.
Hata hivyo, tayari Simba wameshaonekana kurudia makosa baada ya kudaiwa kuwa wameshindwana na mmoja kati ya viungo wao mahiri aliyefanya vizuri msimu uliopita Saidio Kanoute.
Kumpoteza huyu, kutawafanya Simba kurudi nyuma na kutafuta mtu mwingine ambaye atacheza pamoja na Mzamiru Hassan, lakini itabidi apewe muda kuzoea mazingira.
Pamoja na huyo, Simba wanaonekana kuendelea kuwa na magepu mengi ya kuziba, kwenye eneo la beki wa kati ambapo msimu uliopita michezo mikubwa walionekana kutumia Joash Onyango na Inonga Baka pekee, hivyo wanaweza kusajili mchezaji mwingine mwenye kiwango bora.
Pamoja na Moses Phiri na Pape Sakho kuonekana kuwa kwenye kiwango, kocha wao hukuwahitaji kwenye timu yake, hivyo ni vyema msimu ujao akasajili wale ambao anaona wanaweza kucheza nafasi za winga wa kushoto na kulia kama hatawatumia hawa.
Eneo la ushambuliaji, Simba wanaweza kuongeza mshambuliaji mmoja na kuhakikisha Jean Baleke anabaki, hawana shida kubwa hapa kwa kuwa msimu uliopita walikuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga.
Langoni wanatakiwa kusajili kipa mmoja kutoka nje ya nchi mwenye uzoefu na daraja la juu levo ya Aishi Manula au zaidi, kwa kuwa kipa wao huyo namba moja hawezi kutumika kwenye michezo ya mwanzoni na nje hawana kipa mwenye uwezo.
Ukiachana na Robertinho na Juma Mgunda kwenye eneo la makocha wanatakiwa kuongeza wengine bora kwenye benchi tena mapema kabla ya Juni 10 ili kuwa na benchi bora.
YANGA
Mtihani mkubwa walionao Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni mafanikio ya msimu uliopita.
Yanga walifanikiwa kumaliza msimu kwa kutwaa makombe yote ya ndani pia wakafika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuondolewa mapema Ligi ya Mabingwa.
Mashabiki wanasubiri kuona mafanikio makubwa zaidi kwa Yanga msimu ujao na wengi wanaamini kama watashuka shirikisho wanatakiwa kutwaa ubingwa, lakini wakiwa Ligi ya Mabingwa wafike nusu fainali.
Pigo kubwa kwa Yanga hadi sasa hawana kocha mkuu, inawezekana na wasaidizi wote ikiwa imebaki miezi miwili michuano ya Afrika ianze.
Kuna wasiwasi kuwa kocha atakayekuja atakuta ameshafanyiwa usajili kama ambavyo iliwahi kufanyika miaka kadhaa nyuma na Yanga kufeli.
Inavyoonekana kwa sasa Yanga wanalazimika kutangaza benchi lao la ufundi kabla ya Julai 1 ili makocha wafanye usajili wenyewe.
Yanga pamoja na mafanikio yao hawapo salama wakiwa wameshaachana na Bernad Morrison ambaye hakutumika kwa kiwango kikubwa msimu uliopita, ikiwa ni nafasi moja ya kimataifa kwao, lakini bado wanaonekana wanaweza kuachana na Mamadou Douambia ambaye alisajiliwa mwishoni lakini akashindwa kuwika.
Hii itakuwa nafasi ya pili kwa Yanga ya kimataifa, kama hawatauza, Yanga watatakiwa kuhakikisha waongeza beki mmoja wa pembeni upande wa Djuma Shaaban ambaye alionekana kushuka kiwango kwenye michezo ya mwishoni.
Nafasi ya kiungo mkabaji ambayo pia anacheza Yannick Bangala inatakiwa kuwa na mchezaji mwingine imara tena kutoka nje ili kuwasaidia mabeki kucheza kwa utulivu bila kubadilishwa badilishwa.
Endapo Fiston Mayele ambaye msimu uliopita alifunga zaidi ya mabao kumi kwenye michezo ya kimataifa atabaki kwenye timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, Yanga wanaonekana kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji, lakini watakikiwa kuongeza kiungo mwingine mahiri msaidizi wa Aziz Ki ambaye kiwango chake kimeonekana kupanda na kushuka kila siku.
AZAM FC
Kila msimu Azam wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa pamoja na kuonekana kuwa wana kila kitu bora.
Timu hiyo msimu uliopita ilitupwa nje hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho na kila msimu malalamiko yamekuwa ni kuwa hawana uzoefu jambo ambalo linaonekana siyo kweli.
Msimu huu Azam watashiriki tena michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kumaliza kwenye nne bora msimu uliopita, nayo ni timu ambayo inahitaji maboreshe sehemu muhimu.
Azam wanaonekana kuwa na makipa bora, kiwango cha mabao waliyofungwa msimu uliopita kwenye Ligi Kuu kinaonyesha kuwa wanatakiwa kuboresha safu yao ya ulinzi na haswa mabeki wa kati, lakini pamoja na kufunga mabao 55 kwenye ligi msimu huo bado hawapo salama sana.
Inaonekana safu ya ushambuliaji ya timu hii inatakiwa kuongeza mshambuliaji mwingine mwenye uzoefu ambaye atasaidiana na Prince Dube na Abdul Suleymani Sopu ambao wamefanya vizuri misimu miwili mfululizo.
Hata hivyo, baada ya kusafisha benchi la ufundi na kubaki na kocha mkuu pekee, Azam wanalazimika kuleta makocha wapya mapema ili kuziba mapengo yaliyopo kabla ya maandalizi ya msimu mwezi ujao, lakini kuleta watu wa kumsaidia kiungo wao mpya, Feisal Salum Fei Toto.
SINGIDA FOUNTAIN GATE
Hakuna anayewadai Singida kwa msimu huu wa kwanza kwenye michuano ya kimataifa kutokana na uchanga wao.
Ilionekana kuwa kati ya timu bora kwenye ligi msimu uliopita wakiwa na kocha mzoefu Hans van Pluijm ambaye anaonekana kuwa ataendelea kuwa nao msimu ujao.
Timu hii ilifanya vizuri na kuingia kwenye nne bora ya timu zilizofunga mabao mengi kwenye ligi baada ya kutupita mara 35.
Imekuwa ikimtegemea Mbrazili Bruno Gomes ambaye amefanya kazi kubwa kwa kufunga mabao kumi na kuingia kwenye kikosi bora cha msimu.
Anaonekana akisaidiana na mastaa wengine kama Nicholaus Gyan anaweza kuisaidia timu hiyo kuvuka hatua ya kwanza kwenye michuano hiyo.
Kama kipa wao aliyepo Yanga kwa mkopo Metacha Mnata atarejea na kusaidiana na Benedict Haule eneo hili litakuwa halina shida, lakini kama hatarejea basi ni vyema wakakamilisha usajili wa Beno Kakolanya anayeelezwa kuwa anakwenda kwenye timu hiyo.
Kwenye eneo la kiungo wanaweza kumuongeza Bernad Morrison ambaye ana uzoefu wa kutosha na anaonekana anaweza kuwasaidia kwa mwaka huu wa kwanza, akisaidiana na wakongwe, Pascal Wawa, Meddie Kagere na wengine, wanaweza kushangaza wakijipanga vizuri.