VAN DAMME; Mkali wa mapigano anayeendelea kuvuna
Muktasari:
- Iwapo dili hilo litakamilika, Van Damme ataendelea kuongeza utajiri kama mmoja wa mastaa wakongwe waliotengeneza pesa nyingi kutokana na filamu za mapigano.
LOS ANGELES, MAREKANI: MWISHONI mwa wiki iliyopita, jina la Jean-Claude Van Damme lilitikisa tena kwenye vyombo vya habari baada ya taarifa kuibuka staa huyo wa zamani wa filamu za mapigano anatajwa kupewa dili jipya la kushiriki filamu.
Inaelezwa kampuni kubwa za filamu kutoka Marekani na Ulaya zinapanga kumrudisha gwiji huyo katika ulingo wa filamu za mapigano, kitu ambacho mashabiki wake wamekuwa wakikisubiri kwa muda mrefu.
Iwapo dili hilo litakamilika, Van Damme ataendelea kuongeza utajiri kama mmoja wa mastaa wakongwe waliotengeneza pesa nyingi kutokana na filamu za mapigano.
Hapa tumekusogezea ATM yake kufahamu utajiri ambao yupo nao kwa sasa, mali anazomiliki na namna anavyopiga pesa licha ya kutoonekana katika muvi yoyote kwa muda mrefu.
ANAPIGAJE PESA
Jamaa ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 40 milioni. Kwa kiasi kikubwa utajiri wake unatokana na malipo ya maigizo yake ya muvi.
Katika ubora wake, Van Damme alikuwa akilipwa kati ya Dola 5 milioni hadi Dola 10 milioni kwa filamu moja na alipata mpunga mwingi kutokana na muvi zake kama Bloodsport, Kickboxer, Universal Soldier na Timecop na kwa jumla alikunja takribani Dola 40 milioni.
Kijumla filamu zake zote alizoigiza zinakadiriwa kuingiza takribani Dola 1 bilioni kutokana na mauzo.
Kwa sasa katika vipindi vya TV na mikataba ya udhamini ya kampuni kama Volvo Truc, Aqua-VD na 777.be ambayo yupo nayo, anaingiza takribani Dola 5 milioni kwa mwaka.
MIJENGO
Van Damme anamiliki nyumba ya kifahari jijini Los Angeles, Marekani, yenye thamani ya takribani Dola 7 milioni 7 ambayo ndani yake kuna Gym kubwa ya mazoezi, Bwawa la kuogelea, Ukumbi wa sinema binafsi
na Bustani ya kisasa.
Pia ana nyumba nyingine nchini kwao Ubelgiji, ambayo huitumia zaidi kwa ajili ya mapumziko. Mjengo huo una thamani ya Dola 3 milioni.
NDINGA
Ferrari 360 Modena – Dola 150,000
Lamborghini Gallardo – Dola 200,000
Bentley Continental GT – Dola 220,000
Mercedes-Benz SL-Class – Dola 120,000
Rolls Royce Gost-Dola - Dola 440,750
Maserati-Dola 200,000
MSAADA KWA JAMII
Kutokana na shughuli zake binafsi, Van Damme amekuwa akitoa sana misaada kwa jamii kwa kutumia taasisi yake ya Van Dam Charitable Foundation ambayo.
Mara kadhaa pia amewahi kushirikiana na taasisi ya Kevin VanDam Foundation katika kusaidia vituo vya watoto yatima, Kampeni za kupinga matumizi ya dawa za kulevya na kuhamasisha vijana kufanya mazoezi na kuishi maisha yenye nidhamu na kwa mwaka hutumia hadi Dola 100,000 kutoa misaada.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
Van Damme kwa sasa yupo katika ndoa na mtunisha misuli wa zamani Gladys Portugues ambaye alimuoa mara ya pili mwaka 1999 baada ya hapo awali kumuoa mwaka 1987 na kuachana naye mwaka 1992.
Wakiwa pamoja, wamepata watoto wawili ambao ni Kristopher na Bianca.
Katika maisha yake fundi huyu amewahi kuoa wanawake watano tofauti.
Licha ya changamoto mbalimbali alizowahi kukutana nazo katika maisha yake ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya zamani, Van Dame alirejea katika mstari sahihi na sasa amekuwa akishiriki sana kampeni za kusaidia na kutoa elimu ya kujiondoa katika matumizi hayo. Kwa sasa, muda mwingi anautumia kufanya mazoezi.