Kroenke: Tajiri kijana anayeipambania Arsenal
Muktasari:
- Kwa sasa Josh ndiye anaonekana kuwa injini ya Arsenal baada ya kupewa majukumu hayo na baba yake, Stan Kroenke, ambaye ndiye mmiliki wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.
DENVER, MAREKANI: MWISHONI mwa wiki iliyopita jina la Josh Kroenke lilikuwa gumzo miongoni mwa mashabiki wa michezo baada ya kuripotiwa kuwasili London kwa ajili ya kuweka kikao na kocha Mikel Arteta kuhusu maendeleo ya Arsenal na mipango ya msimu ujao.
Kwa sasa Josh ndiye anaonekana kuwa injini ya Arsenal baada ya kupewa majukumu hayo na baba yake, Stan Kroenke, ambaye ndiye mmiliki wa klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.
Hata hivyo, mbali ya kiwango kinachoonyeshwa na Arsenal ambayo ipo karibu kuchukua ubingwa leo tumekusogezea utajiri ambao Josh anamiliki kupitia hisa na miradi mbalimbali ambayo amekuwa akiisimamia.
ANAPIGAJE PESA
Utajiri wa Josh Kroenke unakadiriwa kufikia zaidi ya Dola 500 milioni ukiwa ni sehemu ndogo ya ukwasi ambao familia ya Kroenke inamiliki.
Josh amekuwa akipata kiasi kikubwa cha pesa kupitia kampuni ya Kroenke Sports & Entertainment ambayo yeye ndiye kiongozi mkuu.
Kampuni hiyo ndiyo inamiliki timu kama Arsenal, Denver Nuggets (Marekani), Los Angeles Rams (Marekani) na Colorado Avalanche (Marekani).
Faida ya kampuni hiyo huwa ni mapato ambayo klabu zinaingiza kupitia mikataba ya matangazo, haki za televisheni na biashara ya vifaa vya michezo.
Mbali ya kupiga pesa kupitia mapato ya timu Josh pia anaongoza kampuni nyingine kadhaa alizopewa jukumu na baba yake.
Kampuni hizo zinamiliki viwanja vya michezo, majengo ya biashara na majumba ya kifahari ambayo wamekuwa wakiyapangisha.
Kampuni ya viwanja inamiliki moja kati ya viwanja vikubwa vya michezo duniani kama SoFi Stadium ambacho kimejengwa kwa takribani Dola 6 bilioni.
Kampuni hizo kwa pamoja zinadaiwa kuingiza mapato ya takribani Dola 20 bilioni kwa mwaka.
MIJENGO YAKE
Josh Kroenke anaishi maisha ya kifahari huko Marekani na anamiliki mijengo Denver na Los Angeles ambayo ina thamani ya takribani Dola 30 milioni kwa ujumla.
Nyumba hizo ndani yake kuna maeneo makubwa ya mapumziko, gym za kisasa, bustani na sehemu za burudani.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
Josh Kroenke ni mtu anayependa kuweka maisha yake binafsi mbali na vyombo vya habari. Kutokana na utajiri wake pia imekuwa ngumu hata kumwona katika sehemu za starehe mara nyingi huonekana anapokuwa uwanjani kutazama mechi ya Arsenal na timu nyingine ambazo wanazimiliki huko Marekani.
Licha ya usiri huo taarifa kutoka vyanzo kadhaa zimedai kwamba tajiri huyo ameoa na ana watoto ingawa haikuelezwa ni wangapi.
MSAADA KWA JAMII
Kupitia taasisi na klabu zao familia ya Kroenke kwa ujumla hutoa misaada mbalimbali kwa jamii ikiwa pamoja na misaada ya elimu kwa vijana, miradi ya maendeleo ya michezo na misaada wakati wa majanga ya mlipuko kama ilivyokuwa kwenye Corona.
Kupitia timu kama Denver Nuggets na Arsenal FC wamekuwa wakifanya kampeni za kijamii kusaidia vijana na familia zenye kipato cha chini.