Salah; Tajiri anayewaliza Liverpool kimyakimya
Muktasari:
- Mchezaji huyo ambaye ni miongoni mwa mastaa walioitumikia Liverpool kwa takriban miaka tisa akiipa mafanikio makubwa ya ndani na nje ya uwanja, anaondoka katika timu hiyo akiwa na utajiri wa kutosha.
LIVERPOOL, ENGLAND: WIKI iliyopita ilikuwa ya maumivu makubwa kwa mashabiki wa Liverpool baada ya supasta wa kikosi hicho, Mohamed Salah kutangaza kuwa ataondoka ifikapo mwisho wa msimu.
Mchezaji huyo ambaye ni miongoni mwa mastaa walioitumikia Liverpool kwa takriban miaka tisa akiipa mafanikio makubwa ya ndani na nje ya uwanja, anaondoka katika timu hiyo akiwa na utajiri wa kutosha.
Utajiri huo unatokana na pesa alizovuna akiwa na kikosi hicho kama mshahara na bonasi na pia mkwanja alioupata kutokana na dili nyinginezo nje ya uwanja. Leo unasogezewa ATM yake kuonyesha jinsi anavyopata pesa na mali anazomiliki.
ANAPIGAJE PESA
Salah analipwa takribani 400,000 kwa wiki kama mshahara akiwa na Liverpool, pia huwa kuna bonasi kila anapofunga bao au kutoa asisti. Kwa ujumla pamoja na bonasi fundi huyu hupata hadi Pauni 20 milioni kwa mwaka kabla ya kodi lakini baada ya makato hupata Pauni 10 milioni.
Mbali ya mshahara, pia anapata pesa za kutosha kupitia ubalozi wake wa kampuni mbalimbali ikiwa pamoja na Adidas, Pepsi, Vodafone na Uber ambazo kwa ujumla zinadaiwa kumpa takribani Dola 5 milioni kwa mwaka.
Katika mitandao ya kijamii, jamaa pia hupata mkwanja wa kutosha kwani kpitia ukurasa wake wa Instagram ambao kwa sasa una wafuasi milioni 60, posti moja ya tangazo inaweza kumuingizia hadi Dola 200,000.
Kwa sasa anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 100 milioni ingawa kuna uwezekano mkubwa ukaongezeka maradufu ikiwa atafanikiwa kutimkia Saudi Arabia ambako amewekewa ofa nono.
MIJENGO YAKE
Salah anaishi maisha ya kifahari jijini Liverpool na nyumba anayokaa ina thamani ya Dola 5 milioni.
Ndani ya mjengo huo kuna gym ya kisasa, bwawa la kuogelea, msikiti mdogo na uwanja mdogo wa kufanyia mazoezi binafsi anapokuwa nyumbani.
Mbali ya nyumba hiyo, Salah pia ana mjengo nchini Misri ambako ndiko amekuwa akikaa mara zote awapo likizo.
MSAADA KWA JAMII
Mohamed Salah ni mmoja wa wanamichezo wanaosifika kwa kuwa na moyo wa kusaidia jamii, hasa nchini kwao Misri, ambapo amekuwa akitumia mamilioni kubadilisha maisha ya watu.
Katika kijiji alicholelewa cha Nagrig, mwanasoka huyo amefanikiwa kujenga shule ya kisasa kwa ajili ya watoto, huku
akianzisha kituo cha vijana kwa ajili ya michezo na maendeleo na vilevile amefadhili mradi wa majisafi wenye thamani ya Dola 450,000.
Pia nyota huyo ana taasisi iitwayo Mohamed Salah Charity inayotoa msaada kwa jamii na makundi maalumu, ambapo 2018 alitoa zaidi ya Pauni 200,000 kusaidia mfuko wa taifa wa ‘Long Live Egypt’ uliolenga kuimarisha uchumi wa nchi.
MAISHA NA FAMILIA
Salah yupo katika ndoa na Magi Sadeq tangu 2013 na pamoja wamefanikiwa kupata watoto wawili ambao wote ni wakike wakwanza ni Makka aliyezaliwa mwaka 2014 na Kayan, 2020.
Ripoti nyingine zinadai hadi sasa ana watoto watatu na wamwisho alizaliwa mwaka 2025.
Muda mwingi jamaa amekuwa akiutumia kukaa na familia yake ikiwa yupo mapumzikoni, sio mtu wa starehe kabisa.