Utata pambano la Usyk, Verhoeven
Muktasari:
- Kutokana na uamuzi wa kuwepo kwa pambano hilo lililopangwa kupiganwa Mei 23, 2026, linatafsiriwa kama la maonyesho na si ushindani na kinachofanyika ni kama kuuweka rehani mkanda wa Uzito wa Juu wa WBC.
NEW YORK, MAREKANI: BARAZA la Ngumi Duniani (WBC), limeibua tena mjadala mkali kutokana na uamuzi wa kutatanisha walioutoa kuhusu pambano la uzito wa juu kati ya Oleksandr Usyk dhidi ya mpiganaji wa kickboxing, Rico Verhoeven linalotarajiwa kupigwa huko Giza, Misri.
Kutokana na uamuzi wa kuwepo kwa pambano hilo lililopangwa kupiganwa Mei 23, 2026, linatafsiriwa kama la maonyesho na si ushindani na kinachofanyika ni kama kuuweka rehani mkanda wa Uzito wa Juu wa WBC.
UTATA ULIPO
Kwa mujibu wa Rais wa WBC, Mauricio Sulaiman alisema pambano hilo si la ubingwa bali ni maalumu na la heshima kwa baraza hilo, huku awali lilitangazwa kama la ubingwa.
Ufafanuzi huo wa rais huyo ulionekana kama kupunguza ukosoaji uliokuwa unaongezeka kwa kuona kama kumpa mpiganaji wa kickboxing aliye na ushindi mmoja tu katika ndondi za kulipwa dhidi ya mpinzani mwenye rekodi ya 0–5 nafasi ya kupigania ubingwa wa dunia kunadhoofisha mfumo wa haki unaotegemea ubora na mafanikio ya wapiganaji wa mchezo huo.
Miongoni mwa wanaoonekana kunyimwa nafasi ni bingwa wa muda wa WBC, Agit Kabayel, ambaye inatajwa ana haki ya kuupigania mkanda huo kutokana na kiwango chake pamoja na ushindi wa mapambano ya uzani wa juu.
MABADILIKO YA GHAFLA
Baada ya kuona maneno ni mengi ya ukosoaji, ndani ya saa 24, WBC ilibadilisha msimamo wake na kudai pambano hilo litakuwa la heshima lakini la kuwania mkanda huo, huku ikiomba radhi kutokana na sintofahamu iliyojitokeza.
Hivyo, Bodi ya WBC iliamua kuliruhusu pambano hilo kwa Usyk kutetea mkanda wake kwa hiari na kuonekana kama ni kuweka mkanda halisi wa uzani wa juu hatarini.
Uamuzi huo, uliothibitishwa katika taarifa zilizotolewa mwanzoni mwa Machi 2026 baada ya ukosoaji mkali na wengi wanaamini waliostahili kuwania mkanda huo wamewekwa kando kwa sababu ni pambano lenye mvuto wa kibiashara.
HESHIMA YA MKANDA INAVYOYEYUKA
Kutokana na uamuzi huo, inaonekana kuna tatizo katika uongozi wa WBC kwani kuna kipindi mkanda unalindwa hadhi yake na wakati mwingine unatumika isivyo na hivyo kupoteza thamani yake kwa kuruhusu mapambano ya maonyesho kama hayo.
Kwa mabondia kama Kabayel, inachukuliwa kama kuwanyima haki ya kupigania mkanda huo na kusubiri muda mrefu licha ya mafanikio yao ulingoni, na hivyo fursa zao zinacheleweshwa kutokana na uamuzi unaoweka mbele masilahi ya kibiashara na mapato badala ya uadilifu wa michezo.
Hata hivyo, inaelezwa ingawa Usyk ana haki chini ya kanuni za WBC kuchagua mpinzani wake ili kutetea mkanda huo, wakosoaji wanasema ingewezekana akapambana kwanza na wapinzani wa uzani wa juu kabla ya kushiriki pambano kama hilo.
TAMBO ZAO
Usyk ambaye ni bingwa wa dunia wa uzani wa juu asiye na mpinzani mara mbili, anashikilia mikanda ya World Boxing Association (WBA), World Boxing Council (WBC) na International Boxing Federation (IBF).
Bondia huyu hajapigana tangu mara ya mwisho alipomchapa Daniel Dubois kwa KO, kwenye Uwanja wa Wembley, England, Julai 2025.
Katika pambano hilo ambalo waandaaji wamelipa jina la Glory in Giza, bondia Mholanzi, Rico (36), atapanda ulingo wa ngumi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2014.
Akishusha tambo zake dhidi ya mpinzani wake, Usyk, ambaye hajawahi kupoteza katika mapambano yake 24 ya kulipwa, anasema: “Kwa kweli ninawaheshimu sana watu wanaofika kileleni kabisa katika michezo yao. Rico ni mmoja wao, ni mwanamichezo mwenye nguvu na bingwa mkubwa.
“Kuwa bingwa si suala la kuwa na mikanda tu. Ni miaka ya kazi ngumu, nidhamu na imani. Ninaiheshimu safari yake, kwa hakika yeye ni Mfalme wa Kickboxing. Lakini huu ni mchezo wa ngumi; ni mchezo tofauti wenye sheria zake na wafalme wake. Usiku mkubwa unakuja.”
Verhoeven alipigana mapambano 76 ya kickboxing na kushinda 66 kabla ya kutangaza kuachana na mchezo huo mwezi Novemba.
“Nimetumia miaka 12 kama bingwa asiye na mpinzani wa uzani wa juu katika kickboxing na nimetimiza kila lengo nililokuwa nalo,” anasema Verhoeven.
“Lakini kukaa kileleni kwa muda mrefu hakukuondoa njaa yangu ya ushindi, kulizidi kuiongeza.
“Sikutafuta maisha ya starehe, hivyo nikaanza kutafuta changamoto kubwa zaidi katika ulimwengu mwingine. Usyk ni bingwa asiye na mpinzani katika ndondi. Hiyo ndiyo changamoto inayoniahamasisha, asiye na mpinzani dhidi ya asiye na mpinzani. Bora akipambana na bora.”
MTAZAMO TOFAUTI
Mashirika mengine makubwa ya ndondi kama International Boxing Federation (IBF), World Boxing Association (WBA) na World Boxing Organization (WBO) yameonekana kujiepusha na mjadala huu na yanaendelea na ratiba zao kama kawaida.
Wakati huo huo, licha ya WBC kusisitiza litakuwa pambano la kipekee kutokana na kufanyika karibu na eneo la mojawapo ya maajabu saba ya dunia la Piramidi ya Giza na kuvutia mashabiki wengi, wakosoaji wanaona kinachofanyika ni onyesho tu la kibiashara na kunyima haki za mabondia wenye nia ya kuwania mkanda huo wa uzani wa juu.
Pia wengi wanaona si pambano la uwiano sawa wa uwezo kati ya mabondia hao, licha ya kuwa ni la ubingwa wa WBC, likitofautishwa na yale yaliyovutia kama la Anthony Joshua na Jake Paul, lililokuwa na burudani.
Wengine wameenda mbali zaidi na kuona kuna uwezekano upinzani kwa Usyk ni mdogo kwa baadhi ya mabondia wa uzani wake hivyo hakuna wa kumpa changamoto kuwania mkanda huo ndiyo maana akapambanisha na Verhoeven.
Hata hivyo, inaonekana pia bado wapo mabondia wengine wanaoweza kupambana naye na bondia huyo aliwahi kuachia taji lake la World Boxing Organization (WBO) badala ya kupambana na Fabio Wardley, huku jina la Agit Kabayel likitajwa mara kwa mara na mashabiki kama mpinzani halisi asiye na rekodi ya kupoteza na mwenye kasi ya mafanikio.
Badala yake, pambano lililotangazwa sasa linamkutanisha Usyk na bondia ambaye ni mgeni katika ngumi za kulipwa.
Mwaka 2023, Tyson Fury aliangushwa na kukaribia kushindwa na mpiganaji wa MMA, Francis Ngannou, katika pambano lake la kwanza la ngumi, tukio lililokaribia kuwa la kushangaza katika historia ya uzani wa juu. Hivyo, katika ulingo wa ndondi chochote kinaweza kutokea.
Hata hivyo, bondia mwenye nidhamu na mbinu kali kama Usyk anaonekana kuwa na uwezekano mdogo wa kurudia makosa yaliyofanywa na Fury.
Katika enzi ya sasa ya ndondi, ambako mara nyingine hamasa na faida za kifedha zinaweza kutangulizwa mbele ya mantiki ya michezo, pambano hili linaingia kwenye orodha ya yale yanayowafanya wengi kujiuliza: “Tumefikaje hapa?”
FAIDA KWA NANI?
Kwa upande wa Usyk, pambano hilo linaweza kumletea malipo makubwa ya fedha pamoja na ushindi unaotarajiwa kuwa rahisi dhidi ya mpiganaji ambaye bado anajifunza sheria za ndondi.
Lakini kwa mujibu wa wakosoaji, waliopoteza zaidi ni mashabiki kutokana na pambano hilo wanaloliona halina hadhi na kuna uhaba wa mapambano makubwa.