Usajili 11 ghali EPL historia ya ‘Big Six’
Muktasari:
- Ingawa dhana ya ‘Big Six’ ya Ligi Kuu England imekuwa ikiwakera baadhi ya mashabiki, hasa inapozungumziwa mafanikio ya kihistoria au ya karibuni, kwa upande wa matumizi ya fedha kwenye usajili klabu sita zinazounda kundi hilo zimekuwa zikizitumia fedha nyingi zaidi kuliko wapinzani wao. Zingine ndani ya Big Six ni Liverpool, Arsenal na Tottenham Hotspur.
LONDON, ENGLAND: CHELSEA, Manchester City na Manchester United zinaongoza kwa vikosi vya mastaa walionunuliwa kwa gharama kubwa katika Ligi Kuu England, ambapo matumizi makubwa ya fedha yameendelea kuzidi ligi nyingine kubwa Ulaya na duniani, huku utajiri wa klabu hizo ukiendelea kuonekana kupitia usajili.
Ingawa dhana ya ‘Big Six’ ya Ligi Kuu England imekuwa ikiwakera baadhi ya mashabiki, hasa inapozungumziwa mafanikio ya kihistoria au ya karibuni, kwa upande wa matumizi ya fedha kwenye usajili klabu sita zinazounda kundi hilo zimekuwa zikizitumia fedha nyingi zaidi kuliko wapinzani wao. Zingine ndani ya Big Six ni Liverpool, Arsenal na Tottenham Hotspur.
Kwa kuzingatia hilo, Transfermarkt imeunda kikosi cha wachezaji 11 kwa kila moja ya klabu hizo kilichonunuliwa kwa mamilioni ya Euro kwa kuangalia wachezaji ambao walinunuliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia ya kila klabu. Orodha hiyo inaweza kuwa na wachezaji ambao hawakufanikiwa kama ilivyotarajiwa, pamoja na wale ambao walionekana kuwa usajili wenye mafanikio.
Transfermarkt imezipanga timu hizo kwa kuzingatia jumla ya gharama za usajili wa wachezaji hao 11 kuanzia nafasi ya sita hadi ya kwanza. Fedha zote zimezungushwa hadi kiwango cha mamilioni ya Euro. Kwa mujibu wa Transfermarkt, takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa fedha zinazotumiwa katika soko la usajili, huku vikosi vya wachezaji 11 kutoka klabu hizo sita vikifikia jumla ya zaidi ya Euro 5.1 bilioni, na miongoni mwa mastaa wamehama kutoka kikosi kimoja kwenda sehemu nyingine na kuna mahali wametajwa zaidi ya mara moja.
6. Tottenham (Euro 701 milioni)
Tottenham ina kikosi chenye gharama ndogo zaidi miongoni mwa timu sita, ikiwa na thamani ya jumla ya Euro 701 milioni kwa gharama za usajili. Golini yupo Guglielmo Vicario ambaye ilimnunua kutoka Empoli kwa Euro 19 milioni, ilhali safu ya ulinzi inaundwa na Micky van de Ven (Euro 40 milioni kutoka Wolfsburg), Jan Paul van Hecke (Euro 60 milioni kutoka Brighton), Cristian Romero (Euro 54 milioni) na Pedro Porro (Euro 40 milioni kutoka Sporting). Katikati ya uwanja kuna Mateus Fernandes (Euro 99 milioni kutoka West Ham) na Sandro Tonali (Euro 108m kutoka Newcastle lakini yupo Juventus kwa sasa kwa mkopo) na ndiye usajili wa rekodi wa klabu hiyo. Mbele yao yupo Xavi Simons aliyenunuliwa kwa Euro 65 milioni kutoka RB Leipzig. Safu ya ushambuliaji inaundwa na Savio (Euro 88 milioni kutoka Man City), Dominic Solanke (Euro 64 milioni kutoka Bournemouth) na Mohammed Kudus (Euro 64m kutoka West Ham).
5. Arsenal (Euro 720 milioni)
Mabingwa wa EPL, Arsenal wana kikosi cha pili kwa gharama ndogo zaidi miongoni mwa ‘Big Six’, kwa jumla ya Euro 720 milioni.
Pale golini yupo David Raya aliyesajiliwa kutoka Brentford kwa Euro 32 milioni, ilhali safu ya ulinzi inaundwa na Riccardo Calafiori (Euro 44 milioni kutoka Bologna), Ezri Konsa (Euro 60 milioni kutoka Aston Villa), Shkodran Mustafi (Euro 41 milioni kutoka Valencia) na Ben White (Euro 58 milioni kutoka Brighton). Katikati ya uwanja upo usajili wa rekodi wa Arsenal, Declan Rice aliyesajiliwa kwa Euro 117 milioni kutoka West Ham akiwa pamoja na Bruno Guimaraes (Euro 88 milioni kutoka Newcastle). Eberechi Eze aliyesajiliwa kwa Euro 69 milioni kutoka Crystal Palace yupo nyuma ya mshambuliaji Kai Havertz aliyenunuliwa kwa Euro 75 milioni kutoka Chelsea. Pembeni wanakuwepo Noni Madueke (Euro 56 milioni kutoka Chelsea) na Nicolas Pepe (Euro 80 milioni kutoka Lille).
4. Man United (Euro 837 milioni)
Manchester United ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa na matumizi makubwa kwenye usajili, inashika nafasi ya nne kwa gharama ya kikosi chake cha wachezaji 11, ikiwa na jumla ya Euro 837 milioni. Golini yupo Andre Onana aliyesajiliwa kutoka Inter Milan kwa Euro 52 milioni. Safu ya ulinzi ina Lisandro Martínez (Euro 57 milioni kutoka Ajax), Harry Maguire (Euro 87 milioni kutoka Leicester), Leny Yoro (Euro 62 milioni kutoka Lille) na Aaron Wan-Bissaka (Euro 55 milioni kutoka Crystal Palace). Katikati ya uwanja kuna usajili wa rekodi wa klabu hiyo, Paul Pogba, aliyenunuliwa kutoka Juventus kwa Euro 105 milioni akiwa pamoja na Carlos Baleba aliyesajiliwa kwa Euro 76 milioni kutoka Brighton.
Kule pembeni kuna Jadon Sancho (Euro 85 milioni kutoka Borussia Dortmund) na Antony (Euro 95 milioni kutoka Ajax). Safu ya ushambuliaji inaundwa na Romelu Lukaku (Euro 85 milioni) na Rasmus Hojlund (Euro 80 milioni).
3. Liverpool (Euro 929 milioni)
Liverpool inashika nafasi ya tatu ikiwa na kikosi cha wachezaji 11 chenye gharama ya Euro 929 milioni, huku matumizi makubwa ya msimu uliopita yakichangia kwa kiasi kikubwa. Golini yupo Alisson Becker aliyesajiliwa kutoka Roma kwa Euro 73 milioni, huku safu ya ulinzi ina Milos Kerkez (Euro 47 milioni kutoka Bournemouth), Virgil van Dijk (Euro 85 milioni kutoka Southampton), Jeremy Jacquet (Euro 64 milioni kutoka Rennes) na Jeremie Frimpong (Euro 40 milioni kutoka Bayer Leverkusen). Katikati ya uwanja kuna Dominik Szoboszlai (Euro 70 milioni kutoka RB Leipzig) na Naby Keita (Euro 60 milioni kutoka RB Leipzig), huku Florian Wirtz (Euro 125 milioni) akiwa mbele yao. Safu ya ushambuliaji inaundwa na usajili wa rekodi wa klabu, Alexander Isak aliyesajiliwa kwa Euro 145 milioni kutoka Newcastle pamoja na Bradley Barcola (Euro 125 milioni kutoka PSG) na Hugo Ekitike (Euro 95 milioni kutoka Frankfurt).
2. Man City (Euro 972 milioni)
Manchester City inashika nafasi ya pili ikiwa na kikosi cha wachezaji 11 chenye thamani ya Euro 972 milioni, ambacho golini yupo Ederson, aliyesajiliwa kutoka Benfica kwa Euro 40 milioni. Safu ya ulinzi inaundwa na Josko Gvardiol (Euro 90 milioni kutoka RB Leipzig), Ruben Dias (Euro 72 milioni kutoka Benfica), Aymeric Laporte (Euro 65 milioni kutoka Athletic Club) na Joao Cancelo (Euro 65 milioni kutoka Juventus).
Katikati ya uwanja kuna Elliot Anderson aliyesajiliwa kwa Euro 135 milioni kutoka Nottingham Forest, akiwa pamoja na Ayyoub Bouaddi aliyenunuliwa kwa Euro 95 milioni kutoka Lille. Mawinga kuna Jack Grealish (Euro 118 milioni kutoka Aston Villa) na Antoine Semenyo (Euro 72 milioni kutoka Bournemouth). Nyuma ya mshambuliaji Omar Marmoush aliyesajiliwa kwa Euro 75 milioni kutoka Frankfurt upo usajili mpya wa rekodi wa klabu hiyo, Enzo Fernandez aliyenunuliwa kwa Euro 145 milioni kutoka Chelsea.
1. Chelsea (Euro 1 bilioni)
Chelsea, ambayo imekuwa ikitumia fedha nyingi kwenye usajili ina kikosi ghali zaidi kati ya timu hizo sita, huku jumla ya gharama za wachezaji wake 11 ikifikia Euro 1 bilioni, kwani golini yupo Kepa Arrizabalaga anayeelezwa kuwa kipa ghali zaidi kuwahi kusajiliwa baada ya Chelsea kumsajili kutoka Athletic Club kwa Euro 80 milioni. Safu ya ulinzi inaundwa na Marc Cucurella (Euro 65 milioni kutoka Brighton), Wesley Fofana (Euro 80 milioni kutoka Leicester) pamoja na wachezaji wapya Maxence Lacroix (Euro 61 milioni kutoka Crystal Palace) na Marco Palestra (Euro 57 milioni kutoka Atalanta). Katikati kiungo kuna Enzo Fernandez (Euro 121 milioni kutoka Benfica) na Moises Caicedo (Euro 116 milioni kutoka Brighton), huku Kai Havertz akiwa namba 10 baada ya kusajiliwa kwa Euro 100 milioni kutoka Bayer Leverkusen. Safu ya mbele inamjumuisha Romelu Lukaku aliyesajiliwa kwa Euro 113 milioni kutoka Inter Milan. Pembeni yake kuna usajili mpya wa rekodi wa Chelsea, Morgan Rogers, aliyesajiliwa kwa Euro 138 milioni pamoja na Mykhaylo Mudryk aliyesajiliwa kwa Euro 70 milioni kutoka Shakhtar Donetsk.