Usaili TFF, Mgeusa, Mniga kutoka jasho
Muktasari:
PANGA jingine linalosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka ni usaili wa wagombea, hasa wale watatu wanaowania nafasi ya juu katika uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
PANGA jingine linalosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka ni usaili wa wagombea, hasa wale watatu wanaowania nafasi ya juu katika uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Usaili huo unatarajiwa kufanyika leo ukiwahusisha Wallace Karia, ambaye anatetea kiti chake, Hawa Mniga na Evans Mgeusa, wanaowania kiti hicho chenye mamlaka makubwa katika uendeshaji wa mchezo huo unaopendwa na mamilioni.
Watatu hao walishapita katika mchujo wa awali ambao uliangalia zaidi kukamilisha mambo muhimu ambayo mgombea anatakiwa aambatanishe katika fomu yake; nyaraka za utambulisho na uraia, vyeti, risiti za malipo ya fomu na taarifa nyingine binafsi muhimu.
Lakini usaili unaofuata utaangalia ndani zaidi.
Kifungu cha tisa cha kanuni za uchaguzi za TFF kinaeleza vigezo ambavyo vinatumika kuchambua wagombea uongozi wa TFF na hivyo ndivyo vitakavyohitaji maelezo zaidi na uthibitisho, hasa wa maandishi.
Kifungu cha 1 (1) kinataka mgombea awe Mtanzania, yaani hapa angalau aonyeshe Kitambulisho cha Taifa, au namba na kama hajafanikiwa kukipata hadi sasa, basi vyeti kama vya kuzaliwa kuonyesha ni Mtanzania.
Kifungu cha 1 (2), kinamtaka mgombea—si wa urais—kuwa na elimu ya angalau kidato cha nne na awe na cheti cha elimu. Hapa si cheti cha kuhudhuria elimu ya sekondari au, bali kinachoonyeha kuwa mgombea hakufeli kiasi cha kukosa cheti kinachoonyesha kiwango cha ufaulu wa masomo yake.
Kigezo hiki ndicho kinasumbua wagombea wengi na baadhi kuibua maneno kuwa wameonewa, kumbe hawana cheti hicho muhimu. Kigezo hiki pia ndicho kinachowafanya wachezaji wengi wa zamani washindwe kupanda ngazi za juu za ukocha na hivyo kushindwa kuongoza timu za Ligi Kuu kwa kuwa ndicho muhimu kwa mafunzo hayo.
Sifa nyingine muhimu, itakayowapa shida Mniga na Mgeusa ni uzoefu uliothibitika wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.
Inawezekana mtu akawa mjumbe wa kuteuliwa katika klabu ya Ligi Kuu ya Daraja la Kwanza, lakini uteuzi wake ukawa wa ‘kiushikaji’ usio na nyaraka zozote. Hilo litamuondolea sifa ya kugombea nafasi.
Sifa hii pia husababisha utata na baadhi ya wagombea kuitumia kuelekeza lawama kwa mamlaka kuwa hazimtaki.
Sifa ya tano na sita ni za kawaida maana zinahusu umri wa kuanzia miaka 25 na mgombea awe amewahi kucheza soka, kufundisha, au kuongoza katika ngazi ya mkoa, ligi daraja la kwanza au la pili, lakini inaweka, angalau miaka mitano.
Kigezo cha saba ndicho ambacho kilikuwa kikivutia wadau walio nje ya mpira wa miguu kupeleka pingamizi dhidi ya wagombea ambao wanaonekana wana kasoro.
Kifungu cha 1 (7) kinaeleza kuwa mgombea wa uongozi anatakiwa kuwa muadilifu, mkweli, uwezo wa utendaji na mwenye kutimiza na kutekeleza majukumu na malengo ya TFF.
Ina maana kama Kamati ya Uchaguzi itakuwa na taarifa za kiongozi aliye madarakani kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, atatakiwa aidhihirishie kamati kuwa upungufu huo haukusababishwa na matatizo yake.
Lakini hoja kubwa katika kigezo hicho ni uadilifu. Hapa ndipo wadau walipokuwa wakiingiza mikingamo yao. Kama mgombea alikuwa na matatizo katika biashara zake zilizosababishwa na vitu kama kukwepa kodi, kutakatisha fedha na uhalifu mwingine wa kifedha, alisulubiwa na kigezo hiki.
Wale waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya jinai au wameshakutwa na jinai na kuhumiwa kifungo bila ya mbadala wa faini, nao wanasulubiwa na kigezo hiki.
Hata katika uendeshaji wa mpira wa miguu, kama kuna udhaifu unaoonyesha kuwa kiongozi alikuwa na upendeleo, alishindwa kuongoza vyema eneo lake, anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha, atalazimika kujiandaa kukabiliana na hali hii. Hapa kama kamati itakuwa thabiti dhidi ya wagombea bila ya kubagua.
Sifa ya nane ambayo imemfanya mjumbe wa zamani wa kamati ya utendaji, Abdallah Bulembo kwenda Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) ni elimu ya Chuo Kikuu kwa mgombea wa nafasi ya rais wa TFF. Sifa hii pia inajazilizwa na kipengele kinachomtaka mgombea kuwa na uwezo na haiba ya kuliwakilisha shirikisho ndani na nje ya nchi.
Kama nilivyoeleza katika makala za awali, hoja ya wanaopinga sifa hii ni ubaguzi, na Bulembo anasema kabisa kuwa ni “kuwabagua wanasoka” ambao kutokana na kazi yao inakuwa shida kufikia elimu ya juu kiasi hicho.
Lakini hoja yao inakuwa na mashiko pale katiba ya TFF inaposema kuwa hakutakuwa na ubaguzi wa aina yoyote. Mara nyingi, ibara hii katika katiba za vyombo kama hivyo huibua misuguano na hata kutumiwa vibaya na watetezi wa mambo ambayo hayakubaliki katika jamii.
Mfano watetezi wa ushoga hutumia ibara hii kudai kuwa wanabaguliwa, kitu kinacholazimisha katiba kueleza kwa usahihi aina ya ubaguzi unaozungumziwa na pia kama ni tamaduni basi ziwekwe bayana.
Dhana ya ibara hiyo katika katiba za jamii zilizoendelea ni fikra kwamba wananchi wamepata elimu ya kutosha kiasi cha kuwa na uwezo wa kubeba majukumu yoyote, ili mradi awe na sifa nyingine kama uzoefu wa miaka mitano, rais, muadilifu na nyingine.
Lakini katika nchi kama hii ambayo ujuzi unapatikana zaidi kwa kuwa katika elimu kwa muda mrefu, wale waliotumia muda mfupi katika elimu wanakuwa na ukomo wa kufahamu mambo mengi kuhusu uendeshaji wa taasisi, masuala ya kifedha, masoko na usimamizi wa watu.
Kwa wale ambao hawataridhika na mchujo wa Kamati ya Uchaguzi, katiba inawapa fursa ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa za Uchaguzi kupinga uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi.
Wanatakiwa kuambatanisha rufaa zao na Sh1 milioni.
Lakini tofauti na uamuzi wa Ali Saleh, aliyechukua fomu na kuenguliwa katika uchambuzi wa awali, kifungu hicho kinazuia mrufani kupeleka rufaa yake katika chombo cha serikali au mahakamani.
Tunaendelea na Makala hizi kesho.
Mwandishi wa safu hii alikuwa katibu mkuu wa TFF