Prime
Unafiki unaoua ufungaji bora Ligi Kuu Bara
KWA takribani misimu kumi ya kuwania ufungaji bora kwenye Ligi Kuu Bara, ni mara tatu tu ndio wazawa wamenyakua tuzo hiyo, hapa unamkuta Simon Msuva msimu wa 2016-2017 akiwa sambamba na Abdulrahman Mussa, kisha George Mpole yeye ilikuwa msimu wa 2021-2022 akichukua mbele ya Mkongomani Fiston Mayele baada ya ushindani uliodumu hadi siku ya mwisho na msimu wa 2020/2021 akishinda John Bocco ambaye pia ni mfungaji bora wa muda wote kwenye ligi akiwa na zaidi ya mabao 100.
Utaona huyu ndiye pekee alikuwa na uwezo wa kuhimili misukosuko na kutengeneza walau tabia ya kufunga mabao kwa tarakimu mbili kwa misimu kadhaa huku wengine wakiibuka msimu mmoja na misimu inaofuata wakishindwa walau kutengeneza idadi ya mabao yenye tarakimu mbili.
Kwa sasa kinara wa mabao ni mshambuliaji wa Namungo, Fabrice Ngoy mwenye mabao manane akifuatiwa na viungo wazawa watatu, Feisal Salum (Azam), Saleh Karabaka (JKT Tanzania) na Mudathir Yahya (Yanga) ambao kila mmoja ana mabao saba.
Chini yao kuna washambuliaji watatu, Prince Dube (Yanga), Laurindo Dilson ‘Depu’ (Yanga) na Selemani Mwalimu (Simba) waliofunga mabao sita kila mmoja.
Hata hivyo, katika listi ya wafungaji wa Ligi Kuu Bara misimu hiyo 10, washambuliaji waliobeba tuzo ya ufungaji bora walikuwa watano, waliobaki ni viungo.
Hiyo inatoa picha ni kweli hivi sasa dunia inahangaika kuzalisha wafungaji ndiyo maana wako wachache kulinganisha na miaka ya nyuma kwa sababu kufunga ni sanaa na wasanii hao walikuwa wanatunzwa wakishagundulika ili kufanya kazi yao hiyo kwa ufanisi.
Mifumo ilikuwa inawaruhusu kwa sababu kimbinu ndio kazi waliyokuwa wanaifanya kiwanjani. Mbali na uwezo wao huo wa kufunga ila timu pia zilikuwa zinawatafutia wepesi wa kutekeleza jukumu lao hilo ndani ya kiwanja kuwapunguzia kazi tofauti na nyakati hizi ambazo maendeleo ya sayansi kwenye mchezo yamepelekea kuzalisha washambuliaji wengi kuliko wenye sanaa ya ufungaji wakilazimika kuyatekeleza majukumu mengine kulingana na kimbinu, ishu ya kufunga hutokea kama watapata nafasi.
Washambuliaji wengi wa kisasa wamekuwa wakitumika zaidi kutekeleza mipango ya timu kuzuia na kushambulia, hivyo dunia inahangaika pia kuzalisha hao wasanii ndiyo maana sasa hivi mabao yanatoka kila eneo kulingana na nani amejikuta yuko kwenye nafasi ya kumalizia washambuliaji wa pembeni kazi yao kubwa imekuwa kufunga na jukumu la kutengeneza limekuwa ni la ziada.
Tukirudi hapa kwetu na sisi tuna baadhi ya changamoto zetu ukiachilia mbali hizo za mabadiliko ya kiufundi, wazawa wamekuwa wakikutana na mazingira magumu ya kufanyia kazi tofauti na wageni kwenye timu zetu kubwa ambako ndiko zinapotengenezwa nafasi nyingi za kufunga kuliko timu za madaraja ya kati.
Huku wazawa hawapewi muda wa kujitafuta kama wanavyopewa wageni yaani hawasaidiwi kisaikolojia pindi mambo yanapokuwa hayaendi vizuri.
Wachezaji wa kigeni mara nyingi hupewa muda wa kutosha kujitafuta wanapokuwa hawako kwenye kiwango kizuri. Wanasaidiwa kisaikolojia na kupewa nafasi ya kurejea katika ubora wao. Kwa upande mwingine, wazawa hukutana na ukosoaji mkali kutoka kwa mashabiki, wadau, na hata vyombo vya habari. Hukosa sapoti ya kisaikolojia na mara nyingi hupoteza kujiamini mapema.
Mfano halisi ni hali ya sasa ya mshambuliaji wa Simba, Selemani Mwalimu. Licha ya kuwa na takwimu nzuri ya mabao sita katika mechi 11, bado kuna sauti zinazodai haitoshi na timu inahitaji mshambuliaji mwingine. Hali hii inaonyesha wazi jinsi wazawa wanavyopimwa kwa viwango tofauti na wageni. Kama angekuwa mchezaji wa kigeni mwenye takwimu hizo, huenda angepongezwa na kupewa muda zaidi wa kuimarika.
Kinachofanyika mara nyingi kwa wazawa ni kutafutwa kwa takwimu hasi badala ya chanya. Nafasi wanazokosa, makosa wanayofanya, na upungufu wao hupewa uzito mkubwa kuliko mafanikio yao. Hii huongeza shinikizo kubwa kwao na kuathiri utendaji wao uwanjani. Bila msaada wa kisaikolojia, wengi hushindwa kuhimili presha hiyo na hupoteza mwelekeo wa taaluma zao.
Mfano mwingine ni namna wachezaji wa kigeni wanavyoweza kupewa muda mrefu wa kurejea kwenye kiwango chao. Wakati mwingine mshambuliaji wa kigeni anaweza kucheza mechi nyingi bila kufunga lakini bado akaendelea kuaminiwa.
Lakini mzawa akipitia hali kama hiyo, mara nyingi hutolewa kikosini au hata kutolewa kwa mkopo mapema sana. Hii inaua morali na kuzuia maendeleo yao.
Kauli kama “wachezaji wetu hawajitambui” zimekuwa zikitumika mara kwa mara, lakini ukweli ni kwamba kauli hizi zimekuwa kama kikwazo kwa maendeleo ya wazawa. Badala ya kuwajenga, zinawavunja moyo na kuwafanya waone hawathaminiwi. Ni muhimu kubadili mtazamo huu na kuanza kuwapa sapoti wanayohitaji.
Ili kuboresha hali hii, kunahitajika mabadiliko ya kimfumo na kimtazamo. Kwanza, timu zinapaswa kuwa na imani zaidi kwa wachezaji wazawa na kuwapa nafasi sawa na wageni. Pili, wadau wa soka wanapaswa kubadilisha namna wanavyowachambua na kuwahukumu wazawa. Badala ya kuangalia makosa yao pekee, ni muhimu pia kuthamini juhudi na mafanikio yao.
Vilevile, msaada wa kisaikolojia ni muhimu sana. Wachezaji wanapopitia nyakati ngumu, wanahitaji kuungwa mkono badala ya kubezwa. Hii itawasaidia kurejea kwenye kiwango chao haraka na kuwa na uthabiti wa muda mrefu.
Kwa kumalizia, Selemani Mwalimu ni mfano mzuri wa mshambuliaji mzawa mwenye uwezo mkubwa. Akipewa sapoti sahihi na kuaminiwa, anaweza kufikia viwango vya juu zaidi.
Ni jukumu la kila mdau wa soka kuhakikisha kuwa wazawa wanapewa mazingira bora ya kufanikiwa.
Tukifanya hivyo, tutaona ongezeko la washambuliaji wazawa wanaong’ara na hata kushindania mara kwa mara tuzo ya ufungaji bora.