Umewahi kuisikia vita ya masikio?
Muktasari:
- Mmoja kati ya michezo hiyo ni Ear Pull au mchezo wa kuvutana masikio ambao asili yake ni Marekani.
ALASKA, MAREKANI: INAWEZEKANA umeshuhudia michezo mingi duniani, lakini kuna baadhi ina upekee kutokana na namna inavyochezwa.
Mmoja kati ya michezo hiyo ni Ear Pull au mchezo wa kuvutana masikio ambao asili yake ni Marekani.
Makala haya yanakusogezea undani wa mchezo huo kuanzia historia, kanuni, sheria na kila kitu muhimu kinachouhusu.
HISTORIA YA MCHEZO
Shindano La kuvutana masikio (Ear Pull) ni mojawapo wa michezo ya jadi ya watu wa Kaskazini mwa Alaska, Marekani, ambako ndiko asili yake hasa katika jamii za Inuit na Yupik.
Awali, mchezo huo ulianzishwa ili kuchunguza uthabiti na nguvu za wapiganaji, hasa wakati wa misimu ya baridi ambapo ulilenga kuimarisha miili.
Mchezo huo ulianzishwa kama sehemu ya mazoezi ya kuwajengea uwezo watoto wa kustahimili baridi kali ya eneo la Arctic ambapo masikio ni sehemu nyeti katika kuhimili baridi kali. Kwa hiyo kuvuta masikio ilikuwa njia ya kuimarisha uvumilivu wa mwili na akili ya mhusika.
MASHINDANO YA DUNIA
Mashindano ya Ear Pull hufanyika kila mwaka kama sehemu ya tamasha la michezo ya jadi la World Eskimo-Indian Olympics (WEIO) linalofanyika huko Fairbanks, Alaska, Marekani.
WEIO ilianzishwa 1961 kama njia ya kuhifadhi michezo ya jadi ya asili ya Kaskazini mwa Amerika.
Mashindano hayo hufanyika kwa siku nne na hujumuisha michezo mbalimbali ya jadi ambapo mbali na Ear Pull, pia kuna Knuckle Hop, Blanket Toss, na mingineyo.
SHERIA NA KANUNI
Kwa mujibu wa sheria na kanuni wachezaji huketi wakiangalia ana kwa ana, huku miguu ikiwa imeshikana, kisha kamba nene ya nyuzi ambayo mara nyingi huwa ni ngozi hufungwa nyuma ya masikio yao.
Wachezaji hutakiwa kuvuta kamba hiyo kwa kutumia masikio yao hadi mmoja aachie au kushindwa kutokana na maumivu.
Mchezo huo unachezwa kwa mzunguko wa raundi tatu, ambapo kila mzunguko wachezaji hutumia sikio tofauti, na yule ambaye atashinda raundi mbili huibuka mshindi.
Wachezaji wanapaswa kuvutana moja kwa moja bila kupinda au kutikisa vichwa.
MASTAA MAARUFU, REKODI ZAO
Robert Okpeaha Jr ni bingwa mara 10 wa michuano ya dunia ya WEIO.
Nyota huyo alikuwa maarufu kwa uvumilivu wa maumivu na uwezo wa kuvuta masikio kwa muda mrefu bila kuachia.
Naye Asta Keller ni mshindi mara nane wa mashindano ya dunia ya Ear Pull kwa wanawake.
Alikuwa anatokea katika familia yenye damu ya mchezo huo ambapo baba na bibi waliwahi kuwa wachezaji maarufu enzi zao wakifanya maajabu.
USALAMA
Ingawa Ear Pull ni mchezo wa jadi, lakini una hatari za kiafya.
Mchezo huo mara kadhaa umewahi kusababisha majeraha kama vile kupasuka kwa ngozi nyuma ya sikio, maumivu makali na wakati mwingine majeraha yanayohitaji matibabu ya haraka. Mashindano mengi yanayofanyika kwa sasa yanahusisha uangalizi wa hali ya juu wa kiafya. Mara nyingi wachezaji hutumia barafu baada ya mechi ili kupoza maumivu.
UMUHIMU WA KITAMADUNI
Mchezo wa Ear Pull siyo tu kwamba ni burudani, bali ni njia ya kuhifadhi tamaduni za kiasili na kuelimisha vijana juu ya ushindani wenye heshima, nguvu na ustadi wa kimwili.
Mashindano hayo yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya sherehe za jadi na mikusanyiko ya kijamii katika maeneo ambako huchezwa.
ZAWADI NA SHERIA MUHIMU
Washindi wa mchezo huo hususan katika mashindano ya dunia hupokea vyeti vya ushindi, fedha au zawadi za kiutamaduni.
Mara nyingi zawadi za fedha zinazotolewa huwa ni kati ya Dola 5,000 hadi 10,000 kwa washindi wa kwanza ambapo pia huongezewa na vyeti.
Kulingana na sheria mchezaji hapaswi kutumia mwili mzima kuvuta, ni lazima nguvu itumike kupitia masikio pekee.
Ikiwa mchezaji anasikia maumivu au kuonyesha ishara ya maumivu makali mechi humalizia mara moja. Mara zote mechi hizo husimamiwa na mwamuzi ambaye hutoa maelekezo na kuamua mshindi.
Mashindano hayo mara nyingi yanaweza kuwa ya dakika chache kati ya tano hadi 10.