Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngushi: Kuna umuhimu wa kuwa na wanasaikolojia

NGUSHI Pict

Muktasari:

  • Ngushi, ambaye amewahi kupitia mazingira ya ushindani Yanga, anasema maisha ya soka yana nyakati za furaha na maumivu, lakini mchezaji anatakiwa kuwa na uwezo wa kuvumilia na kuendelea kupambana hata anapokutana na mambo yanayoweza kumkatisha tamaa.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiendelea kushuhudia ushindani mkali, mshambuliaji wa Mashujaa, Crispin Ngushi amefunguka kuhusu changamoto alizopitia nje ya uwanja wakati yupo Yanga, namna zilivyomfanya kutafakari mambo mengi maishani, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na wanasaikolojia kwenye timu ili kusaidia wachezaji hasa wanapokutana na changamoto hiyo.

Ngushi, ambaye amewahi kupitia mazingira ya ushindani Yanga, anasema maisha ya soka yana nyakati za furaha na maumivu, lakini mchezaji anatakiwa kuwa na uwezo wa kuvumilia na kuendelea kupambana hata anapokutana na mambo yanayoweza kumkatisha tamaa.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo amezungumzia pia ubora wa Ligi Kuu msimu huu, maendeleo ya washambuliaji wazawa, malengo yake akiwa na Mashujaa pamoja na umuhimu wa kuwa na wataalamu wa saikolojia katika soka la Tanzania.


NGU 01

MAJERAHA YALIMRUDISHA NYUMA

Ngushi anasema majeraha yaliyomtokea mwaka 2022 yaliyomuumiza na kumfanya ajiulize maswali mengi, hasa alipokuwa akitafakari kwa nini changamoto hizo zimemkuta wakati ambao alianza kupiga hatua.

Anakiri kipindi hicho hakikuwa rahisi kwake, lakini hakukubali hali hiyo imnyime matumaini ya kuendelea na maisha yake ya soka.

“Nilipitia jambo ambalo liliniumiza sana na kunifanya nitafakari mambo mengi kichwani. Nilijiuliza kwa nini limetokea wakati huu ambao niko katika kipindi cha mafanikio, kwa nini lisingetokea kabla au kwa nini limetokea sasa,” anafafanua.

Hata hivyo, anasema aliamua kukubali hali iliyotokea, kumshukuru Mungu na kuendelea kuamini angeweza kupona maumivu aliyokuwa akiyapitia na kurejea katika majukumu yake.

Anasema jambo hilo limemfundisha mafanikio ya mchezaji hayaamuliwi na uwezo wake wa kucheza pekee, bali pia namna anavyokabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza nje ya uwanja.


WANASAIKOLOJIA MUHIMU

Kutokana na uzoefu wake, Ngushi anaamini soka la Tanzania linahitaji kuweka nguvu zaidi katika kuwasaidia wachezaji kukabiliana na changamoto za kisaikolojia, hasa wanapopitia majeraha au matatizo yanayoweza kuathiri hali yao ya kawaida.

Anatoa mfano wa soka la Ulaya, ambako wachezaji wanapokutana na changamoto za aina hiyo wanapata msaada wa kitaalamu unaowasaidia kurejea katika hali nzuri.

Kwa mtazamo wake, msaada huo ni muhimu zaidi kwa wachezaji wanaocheza katika klabu ndogo, ambazo huenda hazina rasilimali za kutosha kama zile za klabu kubwa.

Anasema mchezaji anapoumia, kurejea katika kiwango chake cha awali kunaweza kuchukua muda mrefu, jambo linaloweza kuathiri nafasi yake ya kucheza na hata kuendelea kubaki kwenye klabu yake.

“Ni vizuri kuwepo na wataalamu wa saikolojia kwa sababu mchezaji anapoumia, kurejea katika kiwango chake cha awali kunakuwa kugumu. Kwa klabu kubwa, jambo hilo linaweza kuwa rahisi zaidi kwa sababu zina watu wa kumsaidia, lakini kwa klabu ndogo inakuwa changamoto,” anasema.

Ngushi anaamini Tanzania inapaswa kuwekeza katika wataalamu wanaoweza kuwasaidia wachezaji wazawa, ili waweze kukabiliana na changamoto za kiakili na kuendelea kuonyesha uwezo wao uwanjani.


NGU 02

LIGI YA MOTO

Akizungumzia mwenendo wa Ligi Kuu msimu huu, Ngushi anasema ushindani umeongezeka kwa sababu timu nyingi zimejipanga vizuri na wachezaji wamekuwa wakionyesha kiwango kizuri.

Anasema ligi hiyo imekuwa ngumu kutabiri matokeo yake, huku akiamini ushindani huo utaendelea hadi mwisho wa msimu kutokana na timu nyingi kuwa na malengo na mipango ya kufanya vizuri.

“Ligi ni ya moto sana. Ni ngumu na imekuwa bora zaidi msimu huu kwa sababu unaona kila timu na wachezaji wake wanafanya vizuri. Nafikiri ushindani utaendelea hadi mwisho kwa sababu klabu nyingi zimejipanga na kila moja ina malengo yake,” anasema.

Ngushi anaamini hiyo ni ishara nzuri kwa maendeleo ya soka la Tanzania, kwa kuwa ushindani wa timu nyingi unaweza kuongeza ubora wa ligi na kuwafanya wachezaji wajitume zaidi wanapokuwa uwanjani.


NGU 03

WAZAWA KUTWAA KIATU

Ngushi anawapongeza washambuliaji wazawa kwa kujituma na kuonyesha uwezo wa kufunga mabao.

Anasema wachezaji wa ndani wanahitaji kuendelea kupewa moyo na kuaminiwa, huku akitolea mfano wa Anuary Jabiir, ambaye anaongoza kwenye orodha ya wafungaji akiweka kambani mabao saba.

Ngushi anaamini inawezekana mchezaji Mtanzania akamaliza msimu akiwa kinara wa ufungaji, iwapo ataendelea kuonyesha kiwango kizuri na kupata sapoti.

“Tunapaswa kuendelea kupeana moyo na kufarijiana. Pale ambapo mchezaji anafanya vizuri, tumpe pongezi zake. Anuary anafanya vizuri na tunamuombea aendelee na kiwango hicho, na sisi wengine tuliopo nyuma tuendelee kujituma,” anasema.


NGU 04

MALENGO YAKE MASHUJAA

Akizungumzia mipango yake binafsi msimu huu, Ngushi anasema amejiwekea malengo ambayo anataka kuyafikia huku akilenga kuisaidia Mashujaa kupata matokeo mazuri katika kila mchezo.

Anasema licha ya kuwa na malengo yake binafsi, kipaumbele chake ni kuisaidia timu kufikia malengo iliyoweka, akiamini mafanikio ya pamoja yana nafasi kubwa katika safari ya mchezaji.

“Binafsi nimejipanga kuwa na msimu mzuri ili niisaidie timu yangu kufikia malengo tuliyojiwekea na kupata matokeo mazuri katika kila mechi. Nina malengo yangu, lakini kwa sasa siwezi kuyaweka yote wazi. Ninachotaka ni kuendelea kufanya vizuri na kusogea karibu na malengo hayo,” anasema.


YANGA ILINIJENGA

Ngushi pia anakiri kipindi akiwa Yanga kilimsaidia kujifunza mambo mengi, si kuhusu soka pekee, bali pia namna ya kuishi na watu wenye tabia na mazingira tofauti.

Anasema kukutana na wachezaji wazawa na wa kigeni kulimpa uzoefu mkubwa, huku akijifunza namna ya kuishi katika mazingira tofauti ya ushindani na kuvumilia wakati anapokuwa na nafasi ya kucheza au anapokosa nafasi hiyo.


AFCON 2027 ITAKUWA BORA

Akizungumzia maandalizi ya Tanzania kuelekea AFCON 2027, ambayo itafanyika kwa ushirikiano wa Kenya na Uganda, Ngushi ameonyesha matumaini kutokana na maendeleo anayoyaona nchini.

“Tuna vipaji vingi na kila mchezaji anaonyesha kiwango bora naamini nje ya maandalizi ya mashindano hayo lakini Tanzania itafanya vizuri na ina wachezaji wakushindana.”


OLISE

Ngushi ni mtu wa mitindo na mchezaji anayemkubali na kumfuatilia kwa kuvaa ni Michael Olise wa Bayern Munich na Timu ya Taifa ya Ufaransa.

“Wachezaji sasa hivi wa Tanzania tumebadilika kwenye uvaaji, wengi wanapenda kujiweka nadhifu sana hata mimi ni mmojawapo ukiangalia mtindo wangu wa nywele, mavazi na namkubali sana Olise.”


ANAMSIKILIZA IBRAAH

“Nawakubali wasanii wote wa Bongo na hata nasikiliza sana muziki wa Bongo Fleva lakini kwa sasa namsikiliza Ibraah na albamu yake yote aliyoiachia naikubali sana.”