UFUNDI, NAMBA... Mabao 78, rekodi ya siku mbili Ligi Mabingwa Ulaya itajirudia?
Muktasari:
- Kwa ujumla kila shabiki wa soka anapenda mabao na yanaonekana kwa sasa huko Ulaya. Mechi tisa zilizochezwa Jumatano, Oktoba 14, zilizalisha jumla ya mabao 46.
LIGI ya Mabingwa Ulaya inaendelea tena leo na kesho katika viwanja mbalimbali; lakini nini kinachochochea ongezeko la mabao katika mashindano hayo? Siku ya pili wiki iliyopita ya mechi za msimu wa 2026/27 wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ilishuhudia rekodi ya idadi ya mabao yakifungwa. Je, mabadiliko ya mfumo wa mashindano yamechangia hali hiyo, na ongezeko hilo la mabao litaendelea?
Kwa ujumla kila shabiki wa soka anapenda mabao na yanaonekana kwa sasa huko Ulaya. Mechi tisa zilizochezwa Jumatano, Oktoba 14, zilizalisha jumla ya mabao 46. Katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni siku mbili tu zilizowahi kuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao, na zote zilikuwa katika siku za mwisho zenye ushindani mkubwa za hatua ya ligi katika misimu ya 2024/25 na 2025/26.
Jumanne iliyopita, Oktoba 13, mabao 32 yalifungwa. Ingawa idadi hiyo haikufikia kiwango cha mabao mengi yaliyoonekana Jumatano, bado iliifanya siku hiyo kushika nafasi ya pamoja ya 29 kati ya siku 869 zilizowahi kuwa na mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa kuzingatia idadi ya mabao yaliyofungwa.
Jumla ya mabao 78 yaliyofungwa Jumanne na Jumatano yaliifanya siku ya pili ya mechi za msimu wa 2026/27 kuwa na idadi kubwa zaidi ya mabao katika historia ya mashindano hayo. Hiyo ilikuwa ni mabao tisa zaidi ya 69 yaliyofungwa katika siku ya kwanza ya mechi za msimu huu. Wakati huo, idadi hiyo ya mabao 69 ilikuwa rekodi ya pili kwa wingi tangu kuanzishwa kwa mfumo mpya wa hatua ya ligi katika msimu wa 2024/25.
MWENDO WA NAMBA
Katika siku mbili za kwanza za mechi za msimu wa 2026/27, mabao 147 yamefungwa katika mechi 36. Wastani wa mabao 4.08 kwa kila mchezo ndiyo wa juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Ni misimu ya 1959/60 pekee iliyokuwa na wastani wa mabao 4.19, na 1955/56 iliyokuwa na wastani wa mabao 4.38, iliyozidi kiwango hicho, ikijumuisha pia misimu ya zamani ya Kombe la Ulaya.
Swali la kujiuliza kwa nini mabao yanafungwa kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote? Je, tofauti za uwezo kati ya wapinzani zimeongezeka, au timu zimepata uhuru zaidi wa kupambania matokeo kutokana na mfumo mpya wa raundi ya kwanza?
Katika mfumo wa zamani wa hatua ya makundi uliotumika kuanzia msimu wa 2003/04 hadi 2023/24, timu ziligawanywa katika makundi manane yenye timu nne kila moja. Timu 16 kati ya 32 zilifuzu kwenda hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, sawa na asilimia 50.
Lakini kwa sasa, katika mfumo wa ligi wenye timu 36, timu nane za juu hufuzu moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora. Hata hivyo, jambo muhimu ni kwamba timu nyingine 16 hupewa nafasi ya pili ya kufuzu kupitia raundi ya mchujo ya mtoano. Hii ina maana kwamba sehemu kubwa zaidi ya timu sasa hufuzu kutoka hatua ya ligi. Jumla ya timu 24 kati ya 36 zinaweza kuendelea na mashindano, sawa na asilimia 66.7.
Inaweza kuelezwa kuwa hali hiyo imepunguza kiwango cha hatari ya kutolewa mapema na kuziwezesha timu kuchukua hatua zaidi katika mechi zao nane za hatua ya ligi.
Chukulia mfano wa Benfica katika msimu uliopita. Timu hiyo ilipoteza mechi tano kati ya nane za hatua ya ligi, lakini ilifanikiwa kujipenyeza katika raundi ya mchujo ikiwa nafasi ya 24. Huo ni uthibitisho kwamba katika mfumo mpya timu inaweza kupoteza zaidi ya nusu ya mechi zake na bado ikaendelea na mashindano.
PSG imetwaa mataji mawili ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kumaliza nje ya nafasi nane za juu katika hatua ya ligi katika misimu yote miwili. Kwenye kila msimu, ililazimika kupitia raundi ya mchujo ya mtoano ili kufuzu hatua inayofuata.
Katika misimu hiyo miwili iliyowapa ubingwa, PSG ilishinda nusu tu ya mechi zake za hatua ya ligi, yaani mechi nane kati ya 16. Jambo jingine linaloonekana tangu kuanzishwa kwa hatua ya ligi msimu wa 2024/25 ni kuongezeka kwa ushindi wa mabao mengi katika raundi ya kwanza ya mashindano. Kwa muktadha wa makala hii, chukulia ushindi wowote wa tofauti ya mabao manne au zaidi kuwa ni ushindi wa kishindo.
HUKO NYUMA VIPI?
Katika misimu 21 ya mfumo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia 2003/04 hadi 2023/24, mechi 190 kati ya 2,016 zilimalizika kwa timu moja kushinda kwa tofauti ya mabao manne au zaidi. Hiyo ni asilimia 9.4. Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa hatua ya ligi, asilimia 14.5 ya mechi zimeishia kwa timu moja kushinda kwa tofauti ya mabao manne au zaidi. Hilo ni ongezeko la zaidi ya asilimia tano.
Si hivyo tu, bali wastani wa tofauti ya mabao kati ya timu katika mechi umeongezeka kutoka 1.56 katika mfumo wa zamani wa hatua ya makundi hadi 1.86 katika mfumo mpya wa ligi wenye timu 36. Wakati huohuo, wastani wa tofauti ya ushindi umeongezeka kutoka mabao 2.02 hadi 2.17.
Hali hiyo haiwezi kuelezwa kikamilifu kwa kusema kwamba tofauti ya viwango vya uwezo kati ya wapinzani katika raundi ya kwanza imeongezeka. Baadhi ya ushindi wa mabao manne au zaidi umepatikana katika mechi ambazo, angalau kwa kuangalia uwezo wa timu kwenye karatasi, wapinzani walionekana kuwa na viwango vinavyokaribiana.
Tangu msimu wa 2024/25, kumekuwa na ushindi nane wa tofauti ya mabao manne au zaidi katika hatua ya ligi ambapo timu iliyoshinda iliifunga nyingine inayotoka katika mojawapo ya ligi tano kubwa za Ulaya. Katika misimu minne iliyotangulia ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ushindi wa aina hiyo ulikuwa saba pekee.
Mojawapo ya ongezeko linaloonekana zaidi ni idadi ya mechi zenye mabao mengi sana tangu kuanzishwa kwa mfumo wa hatua ya ligi.
Katika historia nzima ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni mechi 15 pekee ambazo zimekuwa na jumla ya mabao tisa au zaidi. Kati ya hizo, mechi nne zimechezwa katika hatua ya ligi tangu mfumo huo uanzishwe, sawa na asilimia 26.7.
Huenda hii ni hali ya kitakwimu iliyotokea kwa bahati tu, lakini bado inashangaza ikizingatiwa kwamba mechi za hatua ya ligi tangu msimu wa 2024/25 zinachangia asilimia 10.7 pekee ya mechi zote zilizowahi kuchezwa katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Labda, ongezeko kubwa la mabao halihusu mechi za hatua ya ligi pekee. Msimu uliopita ulikuwa na wastani wa juu zaidi wa mabao kwa kila mchezo katika raundi ya kwanza, mabao 3.38, na katika hatua ya mtoano, mabao 3.73, tangu msimu wa 2003/04.
MSIMU HUU UTAVUNJA REKODI?
Msimu huu, hatua ya ligi inaelekea kuvunja rekodi hiyo kwa wastani wa mabao 4.08 kwa kila mchezo. Na kwa kuzingatia kwamba wastani wa mabao katika hatua ya mtoano imeongezeka katika kila mmoja wa misimu mitatu iliyopita, huenda mashabiki wakashuhudia hali hiyo ikiendelea tena msimu huu.
Bado ni mapema mno kusema kama siku mbili za kwanza za mechi za msimu wa 2026/27 zilizopigwa wiki iliyopita zitakuwa zimeweka mwelekeo wa msimu mzima wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, mwenendo wa muda mrefu unaashiria kwamba mashindano hayo yanaweza kuwa na burudani kubwa zaidi kwa mashabiki kuliko wakati mwingine wowote.
Kuanzishwa kwa mfumo wa hatua ya ligi lilikuwa jambo jipya ambalo halikufahamika kwa uhakika matokeo yake yangekuwaje. Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), lilisema lilitarajia mabadiliko hayo ili kuleta mambo yaliyo bora zaidi kwa klabu, wachezaji na mashabiki lilipokuwa likieleza sababu za kufanya mabadiliko kabla ya kuanza kwa msimu wa 2024/25.
Mechi za ziada huenda zimeongeza mzigo kwa klabu na wachezaji, lakini ni vigumu kuona sababu nyingi za mashabiki kulalamika wakati wanapata burudani zaidi kupitia mabao mengi na mechi zenye ushindani mkubwa.