Real Madrid yamtaka Tebas kujiuzulu kwa kauli yake yenye utata
Muktasari:
- Tebas alitoa kauli hiyo kupitia mitandao ya kijamii, akiwatuhumu baadhi ya waandishi wa habari kuwa vinywa vya kueneza malalamiko ya Real Madrid kwa umma, huku akidai kuwa wanatumika kusambaza misimamo ya viongozi wa klabu hiyo.
MADRID, HISPANIAL: KLABU ya Real Madrid imemtaka rais wa Ligi Kuu ya Hispania (LaLiga), Javier Tebas, kujiuzulu mara moja kufuatia kauli yake iliyolinganisha mbinu za uongozi wa klabu hiyo na propaganda zilizokuwa zikitumiwa na Joseph Goebbels, aliyekuwa waziri wa propaganda wa utawala wa Nazi nchini Ujerumani.
Tebas alitoa kauli hiyo kupitia mitandao ya kijamii, akiwatuhumu baadhi ya waandishi wa habari kuwa vinywa vya kueneza malalamiko ya Real Madrid kwa umma, huku akidai kuwa wanatumika kusambaza misimamo ya viongozi wa klabu hiyo.
Rais huyo wa LaLiga alieleza kuwa Real Madrid inajaribu kujijenga kama klabu inayodhulumiwa na waamuzi pamoja na maamuzi yanayotolewa na uongozi wa ligi hiyo. Katika ujumbe wake, Tebas alidai kuwa uongozi wa Real Madrid unasimamia kundi la watu wanaotetea misimamo yake, huku televisheni ya klabu hiyo, Real Madrid TV, ikiwa mstari wa mbele katika kueneza ujumbe huo. Alidai kuwa mbinu zinazotumiwa ni kuchagua matukio yanayowanufaisha, kurudia malalamiko, kuchochea mashaka na kuwanyooshea vidole wanaowaona kuwa wapinzani wao. Tebas alilinganisha mbinu hizo na mfumo wa propaganda uliotumiwa na Goebbels wakati wa utawala wa Nazi kati ya mwaka 1933 na 1945. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ulinganisho wake ulihusu mbinu za propaganda pekee, si itikadi ya Nazi wala mashabiki wa Real Madrid. Kauli hiyo imeibua hasira ndani ya Real Madrid, ambayo imesema matamshi ya Tebas ni ya kukera, hayakubaliki kimaadili na hayastahili kutolewa na kiongozi mwenye nafasi kubwa katika soka la Hispania. Katika taarifa yake, Real Madrid ilisema mwenendo wa mara kwa mara wa Tebas unaonyesha kukosekana kwa kutopendelea upande wowote, heshima na usawa, mambo ambayo ni muhimu kwa mtu mwenye dhamana ya kuongoza taasisi ya soka.
“Real Madrid inaona kuwa haikubaliki kabisa na ni jambo zito kupindukia kwa mtu mwenye nyadhifa mbili muhimu katika soka la Hispania kutumia ulinganisho na mbinu za propaganda za utawala wa Nazi ili kuichafua klabu yetu, uongozi wake na televisheni yake” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
KESI YA NEGREIRA
Real Madrid pia imeeleza wasiwasi wake kuhusu kutajwa kwa sakata la Negreira katika ujumbe wa Tebas, kesi inayohusisha malipo yaliyofanywa na Barcelona kwa aliyekuwa makamu wa rais wa Kamati ya Ufundi ya Waamuzi nchini Hispania, Jose Maria Enriquez Negreira.
Mapema mwezi huu, Real Madrid ilituma nyaraka za ushahidi zenye kurasa 50,000 kwa Shirikisho la Soka la Ulaya (UEFA), ikiishutumu Barcelona kwa kufanya malipo yasiyo halali kwa kiongozi huyo wa zamani wa waamuzi.
Kwa mujibu wa madai yaliyotolewa nchini Hispania, Barcelona ililipa zaidi ya pauni milioni saba katika kipindi cha miaka 17 kuanzia mwaka 2001, wakati Negreira alipokuwa makamu wa rais wa kamati hiyo.
Hata hivyo, Barcelona imekuwa ikikanusha kufanya makosa yoyote, ikieleza kuwa malipo hayo yalikuwa kwa ajili ya ripoti za kiufundi na uchambuzi wa wachezaji na waamuzi zilizotolewa na kampuni inayomilikiwa na Negreira ( 81).
TEBAS KUMJIBU MADRID
Mvutano kati ya Real Madrid na Tebas si mpya, kwani pande hizo zimekuwa zikikinzana mara kwa mara, hasa kuhusu maamuzi ya waamuzi katika michezo ya hivi karibuni.
Mwezi uliopita, Tebas aliishutumu Real kwa kujenga kile alichokiita njama za kudumu kuhusu namna waamuzi wanavyoendesha mechi.