Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tusiiibeze nafasi CAF, tuboreshe haya

NONDO Pict


KWA mujibu wa viwango vya ubora wa ligi Afrika vinavyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Ligi Kuu Bara imekuwa ikitajwa kushika nafasi ya tano nyuma ya ligi za Misri, Morocco, Algeria na Afrika Kusini.


Hii ni hatua kubwa ambayo haiwezi kubezwa, hasa tukizingatia tulikotoka miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, swali la msingi linabaki: je, kweli ligi yetu inastahili nafasi hiyo au bado kuna pengo kati ya hadhi tuliyopewa na uhalisia wa ubora wake?


CAF hutumia vigezo maalum kupima ubora wa ligi na kipimo kikuu ni namna klabu za nchi husika zinavyofanya katika mashindano ya kimataifa wanayosimamia, yaani Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Kutokana na mfumo huu, Tanzania imenufaika sana kutokana na mafanikio ya klabu zake kubwa kama Simba SC na Yanga SC ambazo zimekuwa zikifanya vizuri mara kwa mara katika michuano hiyo.

Ushiriki wao wa mara kwa mara na kufika hatua za juu umechangia kukusanya alama nyingi kwa kipindi cha misimu mitano, ambacho ndicho CAF hutumia kufanya tathmini.

NOND 01

Pamoja na mafanikio hayo, ni muhimu kuwa wakweli, hadhi ya kuwa ligi ya tano bora bado haijaendana kikamilifu na ubora wa ndani wa ligi yetu.

Moja ya mambo yanayochangia taswira nzuri ya ligi ni uwekezaji mkubwa wa Azam TV ambao umeongeza thamani ya matangazo, mwonekano na mvuto wa ligi.

Hata hivyo, ubora wa ligi hauishii kwenye taswira tu, bali unahitaji msingi imara katika maeneo kadhaa muhimu.

Kwanza ni ushindani wa ndani ya uwanja. Ni kweli kumekuwa na maendeleo makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Klabu zimeanza kuwekeza katika mbinu za kisasa na makocha wamepewa nafasi zaidi ya kufanya kazi zao kitaalamu.

NOND 02

Tofauti na zamani, mchezo ulitegemea zaidi uwezo binafsi wa wachezaji, sasa tunaona timu zikicheza kama mfumo mmoja. Kuna uwiano mzuri kati ya mchezo wa kushambulia na kujilinda, pamoja na utekelezaji wa majukumu bila na kwa mpira.

Aidha, uwepo wa wachezaji wa kigeni umeongeza ushindani na kuwafanya wachezaji wazawa kuboresha viwango vyao.

Hata hivyo, ushindani huo bado haujasambaa kwa klabu zote. Ligi bado inaonekana kutawaliwa na timu chache, huku nyingine zikibaki nyuma kwa kiwango kikubwa.

Ili ligi iwe kweli ya daraja la juu, tunahitaji kuona ushindani mpana zaidi na timu nyingi zina uwezo wa kushindana kwa karibu, siyo zile zile kila msimu.

NOND 03

Eneo la pili ni usimamizi wa sheria za mchezo. Hili ni eneo nyeti sana ambalo linaathiri moja kwa moja uhalali wa matokeo ya michezo.

Kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu maamuzi ya waamuzi, hasa katika mechi kubwa. Matukio ya kufungiwa kwa waamuzi mara kwa mara yanaashiria kuwepo kwa changamoto katika ubora wa uamuzi.

Tatizo kubwa linaonekana ni kufanya maamuzi kwa presha au hisia badala ya kufuata weledi na kanuni za mchezo.

Ili ligi iwe na hadhi ya juu, lazima haki itendeke bila upendeleo, na waamuzi wawe na uwezo na ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi bila kuyumbishwa na mazingira ya nje.

Tatu ni miundombinu ya viwanja. Huu ndiyo msingi wa mchezo wenyewe. Ubora wa uwanja unaathiri moja kwa moja ubora wa mechi.

NOND 04

Viwanja vibovu vinapunguza kasi ya mechi, vinazuia utekelezaji wa mbinu na vinaweza kuongeza hatari ya majeraha kwa wachezaji.

Kumekuwa na jitihada za kuboresha viwanja, ikiwemo kufunga na kufungua baadhi yake kwa ajili ya ukarabati, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya. Ligi yenye hadhi ya juu inahitaji viwanja vya kisasa vinavyokidhi viwango vya kimataifa.

Kwa jumla, tunaweza kusema kwamba licha ya mafanikio yaliyopo, bado kuna pengo kati ya nafasi yetu ya tano na ubora halisi wa ligi.

Hata hivyo, hatupaswi kupuuza hatua kubwa tuliyopiga. Kutoka ligi ambayo haikutambulika sana kimataifa hadi kufikia nafasi ya tano Afrika ni mafanikio makubwa. Inaonyesha kuna mwelekeo mzuri na juhudi zinazaa matunda.

Kwa lugha rahisi, tunaendelea kusogea mbele. Kuna mambo mengi mazuri yanaendelea katika soka letu, pia kuna maeneo yanayohitaji maboresho makubwa. Ikiwa tutaimarisha ushindani, kuboresha usimamizi wa sheria na kuwekeza zaidi katika miundombinu, basi hatutakuwa tu na jina la ligi ya tano bora, bali tutakuwa tunastahili kabisa kuvaa kofia hiyo kwa uhalisia.