Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tusihamishie uchambuzi wetu AFCON

ZENGWE Pict


MECHI ya hatua ya 16 bora kati ya Tanzania na Morocco itaendelea kubakia kwenye mijadala kwa muda mrefu, hasa hapa kwetu ambako uchambuzi hujilenga sana katika makosa ya waamuzi kuliko mwenendo mzima wa mchezo.


Wakati mechi ikielekea ukingoni huku waandaaji wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), Morocco, wakiongoza kwa bao moja, Timu ya taifa ya soka 'Taifa Stars' ilipata ahueni kuwa inaweza kulazimisha sare na mchezo kwenda muda wa nyongeza baada ya Iddi Nado kuonekana ameangushwa ndani ya eneo la penalti.


Lakini, refa wa mchezo huo, Boubou Traore hakupuliza filimbi kuashiria kuwa beki wa Morocco, Adam Masina alimsukuma Nado ndani ya eneo la penalti na hivyo Tanzania kustahili penalti. Baada ya mpira kutoka, refa alianza kusikiliza maoni ya Refa Msaidizi wa Video (VAR), huku akizongwa na wachezaji wa Tanzania waliomtaka aende kuthibitisha uamuzi wake kwenye runinga ya uwanjani.

STAR 02

Matokeo yake, Traore akawaonyesha kadi ya njano wachezaji na maofisa wengine wa Tanzania waliokuwa kwenye benchi la ufundi. Na baadaye kidogo mchezo ulimalizika.

Wengi wamezungumzia tukio hilo kuwa ni la kuinyima Tanzania penalti ya dhahiri, lakini hakuna anayefafanua kilichotakiwa kitokee wala kuzungumzia mchezo mzima ili kuona timu yetu ilifanya mazuri yapi na kasoro zilikuwa zipi ili kujisahihisha kwa mechi nyingine zijazo.

Mtaalamu wa uamuzi kutoka Misri, Gamal Al-Ghandour ameungana na Watanzania wengi kupinga uamuzi wa Traore akisema Watanzania wamenyimwa haki yao.

STAR 03

Anasema Masina alimshika na kumsukuma waziwazi Nado wakati akiwa ndani ya eneo la penalti na kwamba mshambuliaji huyo wa Tanzania alikuwa ameumiliki mpira kikamilifu na hivyo kustahili penalti. Anasema timu ya VAR ilitakiwa imuambie refa aende kwenye runinga ye pembeni ya uwanja kuangalia vizuri tukio hilo.

Haya ndio maoni ya Watanzania wengi na ndio utamaduni tuliouzoea kwamba mechi ikiisha, kesho ni kujadili kosa la mwamuzi na baadaye kufikia muafaka kuwa ilikuwa ama ‘penalti ya wazi’ au ‘bao halali’ au ‘bao la kuotea kabisa’.

ZENG 05

Ndio utamaduni wetu wa kuchukua kakipande ka sheria na kushikilia hapohapo kuwa ndivyo sheria inavyosema na si tafsiri ya refa ya hiyo sheria. Refa wa zamani wa Syria, Jamal Al-Sharrif pia amezungumzia tukio hilo katika tovuti ya Africa Foot, akisema Traore alikuwa sahihi kabisa kutoizawadia Tanzania penalti.

Anajenga hoja kwamba kugusana kwa wawili hao kulikuwa asilia na hakukuwa na tukio la wazi la kuvuta au kumsukuma mchezaji mmoja kwa kiwango cha kuwezesha refa aizawadie Tanzania penalti.

ZENG 06

Pia mwamuzi huyo wa zamani amesema tukio hilo halikufikia kiwango cha kusababisha VAR iingilie kati na hivyo kuwaunga mkono mwamuzi wa kati na wa video kwa kutoangalia marudio ya tukio hilo.

Refa msaidizi wa video ni mwamuzi mwenye uhuru wa kuona video za mechi na ambaye anaweza kusaidia tu pale kunapokuwa na “kosa la wazi na dhahiri” au “tukio kubwa ambalo halikuonwa na refa wa kati” linalohusiana na kukubali au kukataa bao, kukubali au kutotoa penati, kadi nyekundu ya moja kwa moja, na kuadhibu mtu asiyestahili.

ZENG 02

Kwa mujibu wa protokali za VAR, ni lazima kuwepo na uamuzi wa refa kwanza yaani refa haruhusiwi kutofanya uamuzi halafu atumie VAR kuamua. Uamuzi wa kuruhusu mchezo uendelee baada ya tukio linaloonekana kama faulo unaweza kufanyiwa marudio ya VAR.

Protokali hizo zinasema uamuzi wa awali uliotolewa na refa utaendelea kuwa halali isipokuwa picha za marudio zitakapoonyesha kuwa kulikuwa na “uamuzi ulikuwa na kasoro ya wazi na dhahiri”. Pia ni refa tu anayeweza kuanzisha mchakato wa kuangalia marudio ya tukio wakati refa msaidizi wa video na wengine wanaweza tu kushauri kuangaliwa kwa marudio ya tukio.

STAR 08

Uamuzi wa mwisho kuhusu tukio hutolewa na mwamuzi ama kwa kutumia taarifa zinazotokana na marudio ya picha za video (VAR) au baada ya refa kwenda kuangalia mwenyewe marudio kwenye runinga ya uwanjani (On-field review, OFR).

Kwa hiyo Ghandoul anazungumzia kutokuwepo ushauri kutoka timu ya VAR kwa mwamuzi ili aangalie marudio ya tukio hilo, lakini Al-Sharrif anasema tukio hilo halikufikia viwango vinavyotakiwa kuwezesha VAR kuingilia kati.

Kwamba wachezaji hao wawili waligusana kwa njia ambayo haiepukiki kimpira na kwamba hakukuwa na tukio la wazi la kusukuma au kuvuta kwa nguvu kiasi cha VAR kuingilia kati.

STAR 01

Maoni ya refa siku zote ndiyo yanasimama na si maoni ya watu waliokaa nje kutathmini tukio kwa kuliangalia kwenye picha za marudio. Ndio maana hata yule wa VAR ambaye huwa kwenye chumba chenye runinga takriban sita, kompyuta na wasaidizi wake hawezi kujiamulia tu kwamba tukio fulani ni faulo, bali humpa taarifa za kutosha mwamuzi ilia one kama kuna umuhimu wa kuangalia marudio au aendelee na uamuzi wake wa awali.

Na kama wataona refa hatosheki na taarifa zao, basi humshauri aende kuangalia runinga ya pale uwanjani ili ajiridhishe.

Tunapowaambia mashabiki kwamba refa alikosea na kwamba ametunyima haki yetu, tunawafumba wasione mambo mengine muhimu na kubakia na ndoto kuwa kama Tanzania ingepata penati ingeshinda mechi ile iliyotaliwa na Wamorocco sehemu kubwa.

STAR 05

Tunapotoa tuhuma kwamba refa aliamua kuwabeba Wamorocco tunajidanganya ili kujipa furaha ya bandia. Kama kweli refa aliamua kuibeba Morocco, angeweza kufanya mengi ya kuidhoofisha timu, n ahata kutopuliza filimbi pale Morocco ilipokuwa inaotea.

Kilicho wazi ni kwamba Tanzania ilijitahidi, hasa nidhamu ya mbinu waliyokuwa nayo wachezaji katika kujilinda na kwenda mbele kwa kasi pale wanaponyang’anya mpira.

Mbali na wachezaji, kocha Miguel Gamondi ameonyesha kuwa anaweza kuwa dawa ya timu yetu kutofanya vizuri kwenye fainali za AFCON baada ya kuibadili timu kwa kiwango kikubwa licha ya kupewa majukumu dakika za mwisho.

Haya hivyo, ni lazima tukubali kuwa Morocco wametuzidi sana na tulichokifanya kwa usahihi ni kuwazuia wasitoke na mabao mengi.

JIC 03

Ni vizuri wale wenye ushawishi kujifunza kuangalia mambo kutokea sehemu tofauti na si kujaribu kuwaaminisha watu kuwa kosa moja liliikosesha timu ushindi. Na tunapozungumzia makossa ya uamuzi ni muhimu kuwapa wataalamu, kama hao waamuzi wa zamani, muda waeleze vizuri tukio na mazingira ambayo refa alifanya uamuzi na tafsiri ya tukio hilo pekee badala ya kusoma sheria inasemaje na kuweka msimamo kwamba ni kosa au si kosa.

Kwa kufanya hivyo tutawawezesha mashabiki wetu kuelewa sheria kwa mapana na marefu yake na hivyo kujikita zaidi katika kuangalia mchezo kuliko kusubiri kupumbazwa na uchambuzi.

Huu ni utamaduni tuliouzoea hapa kwetu, lakini haufai kuhamishiwa huko kwenye teknolojia ya hali ya juu na watu waliobobea kutafsiri matukio.