Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ni Gamondi AFCON 2027 au wazawa?

ZENGWE Pict


KAMA ni kuzungumzia ushiriki wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, maelezo yanaweza kuwa hadi sasa kuna mafanikio makubwa baada ya pointi mbili ilizovuna kupitia mechi tatu kuiwezesha kuandika historia ya kufika hatua ya mtoano.


Pengine pointi mbili zaweza kuonekana ni dhihaka, lakini fainali za mwaka huu zimeonekana kuwa ni ngumu kuliko nyingine nyingi na ndio maana washindi wa tatu bora wamegombana kwenye pointi tatu na mbili, huku Nigeria na Algeria ikiwa timu pekee iliyovuna pointi zote tisa katika hatua ya makundi.


Nilikuwa naandaa safu hii nikijua jioni Taifa Stars ilikuwa na kibarua kigumu mbele ya wenyeji, Morocco katika mechi ya hatua ya 16 bora.

Hatuwezi kusema huo ndio mwisho wa safari kwa kuangalia ubora wa Morocco kwa kuwa haya ni mashindano na timu yoyote iliyofuzu na kufika hatua hiyo inachukuliwa kuwa inaweza kufika hadi fainali na ikiwezekana kutwaa ubingwa.

ZENG 01

Taifa Stars ilikuwa imefunga mabao matatu (kabla ya leo) kwenye fainali za mwaka huu na ilikuwa ikipambania kutikisa nyavu za Wamorocco kupata bao muhimu katika harakati za kutaka kuandika historia zaidi.

Stars pia ilikuwa imeruhusu mabao manne kabla ya jana baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Nigeria na baadaye kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uganda na Tunisia, ambayo hivi sasa imeshatolewa na Mali katika hatua ya 16 bora. Uganda haikuvuka makundi.

Kwa hiyo takwimu zimeibeba Stars na kuipa nguvu wakati ikiikabili Morocco.

ZENG 02

Sehemu ya mafanikio hayo imechagizwa na kocha Muargentina, Miguel Gamondi, ambaye amepewa kikosi hicho kwa muda wa mpito akitokea klabu ya Singida Black Stars inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC.

Gamondi anajulikana kwa soka lake la kumiliki mpira na kukabia juu kun akosababisha mabeki wa timu pinzani kutokuwa na uhuru kamili wa kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma. Gamondi pia anasifika kwa kujenga uhusiano mzuri na wachezaji uliosababisha aonekane kama anawadekeza wakati alipokuwa kocha mkuu wa klabu ya Yanga.

ZENG 03

Nilimsikiliza kocha msaidizi wa zamani wa Stars, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akizungumzia mabadiliko ya timu baada ya Gamondi kuteuliwa, akisema kuwa anachokiona kimebadilika ni ari au hamasa. Kujenga hiyo ari au hamasa ni talanta pia ambayo kocha anastahili kuwa nayo.

Na Gamondi amejaliwa hilo kiasi kwamba wakati mwingine huonekana kama anafanya mambo ya kitoto, kumbe ni kujaribu kuwasogeza karibu wachezaji wake wajiamini na kuweka akili tayari kupokea maelekezo yake.

ZENG 04

Niliwahi kusikia viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakisema sera yao kwa sasa ni kuwapa nafasi makocha wazawa. Jibu hilo lilitolewa baada ya kocha Muargeria Adel Amrouche kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kulituhumu linaipendelea Morocco, nchi yenye uhasama wa kisiasa na jirani zao wa Algeria.

Wakati huo Stars ikiwa chini ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ na wasaidizi wake Juma Mgunda na Kihwelo, ilikuwa ikifanya vizuri, ikirekodi ushindi muhimu wa ugenini dhidi ya Zambia na huku ikifuzu kucheza fainali hizi za AFCON.

ZENG 05

Jibu hilo lisingeweza kumfanya mwandishi aliyeuliza swali hilo, aendelee kuhoji kwa kuwa takwimu ziliwabeba makocha wazawa. Lakini matokeo mfululizo ya mechi zilizofuata yalitikisa sera hiyo.

Nikikumbuka jibu hilo la sera ya kuwapa nafasi makocha wazawa na kuangalia mwenendo wa sasa wa Taifa Stars, makubaliano na Gamondi na fainali  zijazo za AFCON 2027 zitakazoandaliwa na Tanzania, Kenya na Uganda, Napata wasiwasi kwa benchi la ufundi kama litakuwa limeshapata kocha mwingine, au Gamondi ataendelea au litakuwa chini ya wazawa kama sera ya shirikisho.

Kwangu naona maandalizi ya AFCON 2027 yalitakiwa yawe na nafasi kwenye fainali hizi zinazoendelea Morocco. Kwamba tulitakiwa tuwe tunajaribu baadhi ya malengo tuliyojiwekea wakati tunashiriki fainali hizi.

Kwamba tulishaamua benchi la ufundi liweje na hivyo kulipima katika fainali hizi kwamba liendelee au lirekebishwe wapi kiasi kwamba AFCON 2027 inapofika tunakuwa tumejaribu vipimo vingi na hivyo kuingia na uhakika wa nini tunaenda kufanya.

Tayari kelele zimeshaanza kwamba Gamondi apewe mkataba wa kudumu baada ya kuona uchezaji wa Taifa Stars umebadilika.

Kocha huyo bado ana mkataba na Singida BS na haitakuwa sahihi kuwa anafanya kazi ya kibarua Taifa Stars, huku akiendelea na ajira Singida BS.

ZENG 06

Tutaonekana hatuko makini na taifa letu. Ni muhimu hatima ya benchi la ufundi la Stars ikajulikana mapema ili kocha aanze kujishughulisha na timu muda wote kuanzia sasa, akifuatilia maendeleo ya wachezaji wetu kote duniani, akiwasilisha mahitaji yake, akifanya vikao na wasaidizi wake kuwaelewesha falsa yake na mambo mengine muhimu.

Kwa kuwa Stars hukutana pale inapokuwa na mechi, yaani siku takriban tano kabla ya kutawnyika, huwa inaonekana kama kocha wa klabu anaweza pia kufundisha timu ya taifa. Lakini kocha wa taifa anahitaji zaidi ya hizo siku tano kuwaelewa zaidi wachezaji wake, benchi lake na mambo mengine muhimu.

Tumeshavuka 2025 na hivyo tuna mwaka mmoja tu kabla ya fainali za AFCON 2027 na bado hatuna benchi rasmi la ufundi.

Ni wakati wa kufanya maamuzi sasa ili huko mbele tusilaumiane kwa mambo ya nje ya uwanja, bali tukubali uhalisia iwapo hatutafanya vizuri.