Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kumsifu Bacca si unazi wa Kariakoo

ZENGWE Pict


HADI sasa ngome ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeruhusu mabao matatu baada ya kucheza mechi mbili za makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, ikiwamo mechi ya vigogo wa soka wa Afrika, Nigeria.


Na si Nigeria tu, bali timu iliyo na mmoja wa washambuliaji wakali barani Afrika kwa sasa, Victor Osimhen anayechezea klabu ya Galatasaray ya Uturuki.


Mshambuliaji huyo ambaye hadi sasa amefunga bao moja na kutengeneza moja, hakuweza kuziona nyavu za Tanzania katika mechi ya kwanza ya Kundi C ambapo Nigeria iliibuka na ushindi wa 2-1 kabla ya kuishinda Tunisia kwa mabao 3-2 na kukata tiketi ya hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.

Katika mechi hiyo ya pili, Osimhen ndiye alifunga bao la kwanza kwa kichwa na baadaye kutengeneza la tatu alipomburuzia mpiraAdemola Lookman aliyefunga bao hilo muhimu kwa taifa hilo ambalo linahaha kurejesha heshima yake baada ya kushindwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani.

Kushindwa kuziona nyavu za Tanzania na hata kutengeneza bao kumesababisha baadhi ya Watanzania kummwagia sifa beki wa Yanga, Ibrahim Hamad 'Bacca' kwa jinsi alivyotekeleza vizuri jukumu la kumlinda mshambuliaji huyo mrefu, lakini mnyumbufu na anayehangaika wakati wote uwanjani kutafuta bao.

ZENG 01

Bacca, ambaye kwa kawaida hucheza beki wa kati akitumwa kutibua mipira ili beki wa mwisho awe na kazi nyepesi ya kufagia, alihakikisha Osimhen hafanyi uamuzi kwa uhakika, akimsumbua kila wakati alipokuwa na mpira au akitafuta nafasi au wakati wa kona na mipira ya adhabu.

Hali hiyo pia ilisababisha wanamtandao kuvuma mtandaoni video fupi nyingi zinazoonyesha jinsi kulivyokuwa na mpambano mkali baina ya wawili hao wanaokaribia kulingana kwa kimo.

Osimhen alifanikiwa kupiga mipira kadhaa kuelekea golini lakini haikuwa na uhakika na mmoja ambao ulionekana kama unaelekea golini ulifagiliwa na Bakari Mwamnyeto kabla ya kuvuka mstari.

ZENG 02

Lakini kundi jingine limekuwa likiponda wale wanaopongeza kazi ya Bacca kwa madai kuwa wanaomsifia wanafanya hivyo kwa sababu ni mashabiki na wanazi wa klabu yake ya Yanga. Wanadai kuwa aliyestahili sifa ni Mwamnyeto kwa kucheza vizuri kama beki wa mwisho, akishika nafasi ya Dickson Job, ambaye alianzia benchini siku ya mechi hiyo.

Wanadai mipira saba aliyopiga golini inaonyesha kuwa Bacca hakuweza kumdhibiti ipasavyo Osimhen na hivyo apongezwe Mwamnyeto aliyeokoa bao la wazi baada ya Mnigeria huyo kupiga mpira golini ambako hakukuwa na mtu.

Mjadala huo bado unaendelea mtandaoni na unaendelezwa na watu wanaowatuhumu wengine kuwa wanasifia kinazi, lakini ukiangalia uhalisia wale wanaoponda ndio wanazi kuliko wanaosifia.

ZENG 03

Mmoja alijaribu kusema kuwa Bacca na Mwamnyeto walichoka mechi ya pili hivyo angeingia Nangu na wachezaji wengine wa Simba baada ya kocha Gamondi kupanga kikosi ambacho hakikuwa na hata mchezaji mmoja wa Simba katika mechi ya pili dhidi ya Uganda iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

Ni lazima Watanzania waanze kujua umuhimu wa kupenda chao linapofikia suala la utaifa. Kuchambua timu kwa jicho la unazi ni mambo ya kijinga ambayo hayastahili kuendelezwa katika zama hizi.

Udhaifu, kasoro au ubora wa mchezaji wa timu ya taifa hauhusiani na klabu anayotoka bali ni mambo binafsi ambayo yanaweza kusababishwa na mfumo wa timu ya taifa, mbinu tofauti na anazotumia kocha wa timu ya taifa au majukumu anayompa mchezaji.

Hakuna ubishi kwamba kwa kiasi kikubwa Bacca ndiye aliyesababisha Osimhen asitambe kama alivyozoea. Hakuweza kutumia vizuri urefu wake, hakuweza kufanya maamuzi mengi sahihi, hakuweza kupata nafasi ya wazi kutekeleza kile alichokusudia.

Badala yake alifanya kazi katika mazingira magumu yaliyomfanya hata lile shuti moja alilopiga wakati goli likiwa halina kipa, lisipigwe kwa usahihi kuipa Nigeria ushindi mnono.

ZENG 04

Katika mechi ambayo hakupata ulinzi mkali wa mtu-na-mtu dhidi ya Tunisia, Osimhen alifanya yale aliyozoea. Aliruka juu kwa uhuru kabisa kufunga bao la kwanza na baadaye akatoa pasi ya goli kwa utulivu. Hakukutana na ghasia za Bacca.

Na kuonyesha kuwa alikutana na ghasia nyingi siku ya mechi na Stars, Osimhen, ambaye alibadilishwa dakika za mwisho, alienda kumkumbatia Bacca mwishoni mwa mchezo kuonyesha kuwa anakubali kazi yake.

Sasa ni nani anayeona Bacca hakustahili sifa kwa kumdhibiti Osimhen? Jibu ni “wanazi fulani wasiojielewa”.

Pengine wako wanaosubiri Bacca aboronge mechi zinazofuata ili wapate hoja kuwa walishasema kuwa hakustahili sifa kwa kumdhibiti Osimhen. Hao jibu lao ni fupi tu; Bacca anastahili sifa kwa alichofanya hadi sasa. Akiboronga mechi nyingine hakutakuwa na uhusiano na kumdhibiti Osimhen.

Tuache unazi wakati timu ya taifa ikiwa mashindanoni. Mashindano yanayoshirikisha timu za taifa ni vita na wakati wa vita taifa huwa moja hadi iishe.

Kwa vita hii ya AFCON 2025 nchini Morocco, Tanzania ni moja. Hatutakiwi kugawanyika kwa sababu ya unazi wa klabu mbili za Kariakoo.

Kumsifu mchezaji wa Taifa Stars sio unazi.