Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunaua Ligi ya U-20 kwa ajili ya wasotea benchi?

ZENGWE Pict


HAMU ya kupata mafanikio ya haraka imesababisha watu wengi kutumia njia za mkato, njia ovu na za kihalifu kuwezesha hilo kufanyika. Hawataki njia sahihi za kutafuta mafanikio kwa kuwekeza vizuri kwa muda mrefu ili kupata kilicho bora.


Tabia hiyo imesababisha mashindano ya umri mdogo barani Afrika kukumbana na changamoto nyingi na kutokuwa na matunda mazuri au kutovutia hata mashabiki wa soka na kutokuwa na maana.


Tatizo kubwa linalosababisha klabu za soka kulazimika kudanganya umri wa wachezaji ni kwanza mafanikio ya njia za mkato, mawakala kutaka wachezaji walio chini yao kuonekana wana umri mdogo na kutokuwapo kwa rekodi sahihi za raia kuanzia wanapozaliwa hadi wanapoamua kutumia mpira wa miguu kama chanzo cha kipato kimaisha.

Pamoja na nchi ya Shelisheli kutotamba katika soka la Afrika, imeweza kudhibiti udanganyifu wa umri kwa kuwa kitambulisho cha mtoto huanzia pale anapozaliwa na namba yake ndio anaitumia maisha yake yote katika kitambulisho na nyaraka nyingine.

Mtu kama huyo ambaye hakuwahi kufikiria atafanya nini maishani, hawezi kudanganya umri kwa kuwa tayari taarifa zake zote zipo kwenye benki ya taarifa ya nchi.

ZENG 01

Lakini kwetu kijana anaweza kufikisha hadi miaka 18 asiwe na cheti cha kuzaliwa, huku akijaribu kusaka mafanikio kwa kutumia mpira wa miguu. Kunapotokea nafasi kwa timu za umri na kijana huyo anakuwa ameshavuka umri, sarakasi huchezwa kubadili umri wake na hata kumpatia cheti cha kuzaliwa ili afuzu kuchezea timu ya vijana wadogo.

Huku ni kujidanganya ambako hakusaidii mpira wetu kukua. Tumeona timu yetu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 ikiondolewa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kugundulika kuwa Nurdin Bakari aliandikisha umri mkubwa zaidi katika orodha ya wachezaji wa Simba tofauti na ile timu ya vijana.

Mataifa mengine kama Nigeria, Ghana na Cameroon yamekumbana na kadhia hiyo kwa timu zao za vijana kuondolewa mashindanoni baada ya kugundulika kuwa idadi kubwa ya wachezaji walighushi umri.

Hili si tatizo linaloweza kuondolewa kwa viboko au sheria kali, bali kwa kubuni mbinu za kulazimisha klabu kutumia wachezaji wenye umri sahihi na kutokuwa dhaifu katika kusimamia suala hilo. Na zipo njia nyingi, ikiwamo ya kulazimisha klabu kuwa na shule za watoto badala ya kuanzia na mashindano ya vijana walio na umri chini ya miaka 17 au 20.

Nimemsikia rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akisema wana mpango wa kuachana na mashindano ya vijana walio na umri wa miaka 20 na kuelekeza nguvu kwenye mashindano ya timu za wachezaji wa akiba (reserve teams).

Alisema sababu ya kufikia uamuzi huo ni kwamba shirikisho lake limeshindwa kudhibiti tatizo la kughushi umri kwenye mashindano hayo ya vijana na hivyo limeamua kwamba mashindano hayo yatakuwa ya wachezaji wasiopata nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya klabu zao.

Kwanza ni uamuzi ambao ulitakiwa ufanywe na Bodi ya Ligi kwa kuwa ndiyo inayoshughulika na mashindano ya wachezaji waliokwishapita ngazi ya ligi za maendeleo (development leagues) na sasa wako kwenye mashindano tu au waliokwishapikika (ready made players).

Hivyo, kama kuna wachezaji kwenye klabu za Ligi Kuu ambao hawapati nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya klabu zao, hilo si suala la chama cha soka au shirikisho la soka la nchi, bali taasisi inayoongoza mashindano ya wachezaji waliovuka ngazi ya maendeleo.

Shirikisho linatakiwa lijikite zaidi na mashindano ya umri kwa kuwa huko ndiko kuna wachezaji wa kesho na hivyo wanahitaji mafunzo sahihi ili watakapokabidhiwa majukumu wawe wamepikika ipasavyo.

Kwa maana hiyo, TFF kutoa kauli kwamba inaachana na mashindano ya vijana ni kukwepa wajibu wake wa kuendeleza soka kutokana na kushindwa kudhibiti ubabaishaji wa viongozi wa klabu katika suala la umri wa wachezaji.

Nilidhani TFF ingeibuka na mkakati unaoonyesha kuwa imedhamiria kupambana na tatizo la kughushi umri ili kuyalinda mashindano ya vijana na kuzuia wenye umri mkubwa kukandamiza wachezaji wadogo.

ZENG 02

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) liliibuka na mkakati kama huo mwaka 2009 ilipoamua kutumia kipimo cha Magnetic Resonance Imaging (MRI) kudhibiti wachezaji wa mashindano ya umri wa chini ya miaka 17. Kipimo hicho kinaweza kupima ukomavu wa mifupa ya binadamu mwenye umri chini ya miaka 17.

Sitaki kueleweka kwamba nahimiza TFF itafute teknolojia ya kudhibiti wenye umri chini ya miaka 20, bali itafute mbinu ya kujikita zaidi kwenye umri mdogo ili baada ya muda fulani iwe ngumu kumuona mchezaji anayeibuka akiwa na umri wa miaka 23 halafu atake kucheza timu ya U17.

Ukianza na wachezaji wenye umri chini ya miaka 12 katika klabu zote za Ligi Kuu na Championship, utakuwa umezalisha kundi kubwa la wachezaji ambao itakuwa rahisi kuwabaini kadri umri unavyoongezeka.

Tuliocheza shuleni ilikuwa rahisi kujua mchezaji fulani alichezea timu ya mkoa fulani au kanda fulani na hivyo kujulikana umri wake hauwezi kuzidi miaka fulani baada ya muda.

Kama tuliweza kudhibiti elimu ya watu waliokuwa wakigombea uongozi wa mpira wa miguu kwa kushirikiana na taasisi zinazotoa vyeti, kuna tatizo gani kwa TFF kushirikiana na mamlaka ya vizazi na vifo kuchunguza vyeti vya kughushi vinavyotumiwa na wachezaji wenye umri mkubwa?

ZENG 03

Kupambana na tatizo la kughushi inawezekana kabisa kama viongozi wa mpira wa miguu watakuna vichwa kuangalia wanafanikishaje majukumu ya msingi ya chama cha soka au shirikisho la soka la nchi.

Kama mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 yamepotea na haya ya U20 yakiondolewa, TFF itabakia na majukumu gani ya maendeleo? Kusimamia Ligi Kuu? Kwa kuwa hata mafunzo ya makocha yanatolewa kuanzia ngazi za wilaya isipokuwa yale ya ngazi za juu.

Badala ya kukuna vichwa kufikiria wachezaji wanaokosa namba kwenye vikosi vya kwanza vya klabu za Ligi Kuu, TFF ifikirie itawezaje kuendesha mashindano muhimu ya umri ili kutengeneza kizazi kijacho cha wachezaji mahiri.