Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tunaitarajia Taifa Stars ya kina Stoichkov Morocco

ZENGWE Pict


TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kwa mara ya nne, inatarajiwa kushuka uwanjani kwa mechi ya kwanza ya Kundi C kesho Jumanne dhidi ya Nigeria katika mechi itakayopigwa mjini Fez, Kaskazini mwa Morocco.


Hilo litakuwa jaribio jingine kwa Tanzania kutafuta ushindi wa kwanza kwenye fainali hizo kubwa za soka barani Afrika baada ya majaribio yake matatu ya fainali za 1980, 2019 na 2023 kutozaa matunda zaidi ya kuambulia sare.


Ushindi wowote dhidi ya Nigeria, Tunisia na Uganda ambazo ziko kundi moja na Stars katika fainali hizo utakuwa ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na kuvuka hatua ya makundi itakuwa ni historia.

Mwenendo wa Tanzania katika mechi tatu zilizopita haukuwa mzuri na umezidisha hali ya timu hiyo kupoteza mvuto kwa mashabiki wa Tanzania ambao wana wendawazimu wa mpira wa miguu. Kwa hiyo kuendelea kutofanya vizuri kutakuwa chukizo zaidi kwa mashabiki hao ambao walionyesha mapenzi makubwa kwa Taifa Stars mwanzoni mwa milenia hii.

Kwa hiyo deni kubwa kwa wachezaji wa Tanzania itakuwa ni kuhakikisha inafanya vizuri kwenye fainali hizo ili kurudisha mapenzi ya timu kwa mashabiki.

ZENG 01
ZENG 01

Ndio, Taifa Stars haikuondoka kama kikosi kilichotumwa na nchi kutafuta mafanikio baada ya timu kusafirishwa kwenda kuweka kambi Misri bila ya kuagwa kama mashujaa na kupewa bendera kama alama ya kubebeshwa dhamana na taifa, lakini kupambana pekee na kupata mafanikio ndiko kutalipa yote hayo.

Mwaka 1994, Bulgaria ikiwa na kikosi cha dhahabu kilichosheheni wachezaji nyota kama Hristo Stoichkov, Emil Konstadinov, Krassmir Balakov na Yordan Lechtkov, ilikwenda fainali za Kombe la Dunia bila ya shangwe, huku vyombo vya habari vya nchi hiyo vikiwa haviipi timu umuhimu.

Lakini ilishangaza katika fainali hizo. Ilianza kupata matokeo mazuri katika hatua za makundi na bila kutarajiwa ilivuka hatua hiyo hadi robo fainali ilipoiondoa Ujerumani kabla ya kufungwa na Italia katika nusu fainali.

Timu hiyo ilimaliza fainali hizo ikiwa na wachezaji waliopachikwa jina la ‘kizazi cha dhahabu’ huku Stoichkov akitikisa nyavu mara sita, hivyo kuwa mmoja wa wachezaji wawili waliotwaa Kiatu cha Dhahabu.

ZENG 02

Kutoka hapo, vyombo vya habari vikaanza kuimba nyimbo za timu yao ya taifa, huku kocha Dimitar Penev akipewa heshima ya ushujaa.

Si kwamba vyombo vya habari vilikusudia kuisusia timu hiyo, la hasha. Hilo lilitokea kwa sababu ya siasa za wakati za nchi hiyo iliyokuwa ya kijamaa hivyo kutoangalia sana mambo yake ya ndani ya kimichezo na kutangaza zaidi habari za timu za nje.

Hivyo mafanikio ya uwanjani yanaweza kubadili mioyo ya mashabiki wa Tanzania ambao kwa sasa ili Uwanja wa Benjamin Mkapa ujae wakati Taifa Stars ikicheza, ni lazima waambiwe wataingia bure.

ZENG 03

Kocha Muargentina, Miguel Gamondi, anayefundisha klabu ya Singida Black Stars ndio amepewa jukumu hilo la kuongoza kikosi cha Tanzania kwenye fainali hizo.

Gamondi alijijengea sifa nchini kwa kutengeneza kikosi imara cha Yanga kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu na kuifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Pamoja na kwamba kwa muda mrefu amekuwa katika soka la ngazi ya klabu ambako walimu hupata muda mrefu wa kuwasoma wachezaji na kutengeneza timu ya ushindi, muda wa takriban wiki mbili utamtosha kujenga kikosi kitakachorejesha hamasa kwa mashabiki na kulipa taifa heshima.

Gamondi anajulikana kwa mtindo wake wa kutotoa nafasi kwa timu pinzani kuchezea mpira kwa utulivu na hasa wanapoanza kujenga mashambulizi kwenye ngome. Anajulikana kwa mchezo wake wa pasi nyingi na kupenda kutumia viungo wenye pasi cha kuchana ngome.

ZENG 04

Mechi ya kwanza anakutana na Nigeria, timu iliyojaa wachezaji nyota wanaosakata soka katika ligi kubwa Ulaya kama Ademola Lookman anayechezea Atalanta ya Italia, Samuel Chukwueze (Fulham, England), Chidera Ejuke, Akor Adams (Sevilla, Hispania) na bila kumsahau mshambuliaji hatari kwa sasa barani Afrika, Victor Osimhen anayechezea Galatasaray ya Uturuki.

Nigeria haijawa katika kiwango chake bora kilichoifanya iitetemeshe dunia na inaingia fainali hizo ikiwa na kumbukumbu mbaya baada ya kutolewa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mechi za mtoano za kutafuta tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Kwa maana hiyo itazichukulia fainali hizo kwa uzito mkubwa, tofauti na ilivyokuwa ikicheza katika hatua za awali za Kombe la Dunia ambako ilipelekwa puta hata na Rwanda.

Tunisia ni timu ambayo inaweza kufananishwa na Simba aliyelala baada ya kupotea kwenye orodha ya timu zinazotwaa ubingwa wa mashindano mbalimbali ya Afrika.

ZENG 05

Ukweli kwamba nchi hiyo ina program nzuri za maendeleo ya soka, inaifanya iweze kujenga kikosi imara kutoka klabu zake kubwa kama Esperence, Etoile Sportive du Sahel, Club Africain na CS Sfaxien, ambazo zinafanya vizuri katika mashindano ya klabu ya Afrika.

Mbali na wachezaji waliokuzwa nyumbani, Tunisia imebeba nyota wanaosakata soka Ulaya na Misri kama Ellyes Skhiri anayechezea Eintracht Frankfurt ya Ujerumani, Ismael Gharbi (Augsburg, Ujerumani), Ali Ben Romdhane (Al Ahli, Misri), Hannibal Mejbri (Burnley, England), Elias Saad (Augusburg, Ujerumani Elias Achouri (FC Copenhagen), Sebastian Tounekt (Celtic, Scotland) na  Seifdine Jaziri anayechezea Zamalek ya Misri.

Mchanganyiko huo wa nyota wanaosakata soka Tunisia na nje ya nchi hiyo kunaifanya Tunisia kuwa kikwazo kingine kwa Taifa Stars kuondokana na balaa la kutopata ushindi.

Timu nyingine kwenye kundi hilo ni Uganda ambayo tumekuwa na matokeo tofauti tunapokutana nayo. Inaweza kuwa kipigo sare au ushindi, lakini hilo haliwezi kutupa matumaini moja kwa moja kuwa tunaweza kuokota ushindi kirahisi kwa kuwa fainali hizo ni tofauti na mashindano ya kufuzu.

Pamoja na ugumu wa kundi letu, bado Stars inaweza ikafanya vizuri kwa sababu unapokutana na mambo magumu ndipo unaongeza juhudi za kupambana nayo ili uyashinde. Na ndivyo tunavyotegemea vijana wetu wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha mambo magumu yanageuzwa kuwa fursa na hiyo kuwa wawakilishi wazuri.

Tunatarajia moyo wa kina Stoichkov, Kostadinov, Balakov na Leichtkov utaingia mioyoni mwa kina Mbwana Samatta, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Morice Abraham, Dickson Job, Shomari Kapombe, Simon Msuva na wengine na kucheza kishujaa kuipeperusha bendera ya Taifa vizuri.

Kila la heri kwa wachezaji na timu nzima.