Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tufungue mipaka Kombe la Muungano

PUMZI Pict


KWA mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ligi hiyo itasimama kati ya Aprili 21 na 29 mwaka huu kwa ajili ya Kombe la Muungano 2026.


Mashindano hayo maalumu ya kuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mwaka huu unatimiza miaka 62, yatafanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.


Huu utakuwa msimu wa tatu tangu yalipoanza kwa sura mpya mwaka 2024 na Simba ilibeba ubingwa, kisha 2025 ikawa zamu ya Yanga.

Kombe la Muungano ni mashindano yaliyoanzishwa maalumu kuuenzi Muungano wetu na kurudisha kumbukumbu nzuri ya Ligi Kuu ya Muungano iliyofanyika kuanzia 1982 hadi 2003.

Hata kabla ya Ligi ya Muungano, timu za Bara na Zanzibar zilicheza pamoja kutafuta bingwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia 1972 na aliyepatikana ndio alikuwa mfalme wa soka wa Tanzania anayetambuliwa na mamlaka zote za mpira duniani, kuanzia CAF hadi FIFA.

PUM 01

MWAKA HUU

Timu nne za Bara na nne za Zanzibar zitashiriki katika mtindo wa mtoano, hadi fainali. Mashindano haya ni muhimu sana kwa kujenga umoja wetu wa kitaifa sisi kama Watanzania, lakini hata hivyo, tunaweza kufanya zaidi ya hapo na kupata kitu kizuri zaidi na endelevu.

Badala ya kuwa na mashindano ya bonanza kama hayo, tuwe na mfumo rasmi utakaofanya kuwe na mashindano yatakayoshirikisha timu za Tanzania nzima (Bara na Visiwani) yatakayotoa nafasi za ushiriki wa mashindano ya Afrika.

PUM 02

TUFUNGUE MIPAKA

Sisi kama taifa bado tunakumbatia mifumo ya kikoloni inayotutenganisha. Hakuna ligi moja inayoweza kutufanya Watanzania tukacheza pamoja.

Mwaka 2000 kwenye kilele cha UMITASHUMTA pale Morogoro, Rais wa Jamhuri ya Muungano (awamu ya tatu) Benjamin William Mkapa (marehemu) ambaye alikuwa mgeni rasmi siku hiyo, alitoa wito kwa waandaaji wa michezo ile kuhakikisha inakuwa na sura ya Muungano ili watoto wetu wacheze pamoja.

Bahati mbaya ni mwaka mmoja baadaye, yaani 2001 UMITASHUMTA (pamoja na UMIISETA) ikasimama kabisa, hadi 2006 wakati Mkapa mwenyewe alipotoka madarakani.

PUM 04

Hata iliporudi wakati wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, haikuwa na sura ile aliyoitaka Mkapa. Na Hiki ndicho ninachokijadili hapa.

Tuwe na ligi moja itakayoshirikisha timu za Bara na Visiwani kama ilivyokuwa Ligi ya Muungano iliyoanza 1982 na kufa 2003.

Siyo lazima kuunganisha ligi zilizopo, hapana. Hizi ligi zinaweza kuendelea kama zilivyo lakini ziondoe ile kanuni ya hovyo inayokataza timu za upande mmoja kushiriki ligi ya upande mwingine.

Ligi iwe wazi kwa timu zinazotaka kutoka upande wowote kujisajili upande mwingine na kushiriki.

Hivi ndivyo wanavyofanya wenzetu kama England ambapo timu za kutoka Wales; Cardiff City na Swansea City, zinashiriki EPL.

Walichofanya wenzetu ni kuweka milango wazi kwa timu kujisajili inakotaka na kufuata michakato yote inayotakiwa ikiwemo kuanzia madaraja ya chini.

Yaani Cardiff City na Swansea City, zilisajiliwa England na FA na zikaanzia ligi ya chini kabisa hadi zilipo sasa.

Hii ina maana Mlandege ya Zanzibar inaweza kujisajili bara na kuanzia Ligi Daraja la Nne hadi ifike ligi kuu na kushiriki.

Au Singida Black Stars ya Bara inaweza kwenda kujisajili ZFF na kuanzia Ligi Daraja la Nne hadi kufika Ligi Kuu ya Zanzibar.

Zanzibar na Bara ni Tanzania moja, kama Wales na England ambazo ni UK moja.

Lakini ukiacha nchi kama hizi zenye historia ya udugu, kuna zingine ambazo hazina uhusiano kama huu ila zinafanya hivyo.

PUM 03

Ujerumani inaruhusu timu za kutoka kwa majirani zake Austria na Poland kushiriki ligi yao. Japo hazijapanda ligi kuu lakini kuna timu kadhaa kutoka nchi hizo mbili zinazoshiriki kwenye ligi za Ujerumani za madaraja tofauti.

Tanzania tumemuuza kijana wetu Cyprian Kachwele kwenda Canada kwenye timu ya Vancouver White Caps.

Timu hii japo ni ya Canada lakini inashiriki Ligi ya Marekani, MLS.

Siyo kwamba Canada hakuna ligi, la hasha. Ni kwamba Marekani imefungua mipaka kwa majirani zake kushiriki ligi yao.

Kama majirani tu wanaweza, sisi ndugu tunashindwa nini?

Hivi karibu kulikuwa na mjadala mkubwa kufuatia taarifa za Simba kuomba kutumia Uwanja wa New Amaan Complex kama uwanja wao wa nyumbani baada ya kufungwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao ndiyo ulikuwa uwanja wao wa nyumbani.

Hapo hapo zikaanza kunukuliwa kanuni kadhaa zinazokataza timu za bara kutumia viwanja visivyo vya bara kwenye ligi kuu.

Kama tunataka kuutumia mpira kutuunganisha kama taifa, tusiishie kwenye mabonanza kama Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano, tuwe na mashindano rasmi yatakayoubeba Muungano mgongoni na kuunganisha Watanzania.