TONGE MDOMONI: Mastaa waliokaribia kusaini kisha wakanaswa kwingine
Muktasari:
- Spurs ilidhani imeshafanikiwa kunasa saini ya kiungo huyo mchezeshaji wa Crystal Palace baada ya wiki kadhaa za mazungumzo.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imeiacha Tottenham Hotspur kwenye mataa ikishangaa baada ya kuifanyia umafia kwenye usajili wa Eberechi Eze.
Spurs ilidhani imeshafanikiwa kunasa saini ya kiungo huyo mchezeshaji wa Crystal Palace baada ya wiki kadhaa za mazungumzo.
Lakini, Arsenal ilifanya umafia Jumatano iliyopita baada ya kuumia kwa Kai Havertz, ambapo kwa sasa Eze atakuwa staa mpya wa Emirates kwa dili la Pauni 68 milioni.
Na sasa, Spurs imeachwa solemba ikipambania huduma za wachezaji wengine akiwamo winga wa Manchester City, Savinho.
Hata hivyo, hiyo siyo mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu England timu moja kuifanyia umafia nyingine kwa kupora mchezaji katika dakika za mwisho.
Aaron Ramsey
Cardiff kwenda Arsenal, 2008
Klabu iliyoporwa: Man United
Aaron Ramsey alikwenda kuwa staa mkubwa kwa miaka 11 aliyokuwa Arsenal akicheza mechi 369 baada ya kutua hapo mwaka 2008 akitokea Cardiff kwa ada isiyozidi Pauni 5 milioni.
Lakini, kiungo huyo alikaribia kabisa kutua Manchester United. Akiwa na umri wa miaka 17, Ramsey alifanya balaa huko Wales na kuzivutia timu nyingi, huku Man United ikitangaza kwamba imefikia makubaliano na Cardiff ya kumnasa mchezaji huyo.
Lakini, kocha Arsene Wenger aliingilia kati na kumbadili akili Ramsey dakika za mwisho akatua Emirates.
Moises Caicedo
Brighton kwenda Chelsea, 2023
Klabu iliyoporwa: Liverpool
Kiungo Caicedo kwa sasa anahesabika kama moja ya usajili bora kabisa huko Chelsea, lakini mkali huyo alikaribia kabisa kujiunga na Liverpool kabla ya kubadili mawazo na kutua Stamford Bridge.
Chelsea ndiyo iliyoanza kuonyesha dhamira ya kumchukua Caicedo kabla ya Liverpool kuvamia dili na kuweka ubaoni ofa ya Pauni 110 milioni huko Brighton.
Liverpool ilithibitisha kwamba Caicedo ataenda Anfield, kabla ya Chelsea kupindua meza dakika za mwisho kwa kuweka ubaoni ofa ya Pauni 115 milioni na kufanikiwa kumnasa kiungo huyo.
Willian
Anzhi Makhachkala kwenda Chelsea, 2013
Klabu iliyoporwa: Tottenham
Winga wa Kibrazili, Willian alikosa mechi chache sana kwa kipindi chake alichokuwa Chelsea, ambapo alitumika kwenye mechi 339 kwa misimu saba.
Alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, kitu ambacho kisingekuwa hivyo kama angetua Tottenham, ambako alikaribia kabisa kutua.
Spurs ilionekana kabisa kunasa saini ya Willian kutoka Anzhi ya Russia, ambapo Mbrazili huyo alifanya hadi vipimo vya afya kwa ajili ya kujiunga na Spurs. Lakini, simu moja tu ya Chelsea kwa wakala wake, ikabadili mambo, Willian akatua darajani.
Robinho
Real Madrid kwenda Man City, 2008
Klabu iliyoporwa: Chelsea
Kinda matata wa Kibrazili kwa wakati huo, Robinho alionekana kuwa kwenye ubora wa kufikia viwango vya juu huko Real Madrid.
Lakini, baada ya kukasirishwa na kushindwa kumsajili Cristiano Ronaldo mwaka 2008, Robinho alidhani anakwenda kujiunga na Chelsea, ambayo ilikuwa na uhakika wa kukamilisha dili hiyo na klabu ilianza kabisa kuuza jezi zenye jina la Robinho.
Lakini, jambo hilo la Chelsea liliwakera mabosi wa Real Madrid na kuamua kumuuza Robinho huko Manchester City dakika za mwisho kabisa kwa ada ya Pauni 32.5 milioni.
Roy Keane
Nottingham Forest kwenda Man United, 1993
Klabu iliyoporwa: Blackburn Rovers
Roy Keane anaendelea kuwa mmoja wa wachezaji mahiri kabisa waliopata kutokea kwenye historia ya Ligi Kuu England.
Alicheza mechi 480 kwa kipindi cha miaka 12 na nusu kwenye timu hiyo, akibeba mataji saba ya ligi na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya 1999, mwaka ambao Man United ilibeba mataji matatu.
Lakini, kiungo huyo alikaribia kabisa kucheza Blackburn Rovers, iliyokuwa chini ya kocha Kenny Dalglish, ambaye alikuwa shabiki mkubwa wa Keane.
Rovers ilikubali kulipa Pauni 4 milioni kumsajili Keane na kila kitu kilionekana kinakamilika kwamba Keane alionekana Ewood Park, kabla ya Sir Alex Ferguson kumpigia simu Keane kupindua meza na staa huyo akatua Man United.
Park Chu-Young
Monaco kwenda Arsenal, 2011
Klabu iliyoporwa: Lille
Staa huyo wa Korea Kusini hakuwa na mambo mengi Arsenal, alifunga mara moja tu katika mechi saba alizocheza chini ya kocha Arsene Wenger. Lakini, kocha huyo wa Arsenal alivuka vizingiti vingi wakati anamsajili kutoka Monaco.
Park alishuhudia klabu yake ya Monaco ikishuka daraja hadi Ligue 2, hivyo aliwaambia mabosi wa timu hiyo anataka kuhama. Klabu nyingine ya Ufaransa, Lille ilikubali kumchukua Park na alikwenda kupima afya kujiunga huko. Lakini, Park alitoweka hotelini na kuibukia kwenye vipimo vya afya Arsenal, akanaswa.
Cristiano Ronaldo
Juventus kwenda Man United, 2021
Klabu iliyoporwa: Man City
Baada ya kutamba kwenye awamu yake ya kwanza Old Trafford, Ronaldo alikuwa na matumaini ya kutamba kwenye awamu ya pili aliporejea Man United mwaka 2021.
Hata hivyo, wakati anaondoka Juventua, Ronaldo alikaribia kabisa kujiunga kwa mahasimu wa Man United, Manchester City.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola alihitaji saini ya Ronaldo na kufikia makubaliano ya mdomo na kwamba staa huyo wa Ureno alikuwa tayari kwenda kusaini mkataba Etihad.
Lakini, kocha wa zamani wa Man United, Sir Alex aliingilia kati, alimpigia simu mwenyewe Ronaldo na kumrudisha Theatre of Dreams.
Emmanuel Petit
Monaco kwenda Arsenal, 1997
Klabu iliyoporwa: Tottenham
Mashabiki wa Spurs tulieni, hii si mara ya kwanza kwa Arsenal kuwaachia vumbi na kupora mawindo ya mchezaji waliyekuwa wakimsaka kwenye usajili.
Karibu miaka 20 iliyopita, Spurs ilikuwa kwenye mchakato wa kumsajili kiungo Emmanuel Petit kutoka Monaco. Kiungo huyo alikuwa bingwa wa ligi huko Ufaransa na Spurs ilipeleka maombi ya kumsajili, lakini baada ya kuzungumza na Spurs, Petit alipigiwa simu na Arsenal na kukubali kwenda huko kuungana na Arsene Wenger, ambaye aliwahi kumnoa huko Monaco.
Luis Diaz
Porto kwenda Liverpool, 2022
Klabu iliyoporwa: Tottenham
Winga Mcolombia, Luis Diaz alikuwa kwenye rada za Liverpool kwenye dirisha la usajili wa majira ya kiangazi 2022. Lakini, kwenye mchakato huo, Liverpool iliipiku Tottenham wakati inamsajili staa huyo wa zamani wa FC Porto.
Kocha wa Spurs kwa wakati huo, Antonio Conte alihitaji sana huduma ya Diaz ili akaboreshe makali ya safu yake ya ushambuliaji na ilionekana dili hilo linakwenda kukamilika.
Lakini, baada ya Spurs kujivuta na kushindwa kumaliza dili haraka, Liverpool iliingia na kumsajili fasta kwa Pauni 37.5 milioni.
Eyal Berkovic
Maccabi Haifa kwenda West Ham, 1996
Klabu iliyoporwa: Tottenham
Eyal Berkovic jina lake lilikuwa juu sana katikati ya miaka 1990 baada ya kutamba kwa mkopo huko Southampton. Hilo liliwafanya Tottenham kutaka kumnasa jumla kutoka Maccabi Haifa ili akakipige kwenye Ligi Kuu England.
Lakini, akiwa njiani kwenda kusaini mkataba Spurs, Berkovic alipigiwa simu akitakiwa kwenda kukutana na kocha wa West Ham United kwa wakati huo, Harry Redknapp.
Wawili hao walipokutana, Berkovic akashawishika na kusaini kuichezea West Ham. Lakini, Berkovic baada ya kumalizana na West Ham na kukubali kucheza Upton Park bado alienda kuonana na mabosi wa Spurs kwenda kuyaweka sawa na akawafunga kwenye mechi ya kwanza.