Pogba, Sancho wanavyotoa darasa ujenzi wa Manchester United
Muktasari:
- Lakini, wakati huo, hata kabla ya usajili wa Ronaldo, kulikuwa na matumaini makubwa ndani na nje ya Old Trafford. United waliifunga Leeds United mabao 5-1 katika mchezo wa ufunguzi wa msimu, jambo lililoibua matumaini kwamba timu hiyo ingeweza kuwania taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu.
MANCHESTER, ENGLAND: MIAKA mitano ni kipindi kirefu katika soka. Majira ya kiangazi 2021 huko Manchester United sasa yanakumbukwa kama hatua ya mabadiliko katika utawala wa Ole Gunnar Solskjær; uamuzi uliokuja na usajili wa Cristiano Ronaldo ukiwa tukio kubwa lililoifanya kuanza kuelekea kwenye njia isiyo sahihi baada ya miaka kadhaa ya kujenga timu hatua kwa hatua.
Lakini, wakati huo, hata kabla ya usajili wa Ronaldo, kulikuwa na matumaini makubwa ndani na nje ya Old Trafford. United waliifunga Leeds United mabao 5-1 katika mchezo wa ufunguzi wa msimu, jambo lililoibua matumaini kwamba timu hiyo ingeweza kuwania taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza tangu Sir Alex Ferguson alipostaafu.
Baada ya yote, United walimsajili Jadon Sancho aliyekuwa akihitajika zaidi sokoni, na walionekana kumjenga pamoja na Bruno Fernandes na Paul Pogba, ambaye alikuwa mhimili wa ubunifu wa timu hiyo, sambamba na kundi la washambuliaji waliokuwa wakiahidi makubwa.
Sancho alikuwa miongoni mwa wachezaji wa akiba dhidi ya Leeds United, lakini Pogba alikuwa katika kiwango cha juu kabisa cha uwezo wake, akitoa pasi nne za mwisho zilizozaa mabao. United pia walikuwa na Donny van de Beek, aliyesajiliwa kwa Pauni 35 milioni mwaka 2020 kutoka Ajax na ambaye wengi walitarajia angekuwa nyota mkubwa baada ya kung’ara nchini Uholanzi.
Mbali na hao, kulikuwa na wachezaji waliotokea akademi ya klabu hiyo kama Marcus Rashford na Mason Greenwood, pamoja na Anthony Martial. Kama kikosi hicho kilimhitaji Ronaldo au la haikuwa hoja kubwa; kwa vyovyote Solskjær alikuwa na hazina kubwa ya vipaji vya kushambulia. Kwamba wengi wa wachezaji hao wameishia kupotea kwenye ramani ya soka, huku Pogba na Sancho sasa wakiwa hawana timu huenda ni ishara kwamba United hawangeweza kufanikiwa, licha ya nia njema ya Solskjær.
Kocha huyo raia wa Norway, akisaidiwa na Michael Carrick na Kieran McKenna, alijaribu kubadilisha mtindo wa United kutoka kwenye soka la kushambulia kwa kushtukiza hadi mfumo wa kumiliki mpira zaidi na kutawala mchezo. Lakini, baada ya kupata vipigo kadhaa ikiwemo kufungwa nyumbani na wapinzani wao, Manchester City na Liverpool, ilibainika kuwa ilikuwa vigumu kurejesha morali ndani ya chumba cha kubadilishia.
“Tulihitaji kuwa Manchester United. Tusilinde, tusicheze kwa kushambulia kwa kushtukiza, twende nao ana kwa ana, kwa sababu kama sivyo, hakuna maana ya kuwa Man United. Hatukuwa tayari. Hatukuwa wazuri vya kutosha,” anasema Solskjær.
Pogba na Sancho wamekuwa miongoni mwa mifano ya mipango iliyokwenda vibaya katika kipindi cha Solskjær, na kwa miaka mingi baada ya Sir Alex Ferguson kuondoka, United walikuwa wakifukuzia majina makubwa kwa matumaini ya kuuza jezi nyingi na kuvutia watangazaji na wafadhili. Mkakati huo ulifikia kilele katika usajili wa Ronaldo, wakati familia ya Glazer ilipoamini kwamba kumnyakua gwiji huyo wa zamani wa United mbele ya Manchester City kungekuwa ushindi mkubwa kwa mashabiki.
Kutumia Pauni 163 milioni ili kumsajili Pogba na Sancho 2016 na 2021 mtawalia, wakiwa mwanzo na mwisho wa kipindi hicho cha matumizi makubwa, kunaonyesha namna ambavyo uamuzi wa United ulivyokuwa hauna mwelekeo.
Usajili huo uliwasilishwa na United kupitia mitandao ya kijamii kama kurejea kwa wana nyumbani, kaulimbiu iliyotumika wakati wa kutangaza usajili wa Sancho ilikuwa, “hapa ni nyumbani kwako, hapa ndipo unapostahili kuwa.”
Lakini mshambuliaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alionekana kutokuwa tayari kubeba presha iliyokuja pamoja na usajili huo.
Baadaye Solskjaer alifichua kwamba maambukizi ya sikio yalimfanya Sancho alazwe hospitali muda mfupi baada ya usajili wake kukamilika, jambo lililorudisha nyuma maendeleo yake.
“Alikuwa chaguo bora tulilokuwa nalo. Tulitaka kuchukua hatua inayofuata, kubadilisha mtindo wa uchezaji, kuongeza wachezaji katika theluthi ya mwisho ambao wangeweza kuvunja ulinzi wa timu pinzani. Uwezo wa Jadon, namna anavyounganisha mchezo, ulitoa kitu tofauti,” anasema kocha huyo raia wa Norway. “
Mfano rahisi wa kipindi kisichoridhisha cha Sancho huko United ni namna alivyotoka klabuni msimu huu bila shangwe wala kelele kubwa. Winga huyo mwenye umri wa miaka 26 ameachwa kuondoka kimya kimya baada ya mkataba wake kumalizika kutokana na kucheza kwa kiwango kidogo United katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Katika kipindi hicho alipelekwa kwa mkopo Borussia Dortmund, Chelsea na Aston Villa. Sancho hana klabu, na sasa hafuatiliwi tena kwa kiasi kikubwa na vigogo wa soka Ulaya, huku akihusishwa kwa nadra na uwezekano wa kuhamia klabu nyingine za kawaida.
Pogba naye yupo katika hali inayofanana na hiyo, ingawa mazingira yake ni magumu zaidi baada ya kuachwa na Monaco. Alirejea katika klabu yake ya zamani, Juventus, baada ya kuondoka United mwishoni mwa 2021-22, lakini majeraha ya mara kwa mara pamoja na adhabu ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku vilimzuia kucheza mara kwa mara. Hata hivyo, kiungo huyo aliyewahi kushinda Kombe la Dunia sasa ni mchezaji huru tena baada ya kucheza mechi sita pekee Monaco. Je, kuna timu itakayothubutu kumpa nafasi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33?
Rashford alirejea Manchester kwa namna isiyo ya kawaida msimu huu baada ya klabu kuruhusu aende kwa mkopo Aston Villa na Barcelona. Ni Bruno Fernandes pekee katika safu ya ushambuliaji ya United ya Solskjaer aliyebaki Old Trafford tangu 2021 na anayeendelea kufanya vizuri.
Mechi ya mwisho ya Mason Greenwood akiwa United ilikuwa katika msimu wa 2021-22, kabla ya klabu kumsimamisha baada ya kukamatwa kwa tuhuma za ubakaji. Kesi dhidi yake ilifutwa Februari 2023 na baadaye akauzwa Marseille 2024 baada ya kucheza kwa mkopo Getafe, kabla ya kujiunga na Fenerbahce msimu huu.
Martial alishindwa kumpiku Ronaldo na Edinson Cavani katika kupata nafasi ya kuanza katika safu ya ushambuliaji, na hakuwahi tena kuonyesha kiwango bora akiwa United. Kama ilivyo kwa Pogba na Sancho, sasa hana klabu, baada ya mwisho kuchezea Monterrey ya Mexico.
Van de Beek, ambaye United walimuuza kwa Pauni 423,000 mwaka 2024, anajaribu kufufua tena maisha yake ya soka akiwa Girona. Hatima ya wachezaji hawa huenda ikawa somo la tahadhari kwa Carrick, ambaye anaweza kuwa akilitafakari wakati akijaribu kubadilisha mtindo wa uchezaji wa United na kwa mara nyingine kuziba pengo lililopo kati ya klabu hiyo na vigogo wa Ligi Kuu England.