Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TFF inaangaliaje mfumuko wa shule za soka?

ZENGWE Pict


KUMETOKEA hamasa ya ajabu kwa watu mbalimbali kuanzisha shule za soka zinazochukua watoto wa kuanzia miaka mitano hadi chini ya miaka 17.


Hili ni jambo zuri licha ya watu hao kuwa na nia tofauti. Wapo wenye nia hasa ya kutaka elimu ya soka ianze kwa watoto wadogo kabisa na wapo wanaoona suala hilo kama fursa kujipatia kipato.


Yote hayo ni mema kwa sababu mwishowe, soka ndilo linanufaika kwa kupata vijana waliokutana na elimu ya soka tangu wakiwa wadogo na hivyo kulifanya taifa liwe na kundi kubwa la vijana walio tayari kwa mashindano.

Hawa ni watu ambao wanasajili taasisi zao ama Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo lina wajibu wa kusajili vikundi vya michezo au klabu na wengine wanasajili idara nyingine zinazohusika ama na elimu ama na masuala ya watoto.

Hivyo kunakuwa hakuna chombo kilicho juu yao cha kuratibu shughuli zao zaidi ya idara za serikali zinazosajili taasisi hizo. Yaani Chama cha Soka cha Wilaya hakina mamlaka juu ya shule ya soka iliyoanzishwa wilayani kwake hadi viongozi wa taasisi hiyo waombe ushirikiano au wahusishwe kwenye mashindano ya watoto au vijana.

Kwa kuwa umri mdogo ndiyo sehemu sahihi ya kumpa mtoto misingi ya kitu chochote kama mpira wa miguu, kuna haja ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza kuangalia kwa ukaribu mfumuko huu wa shule za soka na kutafuta njia ya kuziratibu.

ZENG 01

Hii ni kwa sababu hizi shule zinaweza kuwa na mafunzo mazuri ambayo yatazalisha kundi kubwa la wachezaji wazuri, ama zikawa na mafunzo ambayo si sahihi tukajenga kundi kubwa la vijana ambao hawakupata elimu nzuri ya soka katika umri mdogo.

Unaweza kukuta watoto wanachezeshwa mazoezi kwenye uwanja mkubwa sawa na vile vinavyotumiwa na watu wazima na kocha haoni tatizo. Wanatumia magoli makubwa badala madogo.

Wengine tunakutana nao barabarani wakikimbia jogging kabla ya mazoezi ya kucheza mpira. Na wengine wanafanya mazoezi ya kucheza mpira tu, hakuna ya kujifunza kupiga pasi, kupokea mpira, kupiga kichwa au mazoezi ya viwanja vidogo (SSG).

Moja kwa moja unagundua kuna hamasa ya kuanzisha shule za soka lakini hakuna makocha sahihi wa kufundisha watoto ili waje kuwa wachezaji wazuri wa baadaye.

ZENG 02

Kwa hiyo ni muhimu sana kwa TFF kuanza kuangalia itawezaje kuratibu shule hizi ili zitoe mafunzo sahihi ya soka kwa kuhakikisha zinakuwa na walimu sahihi wa kufundisha soka kwa ngazi tofauti za umri.

Ni muhimu pia kwa wamiliki wa shule hizi kufundishwa kuhusu umuhimu wa kuwa na mwasiliano mazuri na wadau wakubwa ambao ni wazazi na serikali za mitaa kwa ajili ya masuala mbalimbali ya uendeshaji shule, usalama na masuala mengine muhimu.

Hizi shule zinaweza kusaidia taifa likawa na falsafa yake ya soka iwapo TFF itatafuta njia ya kuziratibu na kutoa mafunzo kwa walimu wa shule hizi ili kuwa na mfumo wa uchezaji utakaoitofautisha Tanzania na nchi nyingine.

Iko hivyo nchini Hispania, Brazil, Ujerumani, Argentina na Italia. Kila nchi ina aina yake ya uchezaji inayotofautiana na nyingine kwa sababu ya falsafa zao zinazoendana na historia na utamaduni wao.

Huwezi kuona ajabu kwa wachezaji wa Kijerumani kuwa wanatumia nguvu nyingi na wenye pumzi kubwa, lakini Brazil ikatofautiana nao kwa kuwa na wachezaji wanyumbufu, wanaotulia na mpira na wajanja kimpira.

Yote hayo hutokana na aina ya mafunzo wanayopata tangu utotoni.

Ndiyo maana naona kuna umuhimu wa TFF kukutana na viongozi wa soka wa wilaya na kukubaliana ni jinsi gani wanaweza kushawishi hizi shule ziwe wanachama ili ione jinsi ya kuzisaidia kiufundi na kutoa mwongozo wa sera ityakayofuatwa na shule zote zitakazokubali kusajiliwa.

ZENG 03

Yaani hapo shule zitakazosajiliwa zitawekewa viwango vya makocha wanaostahili kutoa mafunzo kwa watoto na ikiwezekana vyama husika vitoe mafunzo kwa gharama nafuu kwa watu watakaotaka kujitokeza kufundisha watoto.

Pia kuanza kuweka mkazo katika umri kwa kuwa bado mashindano yanayoshirikisha taasisi hizi huhusisha watoto wenye umri mkubwa tofauti na ilivyokusudiwa na matokeo yake mashindano kupoteza maana iliyokusudiwa na hivyo kutosaidia kukuza vipaji.

Hili litawezekana kama ushirikiano na wazazi utakuwepo na hivyo usajili wa watoto shuleni kuhusisha vyeti vya kuzaliwa. Hali kadhalika mawasiliano kati ya taasisi na shule za kawaida wanazosoma watoto hao yatarahisisha kupata watoto wenye umri sahihi.

Kwa hiyo mfumuko wa shule za soka ni kitu chema kwa mpira wa miguu na hivyo mamlaka zinatakiwa zianze kuangalia zitawezaje kuziratibu ili kuziwezesha kuchangia katika maendeleo ya mpira wa miguu.