TAYLOR SWIFT - Kwa pesa tu, aliufunga mwaka kibabe sana
Muktasari:
- Katika orodha ya wasanii waliopata kiasi kikubwa cha pesa kwa mwaka jana, namba moja alishika Jay Z kisha nafasi ya pili ikaenda kwa mwanadada Taylor Swift anayeimba muziki wa Pop.
PENNSYLVANIA, MAREKANI: MWAKA jana ulikuwa na mambo mengi kwa wasanii wa muziki duniani, kuna wale waliomaliza kwa kuchukua tuzo, wengine walimaliza kwa nyimbo zao kusikilizwa sana na wengine walimaliza na maokoto ya kutosha.
Katika orodha ya wasanii waliopata kiasi kikubwa cha pesa kwa mwaka jana, namba moja alishika Jay Z kisha nafasi ya pili ikaenda kwa mwanadada Taylor Swift anayeimba muziki wa Pop.
Hapa tumekuletea maelezo ya kina jinsi mrembo huyu alivyozipiga pesa na kuwatupa mbali wasanii kibao.
ALIVYOPIGA PESA
Ziara yake ya Eras aliyoimalizia mwaka jana, hadi sasa ndiyo inayoshikilia rekodi ya kuwa ziara ya muziki iliyozalisha pesa nyingi zaidi (Dola 1 bilioni) na kusababisha utajiri wake kukua kufikia Dola 2 bilioni.
Msanii huyu pia alipata pesa nyingi kutokana na uandishi wake wa nyimbo na kati ya Juni 2016 na Juni 2017 aliingiza Dola 50 milioni.
Kabla ya ziara hiyo ya kimuziki miaka yake ya mafanikio zaidi ilitajwa ni 2015 na alipata Dola 170 milioni na Juni 2018 hadi Juni 2019, alipata Dola 185 milioni, huku mwaka 2020 aliingiza Dola 266 milioni.
Tyler ambaye pia ni mfanyabiashara anayemiliki hisa katika kampuni mbalimali, pia ana kampuni yake mwenyewe inayosimamia wasanii na kurekodi nyimbo mbalimbali iitwayo Taylor Swift Productions na inampa zaidi ya Dola 50 milioni kwa mwaka.
Inaelezwa pesa nyingi za mrembo huyu zinatokana na ubalozi wa kampuni mbalimbali zikiwamo AT&T, CoverGirl, Verizon Wireless, Diet Coke, Keds, AirAsia, Qantas, Sony Electronics, Target na Capital One na mwaka jana kutokana na filamu yake ya Eras inayoonyesha matukio yake ya kimuziki sehemu tofauti ilimwingiza jumla ya Dola 205 milioni.
NDINGA
Range Rover
Mercedes-Benz S-Class
Nissan Qashqai
Toyota Sequoia
Ferrari 458 Italia
Porsche 911 Turbo
Audi R8
Maybach S650
Cadillac Escalade
Mercedes-Benz Viano
Mercedes G63
MSAADA KWA JAMII
Mara kadhaa amekuwa akitoa misaada kupitia taasisi mbalimbali za kijamii na mwaka 2023 alisaidia zaidi ya watu 500,000 chakula akiwa na taasisi ya Silicon Valley Food Bank, pia mwaka huo alisaidia watu 120,000 chakula akiwa na taasisi ya Tampa Food Bank.
Staa huyu pia amewahi kuchangia pesa alizopata kutokana na muziki wake wa Ronan ili zitumike kusaidia watu wanaosumbuliwa na kansa.
Kwa mwaka mmoja anakadiriwa kutoa takriban Dola 10 milioni kusaidia jamii.
MJENGO
Amekuwa mwekezaji katika nyumba ambazo baadhi anaishi na nyingine anapangisha ikiwa ni sehemu ya kujipatia pesa.
Kijumla mijengo yake inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 150 milioni na zipo maeneo mbalimbali Marekani ikiwemo Nashville, Rhode Island, New York City, Los Angeles na Massachusetts.
MAISHA NA BATA
Kwa sasa yupo katika uhusiano na mchezaji wa NFL, Travis Kelce ambaye tetesi zilianza kusambaa kuanzia Septemba 2023, kabla ya mambo kuwa hadharani mwezi huo huo baada ya Taylor kuhudhuria moja kati ya mechi alizocheza mchumba wake huyo na akaonekana akishangilia kwa nguvu, baada ya hapo wawili hawa wameonekana sehemu mbalimbali wakijivinjari pamoja.