Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bagamoyo Festival kushirikisha vikundi 146

Muktasari:

Tamasha hilo litafanyika kwa siku nne kuanzia Oktoba 28 hadi 31, 2026, huku likitanguliwa na mkesha utakaofanyika Oktoba 27, 2026.

MWISHONI mwa mwezi Oktoba 2026, Mji wa Bagamoyo unatarajiwa kuwaka moto wa sanaa na burudani, baada ya wasanii na vikundi 146 kutoka ndani na nje ya Tanzania kuonyesha nia ya kushiriki Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, maarufu kama Bagamoyo Festival.

Tamasha hilo litafanyika kwa siku nne kuanzia Oktoba 28 hadi 31, 2026, huku likitanguliwa na mkesha utakaofanyika Oktoba 27, 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 2, 2026, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Gabriel B. Kiiza, amesema maandalizi yanaendelea vizuri huku idadi ya vikundi vilivyoomba kushiriki imefikia 146.

Kwa mujibu wa Kiiza, kati ya vikundi hivyo, 104 vinatoka ndani ya Tanzania, ikiwemo Tanzania Bara na Zanzibar, huku 42 vikiwa vya kimataifa.

“Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo litahusisha shughuli mbalimbali za kisanii, kiuchumi na kijamii, lengo kuu likiwa ni kuvutia wadau na watazamaji kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema.

SANAA KIBAO JUKWAANI

Kwa mujibu wa TaSUBa, Bagamoyo Festival mwaka huu itakuwa na mchanganyiko wa sanaa mbalimbali, jambo litakalowapa mashabiki burudani tofauti ndani ya siku hizo nne.

Wasanii na vikundi watashiriki katika maonyesho ya ngoma za asili na za kisasa, muziki wa asili na wa kisasa, maigizo, sarakasi, ushairi, vichekesho pamoja na mazingaombwe

Kiiza amesema uwepo wa vikundi vya ndani na nje ya nchi unalenga kuifanya Bagamoyo Festival kuwa jukwaa la kukutana kwa tamaduni mbalimbali.

WAFANYABIASHARA NAO WAMO

Mbali na wasanii, wajasiriamali na wafanyabiashara wa sanaa za ufundi nao watapata nafasi ya kuonyesha na kuuza bidhaa zao wakati wote wa tamasha.

Bidhaa zitakazokuwa kwenye maonyesho hayo ni pamoja na batiki, shanga, magauni, hereni, vikapu, ngoma, mashati, picha na michoro ya ubunifu, pamoja na bidhaa za virutubisho na tiba lishe.

“Wataonesha na kuuza bidhaa mbalimbali za sanaa na utamaduni wakati wote wa Tamasha,” amesema Kiiza.

FILAMU NAYO YATINGA

Mashabiki wa filamu nao hawataachwa nyuma, kwani tamasha hilo litakuwa na maonyesho ya filamu kwa siku zote nne.

Filamu hizo zitaonyeshwa katika ukumbi wa wazi wa TaSUBa, unaojulikana kama Open Stage.

Pia taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi zitashiriki kwa kutoa elimu, huduma na fursa mbalimbali za biashara kwa wageni watakaofika kwenye tamasha.

WASANII WAPEWA ELIMU

Bagamoyo Festival haitakuwa burudani pekee, kwani Oktoba 29 na 30 kutakuwa na warsha na mafunzo yatakayolenga kumuinua msanii kupitia kazi mbalimbali za sanaa.

Warsha hizo zitafanyika katika kumbi za TaSUBa na zitawakutanisha wasanii waliofanikiwa kupitia sanaa, washiriki kutoka katika mashirikisho ya sanaa, wasanii wa Bagamoyo pamoja na wanachuo wa TaSUBa.

Kiiza amesema wasanii waliofanikiwa watatumika pia kama waongeaji katika mafunzo hayo.

“Kutakuwa na waongeaji ambao ni wasanii ambao wamepata mafanikio kupitia sanaa,” amesema.

UTALII NAO WAMO

Wageni, viongozi, wasanii na washiriki wengine watapata fursa ya kutembelea baadhi ya vivutio vya kihistoria na utalii vilivyopo Bagamoyo.

Maeneo yaliyopangwa kutembelewa ni pamoja na Mji Mkongwe wa Bagamoyo, Kaole Ruins na Boma la Wajerumani.

Lengo ni kuwawezesha washiriki kupata fursa ya kujionea historia na utamaduni wa Bagamoyo sambamba na kushiriki shughuli za tamasha

CHAKULA NA VINYWAJI

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka Bagamoyo na maeneo mengine watatoa huduma ya chakula na vinywaji kwa wasanii, wageni na wananchi watakaohudhuria.

TaSUBa imesema wageni watapata nafasi ya kula vyakula mbalimbali na kufurahia vinywaji vya asili vya Kitanzania vitakavyopatikana wakati wote wa tamasha.

WAGENI RASMI BADO SIRI

Pamoja na maandalizi hayo, TaSUBa bado haijaweka wazi majina ya wageni rasmi watakaofungua tamasha hilo wala atakayekuwa mgeni rasmi kwenye kilele.

“Uthibitisho wa uwepo wake utakapofahamika tutaufahamisha umma,” amesema Kiiza kuhusu mgeni rasmi wa ufunguzi.

Aidha, viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, wizara nyingine za Serikali, Ofisi za Serikali, balozi, mashirikisho ya sanaa, taasisi binafsi, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na viongozi wa taasisi na kampuni mbalimbali wanatarajiwa kuhudhuria.